VIONGOZI
Wakuu wa Vyama vya siasa vyenye Wabunge vinavyounda Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) wamekuwa katika mashauriano ya zaidi ya mwezi
mmoja tangu tarehe 2 Agosti mwaka huu huku wakishauriana juu ya mwenendo
wa mchakato wa Katiba Mpya na jinsi ya kuwa na uchaguzi ulio huru na wa
haki hapo mwakani.
Akiongea
kwa niaba ya viongozi wengine wa kituo hicho, Mwenyekiti wa TCD, Mhe.
John Cheyo amesema kuwa Katika mashauriano hayo yaliyochukua sura ya
Kamati ya Makatibu Wakuu, Kamati ya Wenyeviti wa Vyama vya CCM, CHADEMA,
CUF na NCCR-Mageuzi katika hatua tofauti.
Mhe.
Cheyo ameeleza kuwa kamati zote zilitoa taarifa zao kwenye vikao vya
Viongozi Wakuu wa Vyama (Summit) ya TCD ambayo wajumbe wake ni
Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Makatibu Wakuu wa Vyama wanachama.
Mhe.
Cheyo aliongeza kuwa katika kutafuta maridhiano, Wenyeviti na Makatibu
Wakuu wa Vyama walifanya mashauriano na Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete siku ya tarehe 31 Agosti mwaka huu, hivyo tarehe Nane Septemba,
2014 hapa Dodoma wakatoa tamko lao.
“Pamoja
na kazi ya msingi inayofanywa na Bunge Maalum la Katiba, mchakato wa
Katiba unaoendelea sasa hauwezi kutupa Katiba itakayotumika katika
Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuwa muda hautoshi kukamilisha mchakato na
kufanya mabadiliko yatakayohitajika ya Sheria, Kanuni na Taasisi
mbalimbali zitakazohitajika”, alisema Mhe. Cheyo.
Mhe.
Cheyo aliendelea kwa kusema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba mwisho wa mchakato ni kura ya maoni itakayofanyika mwezi Aprili
2015.
“Kama
itabidi kura irudiwe kwa mujibu wa Sheria iliyotajwa, kura itarudiwa
mwezi Juni au Julai 2015, muda ambao Bunge la Jamhuri ya Muungano
linatakiwa livunjwe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2015 na ili
Katiba Mpya itumike katika uchaguzi Mkuu utakaokuja, itabidi uhai wa
Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo hatuliungi
mkono”, alisisitiza Mhe. Cheyo.
Akiongelea
juu ya Tangazo la Serikali GN Na 254, Mhe. Cheyo amesema kuwa Bunge
Maalum la Katiba kwa sasa linafanya kazi kwa mujibu wa Tangazo la
Serikali (Government Notice) Na 254 lililotolewa na Mhe. Rais Kikwete
tarehe 1 Agosti, 2014.
“Tangazo
hilo litatumika hadi tarehe 4 Oktoba, 2014 ambapo Katiba
inayopendekezwa inategemewa kupatikana, Wajumbe walikubaliana hatua hii
iachwe ifikiwe”, alisema Mhe. Cheyo.
Kuhusiana
na Kura ya maoni, Mhe. Cheyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba baada ya Bunge hilo kumaliza kutunga Katiba,
ingefuata hatua ya kura maoni kuthibitisha Katiba.
“Kwa
kutambua kuwa hatua ya kura ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015
kualishwa, basi hatua hii iailishwe, na mchakato wa Katiba uendelee
baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015”, alisema Mhe. Cheyo.
Sambamba
na hayo, Mhe. Cheyo ameishauri Serikali kuchukua hatua za kisheria ili
matayarisho kwa ajili ya Uchaguzi wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa, yaanze
haraka iwezekanavyo ili uchaguzi ufanyike mapema hapo mwakani.
Aidha,
amegusia kuhusu Mabadiliko ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya 1977 akasema kuwa, kwa vile Uchaguzi Mkuu wa 2015 utafanyika
kwa kutumia Katiba ya 1977, kuna umuhimu kufanya mabadiliko kidogo
(minimum reforms) katika Katiba pamoja na sheria ya Uchaguzi
yatayowezesha nchi kufanya uchaguzi huru na wa haki.
“Tayari
mambo yafuatayo yamekubaliwa, kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia
uchaguzi, Mshindi wa Uchaguzi wa Rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50%
(50%+1)”, alisema Mhe. Cheyo.
Viongozi
hao Wakuu wa Vyama wamempongeza Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
kwa ujasiri wake na imani yake katika kuimarisha demokrasia nchini na
kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya nchi.
“Tunampongeza
kwa kukubali kukutana na kushauriana nasi kuhusu mambo ya muhimu kwa
mustakabali wa taifa letu kwa lengo la kudumisha amani, upendo na
mshikamano ili nchi yetu iende kwenye uchaguzi ikiwa ni nchi ya
kujivunia yenye amani, mshikamano na itakayokuwa na Uchaguzi Huru na wa
haki, lakini pia tunajipongeza sisi wenyewe Wakuu wa Vyama kwa kuwa
tumetoka mbali na misimamo yetu, lakini utaifa umetufanya tukubaliane
katika mambo ya msingi wa Taifa letu”, alipongeza Mhe. Cheyo.
Post a Comment