Jambo hili liliwezekana, kutokana na misimamo thabiti ya waasisi wa Taifa hili, kukemea hadharani watu ambao walitaka kuligawa Taifa. |
NA: MUSSA JUMA
Waasisi wa Taifa la Tanzania, walifanikiwa kujenga misingi imara
ya kutowagawa Watanzania katika misingi ya dini, makabila na rangi.
Jambo hili liliwezekana, kutokana na misimamo
thabiti ya waasisi wa Taifa hili, kukemea hadharani watu ambao walitaka
kuligawa Taifa.
Ingawa ni kweli kuwa, huwezi kutenga dini na
siasa, pia kwa Taifa lenye wananchi wenye dini na madhehebu tofauti kama
Tanzania, kutumia msingi wa dini moja pekee kuamua jambo ni hatari.
Nasema ni hatari kwa sababu, haiwezekani waumini
wote wa dini zote wakakubaliana na jambo ambalo limeshinikizwa na dini
moja, labda jambo hilo liwe na masilahi kwa dini moja.
Kwa muktadha huu, nataka kuzungumzia kidogo waraka
wa Maaskofu kuhusu Katiba Inayopendekezwa ambao tayari umeanza kusomwa
kwenye makanisa mbalimbali nchini.
Waraka huu wa kitume, licha ya kuwa na maudhui
ambayo yanaungwa mkono na Watanzania wengi, kuelekeza waumini wa
Kikristo kutoipigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa, nadhani kuna
tatizo.
Ni ukweli ulio wazi kuwa kuna maelfu ya waumini wa
dini nyingine, wanaunga mkono maudhui ya waraka huu, lakini kwa
kuhimiza Wakristo pekee kupiga kura ya hapana ni kuligawa Taifa.
Shinikizo la Maaskofu wetu, ni wazi kwa siasa zetu
litaibua baadhi ya viongozi wa dini nyingine nao kusimama na kuwataka
waumini wao waipigie kura ya ndiyo Katiba na hata tutakuwa tumekwisha.
Fikiria mchakato wa kampeni ya kupigia kura Katiba ukianza kuongozwa na viongozi wa dini, hali itakuwaje?
Hapa tutegemee uhasama mkubwa na baadaye kuligawa Taifa kwa misingi ya dini, binafsi namwomba Mungu atuepushie kikombe hiki.
Busara hizi za Kardinali Pengo zinapaswa kuungwa
mkono na viongozi wa dini zote, kuacha kutumia mamlaka yao ya kiimani
kushinikiza jambo ambalo linahitaji ridhaa ya wananchi wote bila kujali
dini zao.
Watanzania wengi wanaipinga Katiba Inayopendekezwa
lakini ni vyema kutumia njia sahihi kutaka wananchi wapige kura ya
hapana na hakika wengi watashinda hata kama zoezi la kura likigubikwa na
mchezo mchafu.
Nawakumbusha uchaguzi mkuu mwaka 2000, baadhi ya
viongozi wa chama tawala, walikuwa wanapiga kampeni chafu wakati huo
wakisema CUF kilikuwa Chama cha Waislamu hivyo kisipigiwe kura.
Walifanikiwa kuwadanganya wananchi hasa wa
vijijini lakini walifanikisha kukijenga Chama cha CUF hasa katika maeneo
yenye Waislamu wengi.
Haikuishia hapo uchaguzi wa mwaka 2010 baadhi ya
viongozi hawa hawa, waliibuka na kuendesha kampeni kuwa, Chadema ni
Chama cha Wakristo na walifanikiwa kuwadanganya wachache, pia
walikiimarisha chama hicho.
Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa, kwa
kawaida dhambi ya ubaguzi ikianza, husambaa na sasa inasambazwa kwa kasi
na viongozi hawa waliotufikisha hapa. Leo wapo kimya wakati maaskofu
wakitoa waraka wao.
Naamini wapo kimya kwa sababu wanajua wao ndiyo
waasisi wa siasa hizi za udini na wameshindwa kufanya uamuzi sahihi
wakati wote, kwa kuzingatia misingi ya dini zao na kutetea masilahi yao
ya kisiasa.
Kwa mfano, suala la Mahakama ya Kadhi ni viongozi
hawahawa, baada ya malalamiko ya Waislamu kwa muda mrefu, waliweka
kwenye ilani yao kuwa wakishinda watarejesha Mahakama za Kadhi, lakini
kwa kuwa hawakuwa na dhamira za dhati na walilenga masilahi ya kisiasa
hadi leo suala hili limekuwa hadithi.
Post a Comment