USHIRIKINA WAZOROTESHA MAENDELEO KANDA YA ZIWA
WAKAZI wa Wilaya za Chato, Bukombe na Mbongwe za mkoani Geita, wamewataka viongozi wote wa Vijiji vya Wilaya hizo kuweka mikakati na sheria ndogo ndogo kwa kila kijiji kukabiliana na tabia za viongozi wasiotekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi pamoja na tabia ambazo hazikubaliki katika jamii ikiwemo vitendo vya kishirikiana na ulevi.
Wakiongea na FikraPevu, wananchi wa Kijiji cha Nyamirembe ‘B’ katika Wilaya ya Chato wamesema kukithiri kwa vitendo vya ulevi wa pombe pamoja na baadhi ya wakazi wake kuendekeza mila potofu za vitendo vya kichawi vinawafanya wengi wao kutegemea hali hiyo na kuwa kama kitega uchumi cha kuendeshea maisha ya familia zao.
Rajabu Athumani, mkazi wa Kijiji hicho amesema wapo baadhi ya watu ambao wanashutumiwa kushindwa kuendesha familia zao kwa kuendekeza vitendo vya kishirikina na kwamba hivi sasa wameandika barua kwenda kwa Wakuu wa Wilaya ili kutolewa amri ya kuhamisha familia zote zilizopo katika makazi yao kutokana na kushutumiwa kuwa ni washirikina.
“Wengine wanakunywa pombe kuanzia asubuhi hadi jioni hali ambayo inawafanya watu wengine kushindwa kufanya kazi na kusababisha migogoro na kuvunjika kwa ndoa nyingi kwani wanapolewa wanasahau na kushindwa kutimiza wajibu wao wa ndoa” aliongeza.
Waliokufa wadaiwa kufufuka Kanda ya Ziwa
Inaelezwa kwamba hofu inazidi kutanda kwa wakazi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa kufuatia matukio ya watu waliokufa na kuzikwa na kwamba baada ya miaka, miezi na wiki kadhaa wanaibuka wakiwa hai.
Mmoja wa wakazi katika Wilaya ya Kahama mkoani Sinyanga, Amina Said, amesema matukio hayo yanawatia hofu mara kwa mara licha ya Jeshi la Polisi kushindwa kuwabana wanaoendekeza vitendo hivyo.
Kufuatia matukio hayo, Polisi katika Nikoa hiyo imesema uchunguzi wa matukio ya watu wanaokufa na kufufuka unaendelea kwani matukio hayo yamekuwa ya kutisha hususani katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Rodrick Mpogolo, Wilaya ya Chato inaongoza kwa kuwa na imani za kishirikiana na kunywa pombe za kienyeji kuliko Wilaya nyingine zote za mkoa huo na kwamba vitendo vya uchawi na pombe vimeharibu sifa ya Wilaya hiyo na mikoa ya Kanda ya Ziwa, kutokana na mila na tamaduni za wakazi wa mikoa hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Nassoro Rufunga, amesema wakazi wengi wa mkoa huo ambao ni kabila la Wasukuma, pasipo kukomesha tabia hiyo kwa wao wenyewe kuamua kubadilika na kuacha tabia hizo, taifa litakosa vijana ambao ndiyo nguvu kazi sasa na siku zijazo.
Walaumiana udhibiti wa mimba kwa wanafunzi
Wanavijiji wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza wametupiana lawama kuhusiana na baadhi ya wazazi na viongozi wa vijiji kuwafumbia macho watu wanaotuhumiwa kuwatia mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari na kuwakatisha masomo bila kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanavijiji wamesema idadi kubwa ya wanafunzi wanaotiwa mimba na kukatishwa masomo ya shule za msingi na sekondari wamekuwa wakirudi vijijini na kulea watoto huku kukiwa hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa kwa wanaotuhumiwa kuwatia mimba.
Daniel Ngolia, mkazi wa Kijiji cha Nditi amesema katika kijiji hicho wapo wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari ambao wanalea watoto wao baada ya kutiwa mimba na kukatishwa masomo yao na wahusika kuendelea kupeta mtaani.
Ushirikina na mapambano dhidi ya mimba shuleni
Vitisho na hofu ya vitendo vya ushirikina imebainika kuwa ni vikwazo vya mapambano ya baadhi ya watu wanaowatia mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika mkoa wa Simiyu. Mwenyekiti wa Kijiji cha Madeko katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Willson Ngigili, amekiri uwepo wa matukio ya mimba kwa kiasi kikubwa kijijini hapo lakini amesema kikwazo katika kushughulikia matukio ya mimba ni uongozi kukosa ushirikiano kutoka kwa wazazi na mwanafunzi ambao wanadaiwa kushiriki vitendo vya kishirikina.
Baadhi ya wanakijiji kutoka katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya hiyo walipofanya mahojiano kwa nyakati tofauti wamesema mbali na tatizo hilo kutokana na Kituo cha Afya cha Ntuzu kutoa huduma zake mchana tu imewapa shida baadhi ya wagonjwa hasa akinamama wajawazito ambao huhitaji huduma ya uzazi/kujifungua nyakati za usiku hivyo wengine kulazimika kujifungulia nyumbani.
Post a Comment