Mwandishi wetu, Arusha
Taasisi ya wanahabari ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC) imekabidhiwa rasmi leseni ya kutoa huduma za habari za mtandaoni kutoka Mamlaka ya mawasiliano Tanzania(TCRA).
Kutolewa kwa leseni hiyo sasa kutaiwezesha MAIPAC kupanua wigo wake wa utoaji habari za jamii za pembezoni na hivyo kusaidia kuchochea maendeleo katika jamii hizo na kukabiliana na changamoto kadhaa , ikiwepo athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Mkurugenzi mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma na Meneja Utawala wa MAIPAC Andrea Ngobole,wamekabidhiwa leseni hiyo na Afisa TEHAMA mwandamizi wa TCRA, Julius Felix katika hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za TCRA kanda ya Kaskazini.
Akizungungumza mara baada ya kukabidhiwa leseni ya usajili, Juma alisema itasaidia sana kuweza kutoa habari nyingi za jamii za pembezoni ambazo zipo nyuma kutokana na kuendeleza tamaduni na mila zao za asili.
"Tunashukuru TCRA kutupa Leseni hii kwani itasaidia utoaji wa habari nyingi za jamii za pembezoni, hasa katika kipindi hiki MAIPAC ikiwa inatekeleza mradi wa matumizi ya maarifa ya asili katika utunzwaji wa mazingira mradi ambao unadhaminiwa na shirika la maendeleo la umoja wa mataifa(UNDP) kupitia programu ya miradi midogo"alisema
Alisema mradi huo, ambao pia unadhaminiwa na Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) kupitia UNDP unaratibiwa na jumuiko la Maliasili Tanzania(TNRF).
Juma alisema mikakati ya MAIPAC kwa Sasa ni kuwa na Luninga, kuwa na Radio na kuwa na Kituo cha Taarifa za Jamii za Pembezoni (indigenous resources center) ili kusaidia kuchochea maendeleo ya jamii hizo.
Naye Meneja utawala wa MAIPAC, Ngobole aliwataka wanachama wa MAIPAC nchi nzima kutumia fursa hiyo ya usajili kwenda kuandika habari za uchunguzi juu ya jamii za pembezoni.
"tunatarajia wanachama wetu wataitumia vizuri MAIPAC MEDIA TANZANIA kuandika habari ambazo zitachochea maendeleo ya jamii za pembezoni, ikiwepo kushiriki kupata chanjo ya Uviko-19, kushiriki katika vita dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto"alisema
Afisa TEHAMA mwandamizi wa TCRA, Felix alipongeza MAIPAC kwa kupata usajili na kuwataka kufanyakazi kwa kuzingatia sheria na kanuni.
Post a Comment