Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt
Hamisi Kigwangalla akizungumza bungeni alipokuwa akijibu hoja wa
wabunge waliochangia mjadala wa bajeti wa kupitisha makadirio ya mapato
na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma
juzi.
.............................. ..............................
Wizara
ya Maliasili na Utalii imetangaza kuanza mchakato wa kuyapandisha hadhi
Mapori ya Akiba ya Burigi, Kimisi, Biharamulo, Ibanda na Rumanyika kuwa
Hifadhi za Taifa.
Mchakato huo tayari umeungwa mkono na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Hayo
yameelezwa juzi bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati akihitimisha mjadala wa bajeti wa
makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha
2018/2019.
“Mheshimiwa
Spika, ninaomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa Mhe. Rais ameridhia
ombi letu la kupandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Burigi, Kimisi,
Biharamulo, Ibanda na Chief Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa, kipekee
namshukuru sana Mhe. Rais kwa kuridhia ombi letu hilo” amesema Dkt.
Kigwangalla.
Amesema
kufuatia hatua hiyo, wizara yake inaanzisha mchakato rasmi wa
kukamilisha taratibu za kupandisha hadhi mapori hayo ili kupanua wigo
wa vivutio vya utalii katika kanda ya Kaskazini Magharibi na hivyo
kufikia azma ya Serikali kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 8 na
mapato ya dola za kimarekani bilioni 16 katika kipindi cha miaka 7
ijayo.
Inaelezwa
kuwa mchakato huo utapitia hatua mbalimbali ikiwemo kuwashirikisha
wadau husika kupata maoni yao, mapendekezo kuwasilishwa baraza la
mawaziri kabla ya kujadiliwa bungeni na hatimaye kuwasilishwa kwa Mhe.
Rais kwa ajili ya kuidhinishwa kuwa Sheria kamili ya kupandisha hadhi
mapori hayo.
Akizungumzia
mikakati mingine mipya ya kuboresha sekta ya maliasili na utalii
itakayotekelezwa, Dkt. Kigwangalla amesema ni pamoja na kuanzisha
mamlaka ya usimamizi na uendelezaji wa utalii wa fukwe nchini, kuhuisha
maeneo ya vivutio vya Mambo ya Kale na kuviunganisha katika 'package'
moja ya utalii na vivutio vya wanyamapori.
Mikakati
mingine ni kuunda mfumo mmoja funganishi wa TEHAMA uitwao "MNRT Portal"
kwa ajili ya kutoa leseni na vibali, ukusanyaji wa takwimu na mapato
kutoka vyanzo mbalimbali vya sekta ya maliasili na utalii, ambapo
utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali iliwemo GePG, NIDA, TIRA,
BRELA, TRA na NBS.
Amesema
mikakati mingine ni kuanzisha Jeshi Usu, Utambulisho wa Utalii wa
Tanzania Kimataifa ujulikanao kama "Tanzania, Unforgettable", kufungua
utalii wa kanda ya kusini, kuanzisha mwezi wa maadhimisho ya Urithi wa
Mtanzania "Urithi Festival" (Septemba), kuhuisha sheria za TANAPA, TAWA
na TFS, pamoja na kuunda kanuni mpya za kusimamia vizuri sekta hizo.
Pori
la Akiba Burigi lina ukubwa wa kilomita za mraba 2,941 katika wilaya za
Karagwe, Muleba na Ngara mkoani Kagera, wakati Pori la Kimisi likiwa na
ukubwa wa kilomita za mraba 1,030 katika wilaya za Ngara na Karagwe
mkoani humo.
Pori
la Akiba Biharamulo lina ukubwa wa kilomita za mraba 731 katika wilaya
ya Muleba mkoani Kagera na wilaya ya Chato mkoani Geita, huku Pori la
Akiba Ibanda likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 200 na Pori la Akiba
Rumanyika kilomita za mraba 800 katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Mapori haya yapo katika ukanda muhimu wa kuunganisha watalii kutoka ikolojia za Magharibi na Mashariki ambapo uwanja wa ndege wa Chato utakuwa muhimu katika kutoa mawasiliano.
Mapori haya yapo katika ukanda muhimu wa kuunganisha watalii kutoka ikolojia za Magharibi na Mashariki ambapo uwanja wa ndege wa Chato utakuwa muhimu katika kutoa mawasiliano.
Mapori
hayo ambayo yanasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania - TAWA sasa yatakuwa chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa
Tanzania - TANAPA punde baada ya mchakato wa kuyapandisha hadhi
kukamilika.
Bunge
limeidhinisha Sh. bilioni 115.794 kwa ajili ya makadirio ya mapato na
matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/2019
ambapo Sh. bilioni 85.816 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh.
bilioni 29,978 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza bungeni alipokuwa
akijibu hoja wa wabunge waliochangia mjadala wa bajeti wa kupitisha
makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha
2018/2019, jijini Dodoma juzi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt
Hamisi Kigwangalla na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet
Hasunga wakipongezwa na wabunge mbalimbali baada ya bajeti ya wizara yao
kupitishwa na Bunge juzi jioni.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa - TANAPA na Mkuu wa Majeshi
Mstaafu, Jenerali George Waitara (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini wa Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania - TAWA, Meja
Jenerali (Mstaafu) Hamis Rajabu SEMFUKO wakiwa kwenye picha ya pamoja
nje ya ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya bajeti ya Wizara ya Maliasili
na Utalii kupitishwa na Bunge.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt
Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet
Hasunga, Katibu Mkuu, Maj. Gen. Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu,
Dkt. Aloyce Nzuki, Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi pamoja na
wafanyakazi wa wizara hiyo baada ya bajeti ya wizara yao kupitishwa na Bunge juzi jioni.
Post a Comment