PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: UKAME NYANDA ZA MALISHO ULIVYOATHIRI MIFUGO NA UCHUMI WA WAKAZI WA LONGIDO
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Baadhi ya Viongozi wa kimila wilayani Longido wakiwa katika kikao cha kujadiliana njia bora ya kulinda nyanda za malisho ili mifugo ipate ch...


Baadhi ya Viongozi wa kimila wilayani Longido wakiwa katika kikao cha kujadiliana njia bora ya kulinda nyanda za malisho ili mifugo ipate chakula cha kutosha


 

Mwenyekiti wa kijiji cha Orbomba Kashilo Alais akielezea namna nyanda za malisho zilivyoathirika na ukame

Na: Andrea Ngobole, Longido


Jumla ya hekta 639,235 ambazo ni sawa na asilimia 82.14 ya hekta 778,575 za wilaya ya Longido zinafaa kutumika kwa ajili ya malisho ya mifugo na wanyamapori.

Hekta hizo hazijaendelezwa kwa ajili ya malisho bora ambayo ingesaidia mifugo kupata malisho ya uhakika kwa mwaka mzima.

Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ukame mkubwa na hatimaye uhaba wa malisho ya mifugo wilayani hapo.

Wataalamu wa hali ya hewa wanatafsiri mabadiliko ya tabianchi kuwa ni mabadiliko katika wastani wa hali ya hewa katika eneo fulani kwa muda mrefu mfano eneo liliokuwa na mvua ya kutosha na sasa mvua kunyesha chini ya wastani uliozoeleka.

Wilaya ya Longido inakadiriwa kuwa na mifugo 918,248, ambao ni Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo na Punda, hupata mvua ya wastani kiasi cha 500mm hadi 900mm kwa mwaka, hali inayosababisha ukame wa mara kwa mara.

Mifugo katika wilaya hiyo imeathirika kwa kukosa malisho ya uhakika. Hali duni ya mifugo imechangia kushuka kwa bei ya mifugo na kuathiri uchumi wa kaya za wilaya hiyo unaotegemea mifugo kama chanzo kikuu cha mapato yao ya kila siku.

Kijiji cha Kimokowa ni miongoni mwa vijiji vilivyoathirika na mabadiliko ya tabianchi. Mwenyekiti wa kijiji hicho Killel Mollel amesema wameamua kutenga maeneo ya nyanda za malisho ili kuyatunza kwa ajili ya malisho ya mifugo.

“Tumekumbwa na ukame mkubwa katika kijiji chetu hivyo tumeona ni vizuri kutenga maeneo maalumu ya malisho ambayo hayatavamiwa kwani tumejiwekea mpango bora wa matumizi ya ardhi ambayo yanakataza uvamizi wa maeneo hayo ili mifugo yetu ipate chakula muda wote,” amesema. 



Naomi Mollel mkazi wa kijiji cha Kimokowa amesema ameshuhudia ukame mkubwa kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2020 mpaka 2023 ambao umeathiri nyanda za malisho na kuathiri maisha yao kwa sababu wanategemea mifugo kupata mahitaji yao ya kila siku.

Anasema wameshauriwa na wataalamu wa mabadiliko ya tabianchi kuondoa mimea vamizi ili kuhakikisha nyasi za asili zinaota za kutosha katika nyanda za malisho ambazo zitasaidia kuipatia mifugo yao chakula cha kutosha kwa mwaka mzima.

David Laizer mkazi wa kijiji ncha Orbomba anakiri mifugo yake kufa kutokana na ukame na michache iliyopona analazimika kuipeleka nje ya kijiji hicho kutafuta sehemu yenye malisho ya kutosha.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Orbomba, Kashilo Alais anasema serikali ya kijiji imechukua hatua za haraka kudhibiti uchomaji wa mkaa na ukataji wa miti katika kijiji hicho ili kuwa na misitu itakayosaidia mvua kunyesha kwa kiwango cha kutosha.

 

Anasema serikali imechukua hatua hiyo baada ya kuona hali ya ukame imezidi na mifugo kufa na watu kuishi kwa tabau kwani mifugo ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya familia nyingi kijijini hapo. 

Aidha baadhi ya watafiti, wafugaji na wahifadhi wanasema kuwa nyanda hizo za malisho zinapaswa kutunzwa na kusimamiwa vema ili kuepusha kuvamiwa na mimea vamizi inayozuia uoto wa majani ya asili ambayo ni chakula cha mifugo.

Mimea hiyo vamizi ya Prosopis juliflora (Mrashia), Parthenium hysterophorus (Gugu Karoti), Astripomoea hyoscyamoides (Gugu Kongwa), Ipomoea hycanoides (ndelemeti), Chromolaena Odorata (Amachabongo), Dichrostachis cinerea (Ndunduru) Acacia nubica (Oldepe) na Solanum incunum (Ndulele) inatajwa kuathiri malisho ya wanyamapori na mifugo kwani licha ya kutoliwa na wanyama pia inazuia uoto wa majani ya asili ambayo ni chakula cha mifugo na wanyama hao.

Taarifa toka kwa mashirika ya TAWA, TNRF, CORDS, TAFORI na CABI yanayotekeleza miradi ya kupambana na mimea vamizi katika nyanda za malisho zinasema kuwa mimea hiyo vamizi imeathiri maeneo mengi ya nyanda za malisho katika wilaya ya Longido.

Mtafiti wa Taasisi ya utafiti wa Misitu (TAFORI), Dkt. Richard John amesema kumekuwa na ongezeko la mimea vamizi katika nyanda za maisho na kutaja miti ya mrashia ambao kitaalamu hujulikana kwa jina Prosopis Juliflora kuwa inaaathiri sana nyanda za malisho kwani hutumia kiasi kikubwa cha maji na hivyo kusababisha ukame.

Ameshauri kamati za mazingira za vijiji Wilayani Longido kuweka mkakati kabambe wa kuhakikisha miti hiyo inakatwa mapema na mimea vamizi inaondolewa ili kuongeza ustawi wa malisho ya mifugo katika maeneo maalumu yaliyotengwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt.Seleman Jafo, akiwa katika kikao cha siku nne na wadau wa mazingira jijini Arusha mwezi Oktoba mwaka 2022 kujadili mkakati wa nchi kuongeza uwezo wa kupata fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi alisema serikali imepanga kutumia dola za Marekani milion 19.2 ambazo ni sawa na shilingi bilion 44 za Tanzania kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.

 

Amesema Serikali inachukua hatua kubwa kama vile kuandaa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2023) na Miongozo na Kanuni za Biashara ya Kaboni, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

 

 Mpango huu wa serikali ukifanikiwa kuwafikia wakazi wa Longido na kamati zaa mazingira za kata na vijiji vikisimamia vema nyanda hizi za malisho huenda zitawanufaisha wafugaji wa wilaya ya Longido kuepukana na adha ya kukosa malisho ya mifugo iliyowakabili kwa kipindi cha miaka minne sasa.


Mbuzi na Kondoo wakiwa machungani katika nyanda za malisho zilizoathirika na ukame



About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top