ASKARI Polisi mkoani Arusha, wameiomba Mamlaka ya Udhibiti wa
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuweka mazingira yatakayowawezesha
kuhamisha mafao yao kutoka mfuko mmoja kwenda mwingine.
Akizungumza katika warsha iliyoandaliwa na SSRA, Inspekta Joseph
Labia, alisema uzoefu unaonyesha kuna ugumu wa kuhamisha mafao kutoka
mfuko mmoja kwenda mwingine.
“Kuna mifuko ina mafao mazuri kuliko mwingine na wengi tungependa
kuwa na hiyari ya kuhamisha mafao yetu, lakini kuna ugumu wa kuruhusiwa
kuhamisha. Tunaomba SSRA muweke mazingira mazuri kwa hili kuwezekana,”
alisema Inspekta Labia.
Awali Mkurugenzi SSRA, Ansgnar Mushi, alisema hivi sasa wanafanya
utaratibu wa kuoanisha kanuni ya ukokotoaji wa mafao ya wastaafu iwe
moja kwa mifuko yote, ili kuwezesha watu kuwa huru kuhamisha mafao yao.
Semina hiyo ilikuwa na lengo la kutoa uelewa wa kutosha kuhusu
shughuli za mamlaka hiyo pamoja na uendeshwaji wa sekta ya hifadhi
jamii nchini.
Post a Comment