Kamati za
Bunge Maalumu, zimekamilisha kazi ya kujadili na kuchambua Rasimu ya
Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku ikiwa
imefanyiwa mabadiliko makubwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Wajumbe
wanatarajiwa kuanza kukutana kama Bunge zima kuanzia Jumanne ijayo,
Septemba 2, 2014 wakati kamati zitakaposoma taarifa zake baada ya
kufanya uchambuzi wa sura 15 za Rasimu ya Katiba kwa zaidi ya wiki tatu,
huku yakitarajiwa mabadiliko makubwa.
Mabadiliko
yaliyofanywa yameondoa mambo makubwa yaliyokuwa yakiifanya rasimu hiyo
kuonekana mpya, hivyo sasa baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaiona rasimu
kama 'Katiba ya 1977 iliyofanyiwa marekebisho.'
Mwelekeo
wa kubadili karibu misingi yote muhimu iliyojengwa na tume iliyoongozwa
na Jaji Joseph Warioba akiwa mwenyekiti, ilianza baada ya kuwekwa kando
kwa mfumo wa muungano wa Serikali tatu uliopendekezwa na badala yake
kurejea katika muundo wa sasa wa serikali mbili.(P.T)
Uamuzi
huo uliathiri mtiririko na muundo mzima wa sura na ibara za rasimu hiyo,
kwani sasa wajumbe wa Bunge Maalumu walilazimika kutengeneza Katiba
yenye mwelekeo wa serikali mbili na siyo tatu tena zilizokuwa
zimependekezwa na tume.
Katibu wa
Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba
mwelekeo wa uchambuzi wa rasimu kwa sura hizo 15, lazima ufuate kile
ambacho kamati zilikiamua katika uchambuzi wa awali wa sura ya kwanza na
ya sita.
Miongoni
mwa mambo ambayo yameachwa baada ya kurejesha mfumo wa serikali mbili ni
muundo wa uongozi wa juu wa nchi hususan nafasi ya Makamu wa Rais,
muundo wa Bunge la Jamhuri, kupunguzwa mamlaka ya Rais, uwajibikaji na
uwajibishwaji wa wabunge na ukomo wa ubunge.
Kadhalika,
habari kutoka ndani ya kamati zilisema suala la kuwekwa kwa maadili ya
uongozi kwenye Katiba nalo lilizua mjadala mkali kutokana na baadhi ya
wajumbe kutaka liondolewe kwa maelezo kwamba linapaswa litajwe kwenye
sheria na siyo Katiba.
Mambo ya muungano
Miongoni
mwa mambo ambayo kuna kila dalili kwamba yatabadilika ni Bunge Maalumu
kuongeza mambo ya muungano kutoka saba yaliyopendekezwa na tume na
huenda idadi yake ikazidi 22 yaliyomo kwenye Katiba ya sasa.
Uchunguzi
wa gazeti hili uliofanywa katika baadhi ya kamati za Bunge hilo na
kuthibitishwa na baadhi ya wenyeviti wake, umebaini kuwa yapo
mapendekezo ya mambo ya muungano kuongezwa, tofauti na mtazamo wa awali
kwamba yangepungua kama moja ya njia za kuondoa kero za muungano.
Tume ya
Jaji Warioba ilipendekeza mambo saba tu kwenye orodha ya muungano chini
ya mfumo wa Serikali tatu, mfumo ambao hata hivyo ni dhahiri umeshawekwa
kando na Bunge Maalumu na kurejesha muundo wa serikali mbili.
Mambo
yaliyopendekezwa na tume hiyo ambayo yapo kwenye sura ya 17 ya Rasimu ya
Katiba inayohusu masharti ya mpito ni pamoja na Mamlaka ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Uraia na Uhamiaji.
Mengine
ni Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa na
Ushuru wa Bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya
Muungano.
Mapendekezo
hayo yaliyaacha nje mambo mengine 15 yaliyopo kwenye Katiba ya sasa
ambayo ni polisi, mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari,
mikopo na biashara ya nchi za nje, utumishi katika Serikali ya Jamhuri
ya Muungano, bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na
simu na leseni ya viwanda na takwimu.
Pia yamo
elimu ya juu, maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya
motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au
bidhaa na gesi asilia, Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania, usafiri
na usafirishaji wa anga, utafiti, utafiti wa hali ya hewa na Mahakama ya
Rufani ya Jamhuri ya Muungano.
Baadhi ya
wenyeviti wa kamati za Bunge Maalumu wamesema kuna kila dalili kwamba
baadhi ya mambo yaliyoachwa yatarejeshwa huku kukiwa na mtazamo kwamba
mengine yanaweza kuongezwa kutoka nje ya orodha ya sasa.
Mwenyekiti
wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid Mohamed alisema orodha iliyopo
kwenye Rasimu ya Katiba ina upungufu mkubwa kwani imeacha mambo mengi ya
msingi yenye sura ya muungano.
"Mathalani
huwezi kuzungumzia kwamba usalama ni suala la muungano halafu ukaacha
mambo ya anga, au ukaacha suala la mitihani, yaani Baraza la Mitihani
limeachwa pia suala la utafiti nalo huwezi kuliacha, kwa hiyo orodha
itaongezeka," alisema Mohamed.
Mwingine
ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita, Stephen Wassira alisema kuna mambo
mengi ya muungano yaliyotajwa kwenye Rasimu ya Katiba lakini hayako
katika orodha iliyowekwa kama moja ya nyongeza kwenye rasimu hiyo.
"Ngoja
nikwambie kwamba mambo hayo yataongezeka, hilo halina ubishi na kamati
yangu tulijadili kidogo na kesho (leo) tutakutana kumalizia. Ukisoma
vizuri ibara kwa ibara, utagundua kuwa kuna mambo mengi kama vile Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo ni chombo cha muungano hata ukiangalia
muundo wake," alisema Wassira.
Alitaja
mambo mengine kuwa mahakama ya juu inayopendekezwa kuanzishwa lakini
haimo kwenye orodha pamoja na masuala ya elimu ya juu na utafiti.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa Kamati Namba nne, Christopher Ole Sendeka
alisema kuna kazi kubwa ya kutazama upya orodha ya mambo ya muungano na
kwamba suala la usalama wa anga ni moja ya mambo hayo.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu alisema, licha ya kwamba
kamati yake haikujadili suala hilo lakini orodha hiyo inaweza kuongezeka
kwani kuna mambo mengi yameachwa.
"Leo
tulikuwa tunaangalia suala la fedha na kuna mambo ukichuguza humo
yanagusa sehemu zote mbili, sisi hatukujadili sehemu hiyo kutokana na
kwamba haikuwa kwenye orodha ya kazi tulizopewa ila nadhani tukipata
fursa bungeni lazina mambo hayo yaangaliwe," alisema Mwalimu.
Kamati
nyingine ambayo haikujadili suala hilo ni namba tatu ambayo mwenyekiti
wake, Dk Francis Michael alisema orodha ya mambo ya muungano iko kwenye
sura ya 17 ambayo haikuwa sehemu ya kazi za kamati.
Post a Comment