PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: WIKI YA HATARI KWA ISSUE YA RIPOTI YA ESCROW BUNGENI LEO
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
  Dodoma/Dar. Pamoja na maneno mengi yaliyosemwa, shutuma lukuki zilizotolewa na mbinu za kila aina kutaka kuzuia mjadala wa ripoti ya uc...



 


Dodoma/Dar. Pamoja na maneno mengi yaliyosemwa, shutuma lukuki zilizotolewa na mbinu za kila aina kutaka kuzuia mjadala wa ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya IPTL, leo ndiyo siku yake ya hukumu.


Katika hukumu hiyo, ukweli utadhihirika kuhusu nani mkweli na nani mwongo wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), itakapowasilisha bungeni maoni yake kuhusu ripoti ya kuchotwa kwa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.


Uchunguzi huo ulifanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa maelekezo ya Serikali baada ya kuombwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alipolalamikia ufisadi huo bungeni.


Pamoja na juhudi za kampuni ya IPTL na PAP kufungua kesi kuzua mjadala huo bungeni, hukumu iliyotolewa jana na majaji watatu ilisema kila kitu kiendelee kama kilivyo na kitakachoendelea kisiathiri kesi iliyopo mahakamani.


Uamuzi huo ulipokewa kwa hisia tofauti, upande wa IPTL ukishangilia kwa kupewa ulinzi, huku baadhi ya watu wakieleza kuwa Mahakama imezuia mjadala huo unaosubiriwa kwa hamu.


Muda mfupi baada ya hukumu hiyo kutolewa na kusambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe ambaye pia alikuwa mdaiwa, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, “Mahakama imetoa zuio la kujadili taarifa ya CAG kuhusu Escrow. Hata hivyo, PAC itawasilisha taarifa yake kwa mujibu wa ratiba ya Bunge hapo kesho.”


Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Sisi hatuna taarifa hizo kutoka mahakamani, ratiba ya Bunge inaendelea kama kawaida.”


Habari zaidi kutoka ofisi za Bunge jana, zilisema kuwa Ofisi ya Sheria ya Bunge nayo imeshauri kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa bila wasiwasi wowote.


Mapema jana katika kikao cha asubuhi, Spika Anne Makinda alilithibitishia Bunge kwamba ripoti ya escrow itajadiliwa na hakuna wa kuwazuia.

Kauli hiyo ilitokana na mwongozo wa Mbunge wa Bariadi (UDP), John Cheyo aliyetaka kujua kama Bunge linatambua kuwapo kesi iliyofunguliwa mahakamani kuzuia mjadala wa ripoti hiyo. Akijibu mwongozo huo, Makinda alisema: “Nyie waheshimiwa wabunge msianze kuishi kwa wasiwasi, sisi kinga zetu zipo wazi, hakuna mtu anayeweza kutushtaki sisi tusifanye kazi yetu, hayupo atakayezuia sisi kufanya kazi za kibunge na kazi ambazo zinapatikana kutokana na maeneo mnayopita.”

Muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa Bunge jana usiku, Kaimu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisimama kuomba mwongozo juu ya hatua hiyo ya Mahakama lakini Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alimkatisha akisema kiti cha Bunge hakijapata taarifa zozote na kwamba msimamo uliotolewa mapema na Spika Makinda ndiyo unaofuatwa.

CREDIT: MWANANCHI

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top