PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: HATI YA MUUNGANO YAWA HOJA NAMBARI 1 KATIKA KUJADILI RASIMU YA KATIBA DODOMA.
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
SIKU ya kwanza ya kujadili rasimu jana, kwa kamati tatu zilizotoa taarifa, zimeeleza mjadala umeanza kwa amani huku wajumbe wen...



SIKU ya kwanza ya kujadili rasimu jana, kwa kamati tatu zilizotoa taarifa, zimeeleza mjadala umeanza kwa amani huku wajumbe wengi wakitaka kuoneshwa kwanza hati za Muungano, zilizosainiwa na waasisi wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume, ndipo waanze mjadala. Baada ya kukabidhiwa hati hizo na kupewa ufafanuzi wake na kuuridhia, wajumbe walianza kujadili Sura ya Kwanza ya Rasimu ya Katiba, ingawa imeelezwa matumizi ya maneno nchi, dola, serikali, shirikisho, taifa na muungano, vimewachanganya. 

Aidha suala la muda kutotosha, limejitokeza katika kamati karibu zote hivyo viongozi wa kamati hizo, wameahidi kuzungumza na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta kuomba awaongezee angalau wapate siku nne za kujadili sura mbili walizopewa badala ya siku mbili. 

Hati za Muungano 

Wakizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, wenyeviti wa Kamati ya Kwanza, Tano na 11, wote walikiri kwamba wajumbe kabla ya kuanza mjadala, suala la kwanza waliloomba ni kuona hati za Muungano. 

Wenyeviti hao na majina ya kamati katika mabano ni Ummy Mwalimu (Kamati ya Kwanza), Hamad Rashid Mohamed (ya Tano) na Anne Kilango Malecela ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya 11. 

Kilango alisema baada ya kukabidhiwa hati hizo, kuliibuka hoja mbalimbali ambazo hakuzifafanua, lakini zilihusu uhalali wa hati hizo. 

Hata hivyo, Kilango alifafanua kuwa Kamati yake imepata bahati ya kuwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ambaye alitoa ufafanuzi uliokubalika na kuwezesha kuendelea na majadiliano. 

Hali kama hiyo, pia ilitajwa kujitokeza katika Kamati Namba Tano inayoongozwa na Rashid na Kamati Namba Moja inayoongozwa na Ummy.Hoja ilikuwa, hati hizo kutokuwa na saini zote mbili za waasisi kwa kuwa zilikuwa na saini moja moja. 

Kwa mujibu wa Ummy, kabla ya kuanza mjadala, suala la Hati za Muungano liliibuka, kama vile wajumbe walikuwa wameambizana na baada ya nusu saa zilipatikana na wajumbe wakaridhika na kuendelea na mjadala. 

Maneno yawachanganya 

Suala lingine lililojitokeza katika kamati hizo ni matumizi ya maneno nchi, dola, taifa, serikali, shirikisho na muungano, ambayo wajumbe walionekana kutaka kufahamu maana na mipaka ya matumizi yake, kabla ya kuendelea na mjadala.

Kilango alisema, amelazimika kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta wapate mtaalamu katika kamati yake, awape ufafanuzi wa matumizi ya maneno hayo. 

“Kanuni inaruhusu nimuombe Mwenyekiti aniletee mtaalamu, nimeomba aje saa 10 (jana),” alisema Kilango. Kwa upande wa Ummy, alisema wajumbe wake walikuwa na vitabu huku kila mtu akitoa ufafanuzi wake, akinukuu kitabu chake kuhusu maana na matumizi sahihi ya maneno hayo. 

Muda hautoshi 

Suala la kutotosha kwa siku mbili kujadili sura mbili, pia liliibuka kwenye kamati. Jana walitakiwa kujadili Sura ya Kwanza na leo Sura ya Sita ya rasimu ya Katiba mpya. 

Kwa mujibu wa Kilango, Sura ya Kwanza ina sehemu mbili na mpaka jana mchana na kwa mtazamo wake mpaka saa 2 usiku, walitarajia kujadili sehemu ya kwanza ya sura ya kwanza yenye ibara tano. 

Sehemu ya pili ya Sura ya Kwanza, kwa mujibu wa Kilango, wanatarajia kuijadili leo na hivyo hawatakuwa na nafasi ya kujadili Sura ya Sita kama hawataongezewa muda. 

“Sasa itabidi leo jioni nizungumze na Mwenyekiti wa Bunge, nimwambie kuwa muda hautoshi,” alisema Kilango. Naye Ummy, alisema mpaka jana saa 9 alasiri, Kamati anayoiongoza ilikuwa ikijadili Ibara ya Kwanza ya Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Kwanza tu. “Kwa kweli muda hautoshi kwa kuwa bado tupo Ibara ya Kwanza tu,” alisema. 

Wenyeviti wote walithibitisha katika kamati zote tatu, hakukutokea hali ya kurushiana maneno makali. Walisema, wajumbe walijadili kwa ustaarabu. 

Aidha, ilielezwa wapo wajumbe waliokuja na majedwali ya marekebisho ya Ibara tofauti, ambayo yalivumishwa kuwa ni Rasimu Mbadala ya CCM, jambo lililokanushwa na wenyeviti wote. 

Maagizo ya Sitta 

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Sitta, juzi aliagiza kamati hizo kuanza kujadili Sura ya Kwanza na Sura ya Sita kwa siku mbili za jana na leo. 

Kesho Kamati ya Uandishi inatarajiwa kukaa na kuandika makubaliano ; na Ijumaa wenyeviti wote 12 wawasilishe taarifa zao katika Bunge Maalum la Katiba. 

Wenyeviti hao watawasilisha hoja za wengi na hoja za wachache, ambazo zitaitwa hoja kinzani na kisha mjadala utafanyika kabla ya kuzipitisha sura na ibara husika na kuhamia sura na ibara nyingine. 

Sitta alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, iliamua kuanza kujadiliwa kwa Sura Namba Moja na Sita, kutokana na sura hizo kuwa na mambo yanayofanana kuhusu muundo wa Serikali na Muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Kupatikana kwa muundo kutafanya mjadala juu ya masuala mengine kuwa rahisi. “Kama mnavyojua sura namba moja, sura namba sita na sura namba nane zina masuala yanayofanana. Lakini kwa vile kanuni zinatutaka tujadili sura mbili mbili tutaanza na sura namba moja na sura namba sita ambazo zinafanana maana zinazungumzia muundo wa Jamhuri na Muungano,” alisema Sitta. 

Aliongeza, “Kamati zitakapojadili kuhusu muundo wa Serikali ya Jamhuri na Muungano masuala kama Mahakama, Dola na mengineyo yatakuwa rahisi kuyaingiza katika rasimu kwa kuzingatia mfumo utakaokuwa umekubaliwa na wajumbe wengi wa Bunge la Katiba.” 

Polisi yakamata waandamanaji 

Katika hatua nyingine, watu watatu wanashikiliwa na Polisi mkoani Dodoma kwa kufanya mkusanyiko usio halali huku wakiwa wamebeba mabango yanayohamasisha uvunjifu wa amani. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema tukio hilo ni la jana katika maeneo mawili tofauti. 

Alitaja waliokamatwa ni Augustino Pancras (60), mkazi wa Kilimani, Cosmas Katebeleza (44), mkazi wa Kikuyu na Jotam Tarukundo (44) mkazi wa Chidachi. 

Kamanda Misime alisema moja ya mabango waliyokutwa nayo, yalikuwa na ujumbe, “Wajumbe msijivunie wingi wenu humo ndani, sisi wananchi tupo nje na ndiyo wengi, maoni yetu yaheshimiwe.” 

Alisema watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika, kulingana na ushahidi, watafikishwa mahakamani kwa kufanya mkusanyiko usio halali na kuwa na mabango ya kuhamasisha uvunjifu wa amani. “Bado Polisi wanaendelea kuwatafuta watu wengine waliokimbia,” alisema Kamanda. 

Inadaiwa Katebeleza alikamatwa eneo la Dodoma Hoteli akiwa amebeba bango. Pancras na Tarukumbo walikamatwa katika eneo la Hoteli ya St. Gasper.

Katika maeneo hayo walikokamatwa, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, walikuwepo kujadili rasimu. Hata hivyo, bado haijafahamika lengo la watuhumiwa hao kuandamana wakiwa na mabango.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top