PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: LOWASSA: Asanteni Chato Kwa Mahaba Yenu.....Mnanifanya Nideke
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katib...


Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa), ameipenya ngome ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, wilayani kwake Chato na kupata mapokezi makubwa.

Mkutano wa jana ulikuwa wa kwanza kufanyika mjini hapo akiwa ametokea Morogoro, mkutano mwingine aliufanya mjini Geita.

"Nikiutazama huu umma nashtuka sana, hapa ni nyumbani kwa Magufuli. Wazanzibari wanasema haya ni mahaba nami nayapokea. Mnanifanya nideke na hapa ni nyumbani kwa Magufuli, watakaonipa kura wanyooshe mikono juu...mikono namna hii inanipa faraja, nimepokea mahaba yenu," alisema Lowassa.

Akizungumzia matatizo elimu Chato alisema atapiga marufuku michango ya wanafunzi na kuanzia Januari watoto wote watasoma bure na elimu bora.

Alisema hatasahau kilimo na akasema wakulima wataruhusiwa kuuza mazao yao popote wanapotaka bila kubugudhiwa.

Alisema atahakikisha pia wakazi wa Chato wanapata maji toka Ziwa Victoria kama alivyowafanyia wakazi wa Mkoa wa Shinyanga ambao wanapata maji toka ziwa hilo.

Aidha, alisema atafufua kiwanda cha kuchambua pamba kichopo wilayani hapa ambacho kimekufa wakati wa CCM.

Wakazi hao walimuahidi kura za ndiyo na kumuangusha Dk. Magufuli mapema asubuhi Oktoba 25, mwaka huu.

Alifanya mkutano huo katika eneo la stendi ya zamani ya mabasi mjini hapa jana.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema wapinzani hawana nia ya kuleta vita na vurugu.

"Sisi hakuna vita, tutawaondoa CCM kwa amani kabisa," alisema na kuongeza: "Chini ya CCM hakuna maendeleo."

Aidha alimtaka Dk. Magufuli kutoka CCM kama anaona kitanda chao kina kunguni na yeye hawezi kukilalia.
Mapema Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alisema yupo tayari kurudi tena mahabusu ya Segerea tena na tena hadi Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema lengo la serikali kumbambikia kesi na kumnyima dhamana, ilikuwa ni kuwatisha wananchi ili wakiona waziri mstaafu kama yeye anapelekwa mahakamani na Segerea, watishike na kuingiwa na woga zaidi ili waachane  na Ukawa.

"Lengo lilikuwa watu waone mimi kama waziri mstaafu na mwanasheria maarufu nimefunguliwa mashitaka, wananchi waogope kujiunga na Ukawa," alisema.

Aliwaomba wakazi wa hapa hata kama wanaipenda CCM kukumbuka hali itakavyokuwa kwa watoto wao chini ya CCM.

Alisema wakumbuke pale wanapokwenda hospitali na kukosa dawa, watoto wao kukosa elimu na ajira, hivyo matatizo hayo yawafanye kuachana na CCM.

Alisema serikali atakayoiunda Lowassa itakuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza kuliko ilivyo kwa Serikali hii ya CCM.

Alisema Dk. Magufuli haijui CCM kwa sababu hajawahi kuwa hata balozi wa nyumba kumi, hivyo hawezi kuwa kiongozi.

Alisema alijiunga na CCM mwaka 1991, lakini akiikumbuka CCM ya wakati huo na hii iliyoshika dola sasa, hazifanani kabisa.

"Kilichobaki kwa CCM hii ya sasa ni rangi ya kijani, alama ya rangi ya njano za jembe na nyundo, basi.

"Hiki siyo tena chama cha wakulima na wafanyakazi, ni chama kilichokosa maadili ya uongozi kiasi cha kuwasafisha watuhumiwa wa Escrow na Epa.

"Ilifikia hatua sisi nafsi zetu zilitusuta, nikiwa nawaangalia watoto wangu nilikuwa napata uchungu kuhusu hatma yao chini ya dola ya CCM,"alisema.

Bila kuwataja majina, alisema CCM imewapitisha baadhi ya wanachama  wao waliokuwa wakituhumiwa na ufisadi wa Escrow na EPA kugombea ubunge.
Kwa upande wake, Richard Tambwe Hizza, alisema huu ni mwaka ambao Mungu ametaka Lowassa awe rais.

Alisema Ukawa wana uwezo wa kuwaletea wananchi maendeleo tofauti na CCM.

'Mkitaka kujua CCM ni watu wa ovyo, mliona jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wote walivyoimba, 'Tuna imani ni Lowassa, lakini Rais Jakaya Kikwete, hakutaka kuwasikiliza," alisema.

Aliwataka wananchi wasigombane huko mitaani bali waelimishane.

Alisema hawawezi kuwaacha Watanzania wakiwa katika hali mbaya namna hii.

Alisema amezunguka nchi hii na kuona jinsi watu wanavyomkubali Lowassa utadhani walikuwa wanaishi nyumba moja.

"Mwaka huu Nyerere atafufuka na kumshuhudia Lowassa akiapishwa kuwa rais," alisema.

Alisema wananchi watakaoipigia kura CCM Oktoba 25, atatakiwa kujipima kwa kwenda hospitali.

Katika hatua nyingine, aliyejitambulisha kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania Wilaya ya Chato, Lucas Michael, alipanda jukwaani na kusema katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato, ndiyo pekee ambayo walimu wanalazimika kujinunulia chaki.

Alisema walimu wilayani humo wananyanyasika na hata walimu wastaafu wanashindwa kurudi makwao baada ya halmashauri kushindwa kuwapatia fedha za nauli.

Aliwataka walimu wenzake mbali na kufundisha popote walipo wasiwe waoga, wawafundishe wanafunzi ukweli.

"Walimu kokote kule mliko kafanyeni uamuzi sahihi, bila woga na wakati ndiyo huu wa kufanya maamuzi ya mabadiliko," alisema.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Chato, Dk. Benedickt Lukanima, alimweleza Lowassa kuhusu matatizo ya maji ingawa wana ziwa, matatizo ya elimu bora kwa watoto wao na dawa hospitalini.

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema wamekubaliana na wenzake kurudi tena hapa kuzungumza mambo ya Chato.

Hata hivyo, wananchi walipaza sauti zao wakimtaka azungumze wakati huo naye akasema, namna pekee ya kuing'oa na kuizika CCM ni lazima ianzie hapa Chato.

"Ili nchi hii  iishi, tunahitaji kuizika CCM na mahali pa kuanzia ni hapa Chato," alisema.

Huku baadhi ya vijana wakiwa wanapitisha mfano wa jeneza lililokuwa limezungushwa bendera ya CCM, Lissu alisema Ukawa wamekuwa wakipata matusi na kejeli nyingi na namna pekee ya kuiondoa madarakani ni kumng'oa Dk. Magufuli na kuizika CCM.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top