Na
Ferdinand Shayo, Arusha
Serikali
na wahisani wametakiwa kuweka mipango endelevu ya kuwahudumia wazee katika
jamii katika kupata huduma za malezi na afya .
Mratibu
wa Taasisi ya Sakila Hope for Elderly Humphrey Mafie alisema
kuwa wazee wengi katika siku hizi wanateseka na hata jamii zao
zinawatenga na kuwaona ni mzigo.
Akigawa
misaada ya vyakula ,nguo na mahitaji mengine kwa wazee 293 wanaolelelewa na
taasisi hiyo katika eneo la Meru ,Mafie alisema kuwa idadi kubwa
ya wazee wenye umri mkubwa wametelekezwa na familia zao na kugeuka kuwa omba
omba.
Aidha
aliongeza kuwa wazee wengi ambao hutegemea kilimo wameathiriwa zaidi na
mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi kufuatia kukosekana kwa mvua.
Alisema
mazingira hayo yamewafanya wazee waishio vijijini kuwa na hali mbaya zaidi
kwani wengi wameachwa na vijana ambao wamekwenda katika maeneo mengine
kutafuta fursa za kiuchumi.
“Umefika
wakati wa jamii kuanza mjadala kuhusu namna ya kuwatunza wazee ,hawa
wazee ni hazina ,wengi wamelitumikia taifa na jamii zao hivyo ni muhimu
familia kuwajali na kuwatunza”alisema Mafie.
Wakizungumzia
misaada hiyo wazee Ndetaniso Ndewario walishukuru Shirika la kuhudumia wazee
pamoja na kampuni ya Sigara kwa kuwakumbuka na kuwasaidia.
“Tunashukuru
tumepata nguo vyakula na hata msaada wa kila mwezi wa chakula na
mahitaji mengine tunayopata ikiwemo ya huduma za kiafya”alisema Ndewario.
Mzee
mwingine Sara Noel alisema amefarijika kupata msaada na kuomba serikali
iendelee kuwakumbuka wazee wasiojiweza.
“Sisi
tunashukuru angalau tunapata msaada lakini sote tunajua kuwa kuna kundi kubwa
la wazee wanaoteseka wakikabiliwa na hali ya kukataliwa na jamii zao
,ni muhimu sasa ukawepo mpango wa kitaifa wa kuwasaidia
wazee”alisema mzee huyo kutoka eneo la Kikatiti.
Naye
afisa mahusiano wa kampuni ya Sigara Tanzania ambao ndio wametoa msaada
huo wenye thamani ya shilingi milioni 10 Martha Saivoye
alisema kuwa kampuni hiyo imetoa msaada kwa wazee hao kama moja ya majukumu
yao ya kusaidia kijamii.
Kwa
upande wake mlezi wa taasisi hiyo ya kuwatunza wazee wasiojiweza ,Mchungaji
Amos Baruti alisema kuwa taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya
kumudu kusaidia wazee wengi wasiojiweza.
“Hili
kundi la wazee wasiojiweza linaongezeka kila kukicha,hatuna rasilimali za
kuweza kuwasaidia hivyo ni muhimu serikali na wadau mbalimbali
wakatuunga mkono “alisema Mchungaji Baruti.
Alieleza
kuwa wamejenga kambi maalum ya kuwatunza wazee ambayo itakuwa na uwezo wa
kuwatunza wazee 24 itakapokamilika.
Post a Comment