UKOSEFU wa elimu ya uzazi wa mpango bado
ni changamoto kubwa kwa wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu
mkoani Shinyanga, hali ambayo imekuwa ni chanzo cha wanawake kutotumia
njia za uzazi wa mpango na kusababisha vifo vitokanavyo na uzazi.
Mbali na vifo pia idadi ya wasichana
wanaobeba mimba katika umri mdogo imekuwa ikiongezeka , licha ya kwamba
mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa ambayo iko mstari wa mbele
kuhamasisha kampeni ya wanawake kujiunga na uzazi wa mpango, lakini bado
juhudi hizo hazijaleta mabadiliko makubwa.
Pamoja na kuwahamasisha wakina mama
kuzingatia uzazi wa mpango ili kusaidia kupunguza tatizo hilo pia
kuwashirikisha wanaume katika masuala ya uzazi wa mpango, hata hivyo
tatizo linaonekana kuendelea kuwepo huku nchi ya Tanzania ikiwa ni moja
ya nchi ambazo zina viwango vya juu vya vifo vya wanawake vitokanavyo na
matatizo ya uzazi.
Elimu ya uzazi pia inahitajika kutolewa
kwa jamii kwa kushirikisha makundi ya vijana ambao ndiyo wako katika
kipindi ambacho wanaweza kujiingiza katika mahusiano, matokeo yake
wanabeba mimba katika umri mdogo na maisha yao yakawa katika hatari ya
kupoteza maisha wakati wakujifungua.
Wataalamu wa afya.
Mtaalamu wa masuala ya uzazi wa mpango mkoani Shinyanga Anna Mwalongo, anasema wasichana wanaobeba mimba chini ya miaka 20 ni tatizo kubwa kwani anaweza kupoteza maisha yeye na mtoto, kutokana na viungo vyake vya mwili havijakomaa kuweza kuhimili mzigo atakao kuwa nao.
Mtaalamu wa masuala ya uzazi wa mpango mkoani Shinyanga Anna Mwalongo, anasema wasichana wanaobeba mimba chini ya miaka 20 ni tatizo kubwa kwani anaweza kupoteza maisha yeye na mtoto, kutokana na viungo vyake vya mwili havijakomaa kuweza kuhimili mzigo atakao kuwa nao.
Anasema kama watu watabadilika na kuanza
kutumia uzazi wa mpango vifo vya watoto wachanga vitapungua kwa
asilimia 20, pia vifo vya wakinamama vitokanavyo na matatizo ya uzazi
vitapungua kwa asilimia 44,hivyo ni vema wakaelimishwa pia madhara ya
kubeba mimba katika umri mkubwa kuanzia miaka 35.
Anabainisha kuwa uzazi wa mpango ni njia
nzuri ambayo itasaidia kupunguza vifo vya wakinamama wakati wa
kujifungua ,sanjari na kuwawezesha wanawake ambao wanakuwa hawajaamua
kupata watoto kujipanga vizuri, pamoja na kuzuia mimba zisizotarajiwa
hususani kwa wasichana ambao hawajatimiza miaka 20.
Mwalongo anasema, kila mwaka takwimu
zinaonyesha wanawake 454 kati ya 100,000 hufariki , ambapo kati ya
watoto 1000 watoto 51 wanafariki kiwango ambacho bado ni kikubwa
kinahitaji juhudi zaidi kukabiliana na changamoto hiyo .
Anaeleza kuwa, pamoja na kuhamasisha
matumizi ya njia za uzazi wa mpango pia jamii inahitaji kupatiwa elimu
juu ya umuhimu wa wakinamama wajawazito kuwahi kwenye vituo vya afya,
hatua itakayosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuchangia kukuza
uchumi wa wananchi na taifa.
Naye mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga
Dkt. Ntuli Kapologwe anasema asilimia 80 ya vifo vinatokana na matatizo
ya uzazi, kutokana na wakinamama wajawazito kuchelewa kufika kwenye
vituo vya afya pamoja na wasichana kuzaa katika umri mdogo kuanzia miaka
14.
Anasema uzazi wa mpango unasaidia
kupunguza vifo vya wajawazito iwapo wanawake watahamasika na jamii kwa
ujumla kutumia njia hizo, ambazo zitasaidia kuimarisha afya ya mama na
mtoto na kupanga uzazi uliosalama kwa kuwa na afya bora.
Mganga mkuu Dkt Kapologwe anabainisha
kuwa, mwaka jana 2014 wakinamama wajawazito 64 walipoteza maisha
kutokana na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutojifungulia
hospitali, huku wengine wakida wanaona aibu kuzalishwa na wauguzi wenye
umri mdogo.
Dkt Kapologwe anasema katika uchunguzi
waliofanya walibaini kuwa mila na desturi zilizopitwa na wakati
zinachangia kuendelea kutokea vifo vya wakinamama wajawazito, kwani
takwimu zinaonyesha nusu yao ndiyo wanajifungulia hospitali ama kwenye
vituo vya huduma na wengine majumbani au kwa wakunga wajadi.
“Kama wakitumia vizuri njia ya uzazi wa
mpango wanaweza kupunguza na kuzuia vifo vya akina mama na watoto kwa
asilimia 25,mikakati iliyopo ni kushirikiana na halmashauri zote
wakiwemo wadau mbalimbali na kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa uzazi
wa mpango ” anasema Kapologwe
Anasema kuwa, asilimia 24 tu ya wanawake
wote hutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango, huku asilimia 27 ni kwa
wanawake walioolewa na wengine wanatumia njia za asili za uzazi ,ambapo
bado changamoto ni kubwa.
Mkoa wa Shinyanga unakadiriwa kuwa na
vijana 625,000 ambao wanahitaji kupatiwa elimu ya uzazi wa mpango,
wanaoanzia umri wa miaka 15 hadi 19 ni 161963 huku waliowengi wamekwisha
olewa na asilimia 33 tayari wana mimba katika umri mdogo.
Mratibu msaidizi wa huduma za afya ya
uzazi na mtoto wa wilaya ya kishapu Suzana Kulindwa anabainisha kuwa ,
idadi kubwa ya wasichana wanabeba mimba kuanzia miaka 14 hadi 19 umri
ambao ni mdogo kuweza kuhimili.
Anasema mwaka 2013 wanawake 13,373
walihudhuria kliniki na kati yao 2,562 walikuwa na umri wa chini ya
miaka 20 ikiwa ni sawa na asilimia 19.1, ambapo kipindi cha Januari na
Juni mwaka jana wanawake 1,370 wenye umri wa chini ya miaka 20
walihudhuria Kliniki sawa na asilimia19.9 wakiwa wajawazito.
Anabainisha kuwa, kuanzia Januari hadi
Juni mwaka 2014, kati ya wanawake 6,871 waliohudhuria 1,370 walikuwa na
umri wa chini ya miaka 20, hali inayoweza kusababisha kutokea vifo
vitokanavyo na uzazi ambapo watu wangetumia njia za uzazi wa mpango
changamoto isingekuwepo.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa mwaka
2010 na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) karibu wanawake 20 hufariki
kila siku kutokana na matatizo ya uzazi,huku mkoa wa Shinyanga wanawake
64 walipoteza maisha mwaka jana. Kutokana na hali hiyo nchi imejiwekea
malengo ya kupunguza kiwango cha vifo kutoka 454 kwa kila wanawake
100,000 hadi 193 ifikapo mwaka 2015.
Wanawake
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya kata ya Bubiki na Itilima ulibaini changamoto kubwa iliyopo ni umbali wa vituo vya kutolea huduma,jambo ambalo linasababisha wanawake wajawazito kujifungulia njiani wakati wakifuata huduma.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya kata ya Bubiki na Itilima ulibaini changamoto kubwa iliyopo ni umbali wa vituo vya kutolea huduma,jambo ambalo linasababisha wanawake wajawazito kujifungulia njiani wakati wakifuata huduma.
Anjelina Yohana (30) mkazi wa kata ya
Bubiki anasema wakati wa ujauzito wa mtoto wake wa tatu, alianza kuumwa
uchungu na kulazimika kusafiri umbali wa saa moja mpaka kufika huduma
ilipo huku akiwa amepakizwa kwenye baiskeli.
“Tulifika kwenye huduma ya afya
nikajifungua ila kwa bahati mbaya mtoto alifariki muda mfupi ,wataalamu
walisema ni kutokana na kuchelewa kufika kwenye huduma kwa kuwa kituo
kilikuwa mbali kisha walirudi nyumbani waliporuhusiwa na
daktari”anaeleza.
Anasema kutokana na mkasa huo alioupata
anaiomba serikali kuboresha huduma zake kwa kusogeza karibu na jamii
zikiwemo njia za uzazi wa mpango,kutokana na wanawake wengi kushindwa
kutumia kwa kukosa ushauri, yeye akiwa ni miongoni mwa wanawake ambao
hawatumii njia yoyote.
Sara Marco (27) na Paulina Herman (39)
kutoka kijiji cha Ikoma kata ya Itilima wanasema umbali wa huduma ni
changamoto kubwa, ambayo imekuwa inasababisha na hofu ya maisha yao
pindi wanaposhika ujauzito na kuamua kuendelea kutumia njia za uzazi wa
mpango ili kuzuia mimba.
Wanasema wanatumia njia za uzazi wa
mpango ambazo zimewasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha afya
zao, huku tatizo kubwa likiwa ni umbali wa huduma za afya na kusababisha
wanawake kujifungulia njiani wakati wakieleka hospitali jambo ambalo ni
hatari.
Umefika sasa wakati kwa serikali
kuchukua hatua za dharura kukabiliana na changamoto zilizoko vijijini
kwa kuboresha huduma za afya na kuwahamasisha wanawake kutumia njia za
uzazi wampango,hatua itakayosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Post a Comment