Dar es Salaam. Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), imeandaa mdahalo maalumu wa Katiba utakaofanyika kesho kwenye Ukumbi wa Mlimani City ambao mzungumzaji mkuu atakuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Joseph Butiku alisema
jana kwamba mdahalo huo wa amani ni kwa ajili ya Watanzania wenye
mapenzi mema na utakuwa wa wazi, ikiwa ni sehemu ya kuziba pengo la
mdahalo wa Katiba uliovunjika Novemba 2 ambao ulifanyika kwenye Hoteli
ya Blue Pearl.
Ulivunjika baada ya kutokea vurugu zinazodaiwa
kuanzishwa na kikundi cha watu kwa lengo la kuvuruga uwasilishwaji wa
ujumbe wa Katiba, huku Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM, Paul Makonda
akitajwa kinara wa vurugu hizo.
Siku moja baada ya vurugu hizo, Makonda alitumia muda mwingi kujisafisha kuwa alichokifanya ni kumkinga Jaji Warioba asidhurike.
“Tunasema ni mdahalo wa amani na utakuwa wa wazi
kwa watu wote wenye mapenzi mema. Tuna mambo mengi ya kujadili, pia
tunazungumza kuhusu maadili… Tunaona namna watu wanavyojichukulia fedha
za watu bila woga, mdahalo huu unatupa fursa za kujadili kuhusu umuhimu
wa Katiba kulinda maadili ya viongozi na vifungu vingine muhimu,”
alisema Butiku.
Aliongeza kuwa hiyo ni sehemu tu ya ushiriki wa
mijadala na midahalo ya umma kuhusu Katiba Inayopendekezwa, ambayo kwa
sasa inaendelea katika maeneo yote ya nchi, ikifanywa na viongozi wa
kisiasa, mashirika ya kujamii na hata watu binafsi katika vyombo
mbalimbali vya habari.
Alisema japokuwa sasa hivi wamepata ukumbi mdogo
unaoweza kuingiza watu 350, watatoa fursa kwa watu kuuliza maswali na
kupata majibu kuhusu vifungu na vipengele mbalimbali vyenye utata
vinavyoyahusu makundi yote ya kijamii ambayo yamepata uwakilishi katika
mapendekezo hayo ya Katiba.
Aliwataja wengine watakaoshiriki kutoa mada kwenye
mdahalo huo kuwa ni waliokuwa makamishna wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Butiku mwenyewe, Mohamed Mshamba, Maria Kasonda, Profesa Mwesiga
Baregu, Profesa Palamagamba Kabudi na Humphrey Polepole.
Alisema midahalo hiyo ya ndani ni sehemu tu ya
mwendelezo wa mijadala inayoendeshwa na taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka
1997 na kuzinduliwa na Rais wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa mjini
Mwanza.
“Hawa vijana waliovuruga mkutano wetu wa awali
pale Ubungo Plaza, ambao ni vijana wetu na tunawafahamu, hatutarajii
kwamba watarudia tena vitendo vya kihuni kama vile. Kimsingi hawana
sababu kwa kuwa hawakunyimwa fursa ya kujadili na kutoa mawazo yao,
tulishawaonya,” alisema.
Post a Comment