CWT IRINGA WAZIDI KUINYIMA USINGIZI SERIKALI
CHAMA cha Walimu Tanzania mkoa wa Iringa, kimetoa siku saba kwa serikali iwe imewalipa walimu wote madeni wanayodai ya zaidi ya milioni 870 vinginevyo kitaitisha mgomo wa kufundisha madarasani na kuandamana katika mamlaka husika.
Taarifa ya Mwenyekiti wa CWT mkoani humo, Stanslaus Muhongola, imesema kwamba kama madeni ya walimu hayatakuwa yamelipwa ndani ya siku hizo, walimu hawataingia darasani kufundisha.
Aidha, amekaririwa leo akisema Septemba 15, 2014 walimu wa wilaya zote za mkoa huo watafika katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa kama waajiri na kudai haki zao kwa kuwa madeni hayo sasa hayavumiliki.
Amebainisha kuwa chama hicho kimeshangazwa na taarifa kuwa serikali imeokoa kiasi kikubwa cha fedha zilizokuwa zikilipwa kama mishahara hewa pasipo kuvishirikisha vyama vya wafanyakazi.
Kwa upande wake Katibu wa umoja huo mkoani humo, Mshamu Mshamu, amesema walimu mkoani humo wanaidai serikali zaidi ya shilingi milioni 870.
Katibu Tawala wa mkoa huo, Wamoja Dickolangwa, amekanusha madai hao na kuwa Ofisi hiyo haijapata taarifa yeyote juu ya madai hayo, huku akisema atanza kufuatilia katika halmshauri zote ili kujiridhisha na madeni yanayolalamikiwa kutokana na baadhi ya watu hutumia mbinu nyingi kutaka kulipwa mishahara hewa.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri hizo , wamethibitisha kuwepo na malalamiko ya madeni kwa walimu hao na kuwa tatizo hilo linatokana na mkanganyiko wa baadhi ya taarifa ambazo zimepelekea mlundikano wa madeni ya walimu kulingana na halmashauri husika.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa hivi karibuni takribani Walimu 298 wa shule za msingi na sekondari walioajiriwa mwaka huu katika ya Wilaya Igunga mkoani Tabora, waliendesha mgomo wa siku nne mfululizo wa kubaki na kulazimika kulala katika viti na meza katika ukumbi wa Halmashauri hiyo wakishinikiza serikali ya Wilaya ya Igunga kuwalipa mishahara yao suala ambalo lilileta msuguano mkali baina ya walimu hao na halamshauri ambapo licha ya kufanyika kwa mashauriano baina yao hawakulipwa malipo yote kama walivyokuwa wanahitaji.
Post a Comment