WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WAIOMBA SERIKALI KUREJESHA ARDHI ZA WAKAZI WA LOLIONDO
Odero Charles Odero Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Elimu ya Uraia na msaada wa kisheria (CILAO) akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake mapema leo kuhusu hali ya haki za Binadamu katika maeneo ya Loliondo na Msomera
Baadhi ya wakazi wa kata ya Loliondo wakizungumza na watetezi wa haki za Binadamu walipofanya ziara katika eneo la Loliondo
NA: ANDREA NGOBOLE ARUSHA
Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania wameiomba serikali kusitisha zoezi la kubadili vijiji 14 na kuwa pori tengefu la Pallolet ili kulinda, kuhifadhi na kuendeleza haki za binadamu kwa wananchi wa Tarafa ya Loliondo na sehemu ya Tarafa ya Sale.
Ombi hili la watetezi wa haki za binadamu limekuja baada ya watetezi hao kufanya ziara mwezi Mei katika vijiji vya Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga, Tarafa ya Loliondo na Sale wilayani Ngorongoro mkoani Arusha ili kuangalia hali ya haki za binadamu katika maeneo hayo.
Odero Charles Odero, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la elimu ya uraia na msaada wa kisheria (CILAO) amewaambia waandishi wa habari jijini Arusha kuwa watetezi wa haki za binadamu wamegundua ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za ardhi, vijiji na uhifadhi wa wanyamapori.
Amesema ukiukwaji mwingine ni Watu kupigwa na kuumizwa wakati wa utekelezaji wa zoezi la kutwaliwa ardhi za vijiji hivyo, Viongozi na wawakilishi wa wananchi kukamatwa na kubambikiwa kesi ya mauaji na kisha kufutiwa kesi baada ya kukaa mahabusu kwa takriban miezi 6 na kuachiwa baada ya Jamhuri kusema haina nia ya kuendelea na kesi hiyo.
‘’Wananchi 92 walikamatwa na kufunguliwa shitaka la kuingia na kukaa nchini kinyume cha sheria kwa madai kwamba sio raia na baadaye kuachiwa huru na mahakama baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha madai yao au kudai haina nia ya kuendelea na kesi yao.” Alisema bwana Odero.
Watetezi hao pia wamesema wameshuhudia Ukamataji na utaifishaji wa mifugo na kupiga faini kubwa kwa kile kinachodaiwa kwamba mifugo hiyo imeingia kwenye eneo la pori la Pololeti na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuwasababishia umaskini mkubwa wananchi hao.
Amesema Mifugo ime kufa kwa sababu ya kukosa eneo la malisho, maji na chumvi na kusababisha Umasikini kwa wananchi kutokana na kupoteza mifugo kutokana utaifishaji,mifugo kufa kutokana kukosa maji na majani kwani eneo lililochukuliwa ndilo llikuwa tegemeo la wananchi kufanyia shughuli za ufugaji.
Watetezi hao wameiomba serikali kutekeleza yafuatayo.
1. Serikali ifute Tangazo lake la Juni 2022 lililofanya eneo la Vijiji 14 kugeuzwa kuwa Pori Tengefu la Pololeti.
2. Serikali ifute Tangazo lake la Oktoba mwaka 2022 lililofanya eneo la vjjiji kugeuzwa kuwa eneo la Pori la Akiba la Pololeti.
3. Serikali izingatie Sheria na Utawala Bora katika kutimiza majukumu yake ili kulinda na kutetea haki za Binadamu kama Katiba inavoeleza kwenye Ibara yake ya 9 (e) na (f)...Heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Knuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu.
Watetezi hao wamewaomba Wadau mbali mbali wa Maendeleo kujitoa kusaidia familia kwa misaada ya kiutu ambazo zimeathirika kwa njaa kwenye eneo la Tarafa ya Loliondo na Sale baada ya kupoteza mifugo na wengine kupoteza wenza wao na wengine kuwa vilema.
wameomba Viongozi wa dini nchini Tanzania kama Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) waunde kamati kutembelea eneo la Tarafa ya Loliondo na sehemu ya tarafa ya Sale ili wajionee wenyewe hali ya haki za binadamu kwani wanaamini kwamba wao bado wana nafasi ya sauti kinabii kuikemea, kuishauri na kuiombea serikali kutimiza majukumu yake ya usatwi wa wananchi.
Post a Comment