ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ametoa siri ya msimamo wa majeshi ya Tanzania kuhusu muundo wa Muungano wa sasa.Jaji Warioba ametoa siri hiyo huku kukiwa na vitisho kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na viongozi waandamizi wa serikali kwamba muundo wa Muungano wa serikali tatu ukipitishwa jeshi litachukua nchi.
Akifichua msimamo huo wa majeshi, Jaji
Warioba alisema wakati wa kukusanya maoni ya rasimu ya kwanza na ya pili
ya Katiba, baadhi ya wanajeshi walieleza bayana kuwa moja ya kero kubwa
ya Muungano wa serikali mbili wa sasa ni kupiga mizinga 21 kwa viongozi
wawili tofauti walio katika nchi moja.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo jana
jijini Dar es Salaam wakati akichangia mada katika uzinduzi wa ripoti ya
utafiti ya taasisi ya Twaweza iliyolenga kujua ni jinsi gani Watanzania
wanaiona Katiba.
Katika uzinduzi huo wa Twaweza wasemaji
wengine walikuwa Dk. Khamis Kigwangwala, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahaman Kinana, na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi
(CUF), Julius Mtatiro.
“Kila nilipokwenda kukusanya maoni
sehemu yenye makambi ya jeshi, tulifika na mara nyingi tulikuwa na Jaji
Agustino Ramadhani na Dk. Salim Ahmed Salim, kero yao kubwa waliyokuwa
wanatueleza ni kitendo cha kuwapigia mizinga 21 viongozi wawili walio
katika nchi moja, mara Bara mara Visiwani,” alisema Jaji Warioba.
“Kama jeshi lina dhamira ya kuchukua
nchi lingeweza kufanya hivyo kwa vitendo vya rushwa na ufisadi
vilivyotamalaki nchini. Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanapaswa
kuwa makini na kauli zao katika kulihusisha jeshi na masuala ya
kisiasa,” aliongeza.
Akizungumzia vitisho vinavyotolewa na
baadhi ya viongozi kwa wananchi kwa kutumia mgongo wa jeshi, Jaji
Warioba alisema wanaofanya hivyo hawalitakii mema taifa na badala yake
wanataka kuwapa hofu ya bure wananchi.
“Mimi nasema wasinishambulie binafsi,
wajibu hoja za wananchi kwa sababu walizozitoa za kutaka serikali tatu
na huu mtindo wa kusingizia kuwa gharama zitakuwa kubwa, mara jeshi
litachukua madaraka ni upotoshaji mkubwa unaofanywa kwa makusudi,”
alisema.
Ingawa hakutaja majina ya viongozi
waliotoa kauli kwamba serikali tatu zikipitishwa jeshi litachukua nchi
ni dhahiri kuwa Jaji Warioba alimlenga Rais Jakaya Kikwete na William
Lukuvi, ambao kwa nyakati tofauti wamepata kutoa kauli za kutishia jeshi
kuchukua nchi.
Jaji Warioba ambaye amepata kuwa waziri
mkuu, aliongeza kuwa ni jambo la hatari kwa viongozi wa serikali kutumia
majukwaa ya dini kuligombanisha taifa kwa misingi ya imani.“Kwa kweli hii ni hatari, tumezoea pale tunapokuwa na tofauti zetu kukimbilia kwa viongozi wa kiroho kupata nasaha zao, leo tunakimbilia kwenda kuwagawa wananchi na jambo hili linafanywa wazi wazi,” alisema Jaji Warioba.
Ahofia mchakato mwingine wa Katiba
Jaji Warioba alisema kwa hali ilivyo ndani ya Bunge la Katiba, hata kama Katiba itapatikana haitaishi kwa miaka 50 ijayo bali itaamsha ari ya wananchi kutaka katiba yenye ridhaa yao ndani ya miaka hata mitano tu.Alisema kinachofanyika bungeni ni walio wengi kutaka kupitisha mambo yao na wachache kuzuia hali hiyo isitokee, huku rasimu nzima ikiwa imeachwa pembeni.Jaji Warioba aliongeza kuwa kinachomshangaza zaidi ni kuona rasimu ambayo ni mawazo ya wananchi ikibezwa na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo, huku wakiendelea kusema wametumwa na wananchi wawawakilishe.Katika hali ya masikitiko Jaji Warioba aliwaomba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutambua wajibu walio nao mbele ya Watanzania na wafanye kila wanaloweza kuhakikisha majadiliano wanayoyaendesha hayawi chanzo cha kuigawa nchi.Alisema hatari kubwa inayoonekana ni kuligawa taifa kutokana na lugha inayotolewa na kila upande katika kutetea hoja wanazoamini.“Kama leo unamuita mtu mtoto wa shetani, halafu unasema mkutane katika maridhianao, hii ni ngumu na tusipokuwa makini na lugha hizi nchi itagawanyia huku tukiona,” alionyo Jaji Warioba.
Hataki uteuzi wowote
Katika hatua nyingine, Jaji Warioba
alisema hayupo tayari kushika nafasi nyingine yoyote ya uteuzi na badala
yake anataka aachwe akalee wajukuu zake.
Alitoa kauli hiyo baada ya mwandishi wa
gazeti hili kumuuliza kama atakuwa tayari kupokea uteuzi mwingine wowote
baada ya wajumbe wa Bunge la Maalumu la Katiba na viongozi waandamizi
wa serikali kuamua kumshambulia binafsi kutokana na maoni ya wananchi
aliyoyaratibu chini ya usimamizi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema hali hiyo inamsikitisha na hawaelewi watu wanaomshambulia kwamba wanafanya hivyo kwa sababu gani.
“Kuna watu walikuja na kusema haya ya
tume ni mawazo yetu ya zamani kwa kuwa tulikuwa katika tume ya Jaji
Kisanga na Bunge la G 55, ninachoweza kusema katika tume ya Jaji Kisanga
hatukuwa sehemu yao na G 55 wengine katika tume ya sasa wala hawakuwa
wabunge, hivyo mashambulizi haya hayana msingi kwetu na mimi nimeshasema
waniache niwalee wajukuu zangu, wao wajibu hoja za wananchi,”
alisisitiza Jaji Warioba.
Kigwangwala aja na wazo jipyaMchangiaji wa pili katika mjadala huo, Dk. Khamis Kigwangwala, aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, alisema kilichofanywa na tume ya Jaji Warioba ni kinyume cha hadidu rejea walizopewa kukusanya maoni.
Alisema kama tume iliona kuna haja ya
wananchi kujadili muundo wa muungano, wangerudi kwa mtu aliyewateua
(Rais) ili wapate ridhaa ya kukusanya maoni hayo kutoka kwa wananchi.Alisema tume haikutumwa kujadili muundo wa Muungano au kwenda kuifufua Tanganyika na badala yake ilitakiwa ihakikishe Watanzania wanapata Katiba mpya bila kuathiri muundo wa Muungano uliopo.
Aliongeza kuwa muundo wa Muungano unahitaji mchakato wa peke yake, tofauti na ilivyofanywa na tume ya Jaji Warioba.
Kuna mambo mengi na mazuri yaliyoletwa
na rasimu sasa yanapitishwa bila ya kujadiliwa na badala yake tunajikita
katika muundo wa Muungano, hili ni tatizo ambalo tume imezalisha,”
alisema Dk. Kigwangwala.
Hata hivyo kauli hiyo ya Kigwangwala
ilipata upinzani kutoka kwa washiriki mbali mbali, ambapo Maria Sarungi
alisema sheria ya mabadiliko ya Katiba iliipa tume uhuru wa kujadili
yale mambo watakayoona yanafaa, kauli iliyoungwa mkono na Jaji Warioba
na Profesa Sharif Ahmad.
Katika hatua nyingine, Profesa Samuel
Wangwe, alionyesha kumshangaa Dk. Kigwangwala kutetea hoja ya muundo wa
serikali mbili na kusema ni msimamo wa CCM huku wanachama wakiwa
hawajashirikishwa katika maoni hayo.
Mtatiro ataka utafiti uheshimiwe
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alieleza kuwa kinachofanyika
katika Bunge Maalumu la Katiba ni kundi moja kutaka kujadili rasimu
waliyotoa mfukoni na kuiacha iliyofanyiwa utafiti.
Alisema rasimu ya tume ipo na inaelekeza
namna walivyofanya utafiti, na kupata maoni ya wananchi, lakini rasimu
nyingine haielezi, jambo aliloeleza wazi kuwa hawako tayari kuijadili.
Alisema hatua ya Rais Jakaya Kikwete
kutaka kuacha jina kuwa amewapatia Watanzania Katiba, ndiyo imelifikisha
suala hili kuwa la kichama zaidi badala ya kuzingatia mapendekezo
muhimu aliyofikishiwa.
“Sisi wapinzani tulimwambia suala la Katiba ni uhai wa taifa lolote, halihitaji haraka kama ya Voda fasta, tukapendekeza maeneo ya msingi ya kufanyiwa kazi kisha ndiyo tuanze mchakato mzima, wenzetu hawakukubali na rais alitaka aache jina kuwa amewapatia Watanzania katiba mpya lakini tunayokwenda kuipata haitakuwa ya wananchi,” alisema Mtatiro.
About Author
Journalist , Enterpreneur, Lecturer and Blogger. Email :ngoboleaa@gmail.com.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment