PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: WAKULIMA WAFUNDWA KUTUMIA PILIPILI KUWADHIBITI TEMBO WANAOVAMIA MAZAO
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
    Dkt. Alex Chang'a kulia akiwa na  wadau wengine katika mafunzo maalumu ya kutumia pilipili katika kudhibiti wanyama wanaovamia makaz...

  

Dkt. Alex Chang'a kulia akiwa na  wadau wengine katika mafunzo maalumu ya kutumia pilipili katika kudhibiti wanyama wanaovamia makazi ya wakulima




Na: Mwandishi wetu, Babati



Wakulima 1000  wanaoishi pembezoni mwa maeneo yaliyohifadhiwa, mkoa wa Arusha na Manyara wamepewa mbinu mpya za kukabiliana na Tembo waharibifu wa mazao ikiwepo kutumia vilipuzi, pilipili na vuvuzela.


Kumekuwepo na ongezeko la matukio ya tembo kuingia katika makazi ya watu kula mazao na kusababisha vifo vya watu,  katika maeneo ya Ikolojia ya hifadhi za Tarangire-Manyara  hadi Ngorongoro .


Akizungumza katika kongamano la wakulima hao lililofanyika kijiji cha Kakoi wilayani Babati,  Mkurugenzi wa mradi wa Tembo Pilipili Dk Alex Chang'a alisema ni muhimu wakulima kuanza kutumia mbinu salama kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu.


Dk Chang'a alisema miongoni mwa mbinu ambazo zinaweza kutumika ambazo wakulima walifundishwa ni jinsi ya kutumia vilipuzi,tochi zenye mwanga mkali,Vuvuzela zenye mlio mkali na pilipiki.


"vifaa hivi unaweza kuvitumia ukiwa shambani katika eneo ambalo limevamiwa na Tembo na ni rahisi kutumia bila kusababisha madhara kwa mkulima na Tembo"alisema


Alisema tayari wakulima 7110 ambao wapo katika vikundi 237 vya kudhibiti tembo wamepatiwa elimu na shirika  la Tembo Pilipili kwa kushirikiana na wadau wengine.


"tunashirikiana na shirika la Vision Fund ambao wanatoa mikopo ya fedha na pembejeo katika vikundi na hii ni inawezesha wakulima kufanya kilimo chenye tija"alisema


Alisema, wanufaika wa mradi huo ni kutoka katika maeneo yanayozunguka hifadhi za Taifa za Serengeti,  Mikumi, Ruaha, Tarangire, Lake Manyara, Hifadhi ya Nyerere, eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na pori la akiba la Maswa .


" unaweza kutumia Pilipili  kwenye kamba ya kudu ambayo hufungwa vitambaa imesaidia sana kudhibiti na kuokoa mazao maeneo mengi,"alisema.



Mtafiti wa Tembo wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini(TAWIRI) Muna Habibu alisema kutokana na wanyama hao kubadili tabia wakulima wanapaswa pia kuwa na mbinu tofauti kuwadhibiti Tembo.


"unatakiwa kubadili mbinu mara kwa mara ikiwepo mbinu ya kuwa na  Mizinga ya Nyuki pembezoni mwa shamba, kutumia Tochi za mwanga mkali,vuvuzela na vipulizi ambavyo ni rafiki kwa mazingira"alisema.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Minjingu Samwel Melami ameiomba halmashauri ya wilaya ya Babati  na jumuiya ya hifadhi wanyamapori ya Burunge kununua magari na kuongeza askari katika maeneo ambayo wananchi wanaathirika sana na tembo.


"Kwa kuwa tunapata fedha nyingi kupitia   Burunge WMA sasa  wanunue magari ili kuongeza ulinzi ,kwa kutumia mbinu hii ya Tembo pilipili na askari itasaidia  kupunguza migogoro"alisema.

Lekule ole Sindai, mkazi wa Kakoi alisema hivi sasa wanaume hawalali ndani kwa ajili ya ulinzi wa Tembo na wengine mazao yao yameliwa lakini hawajawahi kupata malipo.

"Tembo wamekuwa kero kubwa, tunashukuru kwa hii elimu lakini tunaomba msaada zaidi ili kuwadhibiti Tembo hawa"alisema

Akizungumza katika kongamano hilo,  kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri ya Babati, Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Benedict  Ntabagi alisema halmashauri hiyo, itaendelea kusaidia wakulima kukabiliana na Tembo.


"Tunajua changamoto zenu wakulima na ndio sababu tunashirikiana na wadau mbali mbali kuhakikisha tunadhibiti Tembo kufanya uharibifu wa mazao lakini pia kutishia usalama wetu"alisema.

Kongamano hilo la tisa la Wakulima, lilishirikisha pia maafisa mifugo na wanyamapori katika halmashauri za Babati,Monduli na Karatu na viongozi wa serikali katika wilaya hizo.



About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top