Rais Magufuli akiwa na Waziri Mkuu Majaliwa Wakiteta Jambo |
Dk Magufuli alitua Ikulu ya Chamwino, Novemba 17 kwa kutumia usafiri wa barabara akisafiri kwa zaidi ya kilometa 300 kwenda katika Makao Makuu ya Serikali ambako kwanza alikuwa na majukumu mawili makubwa.
Novemba 19, mwaka huu, alimteua Mbunge wa Ruangwa mkoani Lindi, Majaliwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu na siku iliyofuata alimwapisha katika Ikulu hiyo iliyoko takribani kilometa 40 kutoka Dodoma Mjini.
Aidha, baada ya kumwapisha Majaliwa asubuhi, jioni hiyo ya Novemba 20, Dk Magufuli aliyeingia madarakani Novemba 5, mwaka huu, alilihutubia na kulizindua Bunge la 11 mjini Dodoma katika hotuba iliyosisimua wabunge na Watanzania kwa ujumla kwa kugusa kero na mipango mbalimbali anayokusudia kuifanya.
Dk Magufuli alirejea Dar es Salaam huku tetesi zikiimarika kwamba atatangaza baraza lake la mawaziri siku yoyote kuanzia jana, na aliondoka Dodoma kwa ndege majira ya saa mbili asubuhi.
Kuwapo kwake kwa siku nyingi katika kijiji cha Chamwino akifanya kazi, kulipongezwa na wanakijiji hao. Aidha, wanazuoni na wanasiasa walitafsiri uwapo wake kijijini hapo kuwa ni kujichimbia asibughudhiwe wakati akipanga baraza lake la mawaziri na mfumo wa uendeshaji mpya wa baraza hilo.
Na ishara au dalili kwamba Baraza la Mawaziri limeiva au litatangazwa wakati wowote ni hatua ya Dk Magufuli kutua Dar es Salaam na baadaye mchana kwenda ofisini kwa Majaliwa ambako ni jirani na Ikulu ya Magogoni.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Rais atateua Baraza la Mawaziri kwa kushauriana na Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, hivyo kuna kila dalili wawili hao kama sio wote watatu, wameshafanya kazi hiyo.
Ofisi ya Waziri Mkuu ilithibitisha Dk Magufuli kutinga ofisini kwa Waziri Mkuu, Majaliwa na kufanya mazungumzo ya takribani saa moja.
“Rais aliingia ofisini kwa Waziri Mkuu Majaliwa majira ya saa tisa na kulakiwa na mwenyeji wake na baadaye walikaa kwa mazungumzo yao wawili tu.
“Baada ya mazungumzo hayo, Rais alizungumza kwa muda mfupi sana na makatibu Muhtasi wa Waziri Mkuu kabla ya kuondoka kuelekea Ikulu,” ilieleza taarifa fupi ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mapema wiki hii, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa Rais akishakamilisha kazi hiyo ya kuteua Baraza la Mawaziri waandishi wa habari watajulishwa ili waupashe habari umma wa Watanzania.
Akilihutubia Bunge na wakati akiwa katika mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi Mkuu, Dk Magufuli aliahidi kuunda Baraza la Mawaziri dogo ikiwa ni mojawapo ya njia za kudhibiti matumizi ya serikali kwa nia ya kutafuta majawabu ya kero za wananchi kwa kasi inayostahili.
Na hilo tayari limeonekana katika hatua kadhaa ambazo amezichukua tangu aingie Ikulu. Alianza kwa kusitisha safari za nje zisizo na umuhimu mkubwa, sherehe za Uhuru na kuzipa mwelekeo mwingine kwa mwaka huu na pia kusitisha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi.
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, maamuzi mazito kuhusu namna anavyotaka nchi iende yamefanyika ikiwa na kuhimiza ukusanyaji wa kodi kwa kufanya ziara ya kushtukiza Hazina na pia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alivunja Bodi kabla ya kutumia fedha za sherehe za uzinduzi wa Bunge (mchapalo) kiasi cha Sh milioni 225 kutumika kuboresha hali ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
Post a Comment