TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imebanwa mbavu ikitakiwa kutoa hadharani Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa uandikishaji wa wapigakura ulivyofanyika nchi nzima.
Sambamba
na kibano hicho mbele ya waandishi wa habari jana, Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) kilirudia msimamo wake wa kuyatangaza matokeo ya urais kabla ya Tume hiyo
kwa kuwa kura zinahesabiwa vituoni na matokeo kubandikwa kabla ya
kuwasilishwa kituo kikuu cha tume kwa ajili ya majumuisho.
Naibu
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika alisema kwamba chama hicho ambacho
safari hii kinashirikiana na vyama vingine vitatu chini ya muungano wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kimeshaamua kutozembea kwa namna
yoyote ile kuhusu matokeo ya uchaguzi mwaka huu.
“Mabere
Marando alishasema kuwa mwaka huu tutatangaza wenyewe matokeo kabla ya
Tume kwa kuyajumlisha kutoka katika vituo vya kupigia kura nchi nzima,
msimamo wetu bado ni hai tutatangaza wenyewe hata kama watasema ni
uchochezi,” amesema.
Marando
ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na wakili maarufu wa Mahakama
Kuu nchini, alitoa kauli hiyo iliyonukuliwa na gazeti la MAWIO, wakati
akielezea maandalizi ya UKAWA katika kudhibiti uchakachuaji wa matokeo.
Kwa
mujibu wa sheria za Tanzania, hakuna haki ya kuhoji matokeo ya urais
wakati wa uchaguzi mkuu. Haki hii imekuwa moja ya madai ya vyama vya
upinzani nchini kwa muda mrefu.
Mnyika
ambaye alikuwa mbunge wa Ubungo, safari hii akigombea jimbo jipya la
Kibamba lililochomolewa ndani ya Ubungo, alitoa uzoefu wa jimboni kwake
ambako mwaka 2010, alitangaza matokeo ya kura zake kabla ya Tume baada
ya kuona mpango wa kumuibia ushindi wake.
“Kutangaza
matokeo kabla ya tume ndio jambo lililonisaidia kutoporwa ushindi wangu
2010. Kile kilichotuokoa Loyola (eneo la kutangazia matokeo ya Ubungo)
ni sisi kutangaza matokeo kwa wananchi na kuishinikiza tume iyatangaze
pia,” alisema.
Msimamo
huo unasisitizwa na CHADEMA wakati tayari Mwenyekiti wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva ameshasema watatangaza matokeo
ya urais ndani ya siku tatu (saa 72) na utaratibu utakuwa kura
kuhesabiwa kituoni, matokeo yake kubandikwa kituoni na nakala itaskaniwa
na kupelekwa kituo kikuu cha Tume.
“Hakutakuwa
na wizi wa kura katika uchaguzi wa mwaka huu. Hao wenye wasiwasi kwamba
kura zao zitaibiwa kama wanajua mianya ya wizi wa kura waje walete
taarifa na tume itatumia mamlaka yake kuzima mianya yote, si kwa zege tu
bali hata kwa kutumia nondo,” alisema Jaji Lubuva.
Jaji
Lubuva amekuwa akisema kwamba safari hii kumewekwa utaratibu wa
kiteknolojia usiotia shaka wa kuzidhibiti kura dhidi ya uwezekano wa
kuchakachuliwa na kwamba wamedhamiria kutangaza matokeo vituoni hata ya
urais ili kuondoa hofu na kuwawezesha wananchi kurudi kwenye shughuli za
ujenzi wa taifa.
Mnyika
katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika eneo la Ngome ambako
ndiko makao makuu ya UKAWA kwa ajili ya uchaguzi, alisema wakati umefika
Tume itoe orodha ya wapigakura na kujiandaa kuondoa hitilafu
zitakazobainika.
“NEC
imetangaza jana wapiga kura wote ni milioni 23.7 lakini maelezo yao
wanadai idadi kamili itafahamika kadri muda na uhakiki unavyoendelea.
Huu ni mkanganyiko, tunatoa wito watoe rasmi orodha ya wapiga kura kwa
vyama vya siasa,” alisema.
Alisema
panahitajika kuundwa tume shirikishi inayohusisha vyama vyote ambayo
itakagua orodha ya wapiga kura na kuona kama kuna utata wowote ili
utatuliwe.
Mnyika
alieleza kuwa uandikishaji kwa mfumo mpya wa kielektroniki (BVR) na
hata uhakiki wa majina umetawaliwa na utata na “inaonekana tayari tume
inalo daftari lake ambalo vyama kama wadau wa kwanza wa uchaguzi huo
hawana mpaka sasa.”
Tume
imetangaza kwamba uchaguzi huu utakuwa na vituo 72,000 natayari vifaa
vya uchaguzi vimewasili nchini, zikiwemo karatasi za mfano huku Jaji
Lubuva akisema karatasi halisi zitaletwa nchini wiki moja kabla ya
Oktoba 25 na kudhibitiwa na Tume yenyewe kwa ajili ya usalama.
Post a Comment