Rais Kikwete na Lowassa kulia.
Dar es Salaam. Ndivyo alivyosema na bila shaka ndivyo anavyoamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini kauli ambazo amekuwa akizitoa tangu kuanza kwa mbio za urais zinamuweka katika hali ngumu Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Lowassa alirudia moja ya kauli hizo juzi alipokuwa Dar es Salaam kuendelea na kazi ya kutafuta wadhamini aliposisitiza kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa “Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje,” akisisitiza kuwa yeye ndiye anayeweza kuleta mabadiliko hayo.
Mbunge huyo wa Monduli ametoa kauli hizo kabla ya vikao vya juu vya kufanya uamuzi wa mgombea urais wa CCM vitakavyoongozwa na Rais Kikwete. Vikao hivyo vitaanza Julai 8.
Tayari makada 42 wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya chama hicho kikongwe kugombea urais na kutoa ahadi mbalimbali, lakini Lowassa, ambaye amekuwa akipata wadhamini wengi kuliko makada wengine, ndiye ambaye ametoa kauli zinazomuweka Kikwete kwenye hali ngumu.
Tangu alipoanza kuzungumzia urais kwenye kikao cha kwanza na wahariri Mei 25 mjini Dodoma, Lowassa amekuwa akitoa kauli kadhaa katika mikoa mbalimbali nchini, akianzia Arusha ambako alitangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM na baadaye kwenye harakati za kusaka wadhamini.
Asiyenipenda ahame CCM
Akijibu swali kwamba anaweza kuhama chama iwapo jina lake litakatwa kwenye mchakato wa ndani ya CCM, Lowassa alieleza jinsi alivyokitumikia chama na imani yake.
“Sina mpango wa kuhama chama changu, sina Plan B. Mimi ni Plan A tu. Tangu nimalize chuo kikuu mwaka 1977, nimekuwa mwana-CCM. Sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha. Maisha yangu yote ni CCM,” alisema Lowassa.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiyo ahame, siyo mimi.”
Safari hii JK ataniunga mkono
Akihutubia maelfu ya wananchi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mei 30 wakati akitiania, Lowassa alielezea tukio la kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kuwania urais mwaka 1995 wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Kikwete, ambaye pia alichukua fomu hizo.
“Wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Pamoja tulikwenda kuchukua fomu na baadaye kwa pamoja tukazungumza na waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati yetu, mwenzake ambaye hangefanikiwa angemuunga mkono mwingine,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa wakati ule alimuunga mkono Kikwete...“Natarajia safari hii, Kikwete ataniunga mkono.”
Mwaka huo, Kikwete alishindwa na Benjamin Mkapa ambaye baadaye akawa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Mwaka 2005, Lowassa hakuchukua fomu na badala yake alimuunga mkono Kikwete aliyeshinda na mbunge huyo wa Monduli kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Pengine kauli hiyo ya Lowassa kutaka amuunge mkono ndiyo iliyosababisha Rais Kikwete kutupiwa swali na mwanadiplomasia wa Marekani Juni 9 wakati akizungumza na Jumuiya ya Watanzania waishio Uholanzi katika hoteli ya Chawnie Plaza. Rais Kikwete alijibu kuwa hana mtu wake na kwamba wote ni wagombea wake, na kama ni suala la kuchagua, ana kura moja tu kama wajumbe wengine.
Mabadiliko aliyotabiri Nyerere
Akiwa mjini Iringa Juni 20, Lowassa alitumia kauli hiyo ya Nyerere kuhusu mabadiliko ndani na nje ya CCM.
“Baba wa Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisema Lowassa.
“Huu ni wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga inaweza kuleta mabadiliko na mtu wa kuleta mabadiliko hayo ni mimi,” alisema Lowassa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa.
Pia aliwaambia wahariri mjini Dodoma kuwa hawezi kuondoka CCM na kama kuna watu wanadhani hivyo, waondoke wao. Alikuwa akijibu swali kama atakuwa tayari kuondoka CCM iwapo ataenguliwa kwenye mchujo wa wagombea urais.
Hakuna wa kumkata jina
Juni 22, akizungumza mara baada ya kuwasili mkoani Ruvuma alisema hatarajii jina lake kukatwa katika vikao vya CCM vitakavyoketi kumteua mwanasiasa atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais.
“Nimekuwa mwanaCCM tangu mwaka 1977 nilipomaliza chuo kikuu, sijawahi kufanya kazi nje ya CCM hivyo nakijua chama na hakuna mgombea atakayeweza kuvunja rekodi ya utendaji wangu katika chama, sasa leo anayetaka kukata jina langu anatoka wapi? Anakata kwa sababu gani? Sioni kosa la kukatwa jina na Watanzania hawaoni, kwa hiyo msiwe na wasiwasi jina litarudi tu,” alisema Lowassa.
Anayemtuhumu kwa ufisadi amtaje
Siku ya kuchukua fomu Juni 5, Lowassa alijibu kwa kifupi maswali ya wanahabari na kusema kama kuna mtu ana ushahidi wa tuhuma za ufisadi dhidi yake amtaje jina.
“Kama hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme na anitaje. Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za matusi ila tu zijengwe hoja.
CCM ikijipanga itashinda
Juni 25, akiwa mjini Babati kutafuta wadhamini, Lowassa alisema iwapo CCM itajipanga vizuri, ikamaliza migogoro na kujiamini, itashinda mapema katika uchaguzi.
“Tukijipanga vizuri, tukajiamini tukaacha magomvi katika umoja wetu huu, tutashinda uchaguzi mapema dhidi ya watani wetu.”
Kwa kujipanga, Lowassa alikuwa akimaanisha kumteua yeye kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akisema kufanya hivyo kutamaliza uchaguzi mapema.
Alichokisema Dar
Akiwa Dar es Salaam juzi kusaka wadhamini alirejea kauli ya Mwalimu Nyerere ya mwaka 1995 kwamba mabadiliko yasipopatikana ndani ya CCM, yatatafutwa nje ya chama hicho.
Kutokana na kauli hizo ni wazi kuwa rais Kikwete atakuwa katika mtihani mzito wakati atakapokuwa akiendesha vikao vya chama hicho vya kupata mgombea urais.
Kwa mujibu wa ratiba za CCM, kikao kitakachoanza kitakuwa na Usalama na Maadili kitakachofanyika Julai 8 na kufuatiwa na Kamati Kuu Julai 9 ambayo itawachuja wagombea hao 42 na kubaki watano ambao majina yao yatawasilishwa Halmashauri Kuu (NEC) Julai 10 kuchuja wagombea hao na kubaki watatu watakaopigiwa kura na mkutano mkuu kumpata mmoja. Mkutano mkuu utafanyika Julai 11 na 12.
Vikao vyote isipokuwa cha Usalama na Maadili vitaongozwa na Rais Kikwete.
Jambo jingine linaloonekana kukitesa chama hicho katika kupitisha mgombea ni idadi kubwa ya wana-CCM wanaojitokeza kumdhamini waziri mkuu huyo wa zamani.
Kwa mujibu wa taratibu za chama hicho kila mgombea urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama 30 katika mikoa 15 nchini ili kufikisha idadi ya wadhamini 450, lakini Lowassa amekuwa akipata wanachama hadi 50,000 wanaotaka kumdhamini katika baadhi ya mikoa.
Makada, wasomi wazungumzia kauli
Pius Msekwa alisema chama kikongwe kama CCM hakiwezi kutishika kwa kauli kama hizo ambazo zinaweza kuwa na tafsiri tofauti kwa wananchi wa kawaida ambao hawafahamu taratibu za chama wanaoweza kuamini kuna watu wanaonewa.
Alisema kwa taratibu za chama, mgombea anatakiwa kueleza sera zake atakachowafanyia wananchi, lakini akiwa anatoa kauli za vitisho anakuwa kero kwa wanaomsikiliza kwani haziwasaidii.
“Sidhani kama ni kauli nzuri, kinachotakiwa wagombea wanadi sera zao na wasubiri kupitishwa na kamati itakayokaa kwa ajili hiyo badala ya kutamka kauli zisizokuwa na tija wala faida kwa mwananchi wa kawaida, ”alisema Msekwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Frank Tilya alisema ameshangazwa na tabia hiyo ya wagombea wa CCM iliyoibuka kabla ya taratibu za uchaguzi kutangazwa kwani huko nyuma haikuwapo.
Alisema anachofahamu CCM ina taratibu zake za kupata wagombea kwa kuwachuja, hivyo kauli hizo zinaonyesha kuingilia mamlaka hizo na wanaozisimamia.
Alisema ameshangazwa na kinachojitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu wagombea wa CCM badala ya kutangaza nia na kuomba wadhamini wao wanafanya kampeni kabisa utafikiri wameshapitishwa.
“Hii ni hatari kwa siasa, watu kufanya mambo kwa kutokuzingatia taratibu siyo jambo jema, nahisi kuna kitu hakipo sawa huko, wanapaswa wajichunguze na kuacha wahusika wafanye kazi yao badala ya wao kuwa majaji,” alisema Dk Tily.
Mhadhiri wa UDSM, Dk Benson Bana alisema anayachukulia hayo kama majigambo ya wanachama kutafuta nguvu na kujiamini na kwamba haoni kama kuna shida, kwa sababu mwisho wa siku watajulikana nani anabaki na nani anaondoka katika kinyang’anyiro hicho.
“Ninachoomba kifanyike hapa ni kamati kufanya kazi yake bila kupindapinda wala kumuogopa mtu, kwani inaonekana wazi kuna ambao wanajinadi wakiwa na lengo la kutafuta nafasi huko mbele ya safari ili wasiachwe na atakayeshinda, kutengeneza historia katika maisha yao, pia wapo wenye nia ya kweli,” alisema Dk Bana.MWANANCHI
Post a Comment