Na Benny Mwaipaja, WFM-Dar es
Salaam
Serikali
ya Tanzania imetiliana saini na Serikali ya China mkataba wa msaada wa kiasi
cha Shilingi Bilioni 146.47. Mkataba huo umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya
Fedha na Mipango Dotto James na Balozi wa China nchini Wang Ke Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
baada ya kusaini mkataba huo Katibu Mkuu alisema kuwa fedha hizo ni msaada na
siyo mkopo na zitatumika katika miradi miwili ya miundombinu. Mradi wa kwanza
ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) ambacho kitajengwa
Mabibo Jijini Dar es Salaam kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 62 sawa na
takriban Shilingi bilioni 138.3.
Mradi
wa pili ni kwa ajili ya kusaidia upembuzi yakinifu na upembuzi sanifu wa mradi
wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR), ambapo kiasi cha Sh.
bilioni 3.2 kimetengwa kwa ajili hiyo.
Bw.
Doto James alisema kwa sasa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha
Kimataifa umeanza kwa awamu mbili ambazo moja ni kuanzia Dar es Salaam hadi
Morogoro, na kuanzia Morogoro hadi Makutopora-Dodoma, upembuzi yakinifu
utakaofanywa na Serikali ya China ni kwa maeneo mengine ya ujenzi wa Reli hiyo
kuanzia Dodoma, Tabora hadi Mwanza na Kuanzia Kaliua hadi Kigoma.
"China
imetusaidia miradi mingi ikiwemo mradi wa maji Chalinze, Ujenzi wa uwanja wa
Michezo wa Taifa, Mradi wa teknolojia za Kilimo mkoani Morogoro, Kituo cha
upasuaji wa moyo na mafunzo, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Nyerere
pamoja na misaada ya dawa na vifaa tiba" alieleza Bw. James
Kwa
upande wake Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke, Alisema
kuwa China inategemea kuona kuwa msaada huo utasaidia kuimarisha maendeleo na
kuisaidia Tanzania kupata maendeleo haraka.
Aidha
alisema China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi
mbalimbali ya kimaendeleo ambayo itawasaidia Watanzania na kuendeleza urafiki
uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Balozi
Wang Ke, amesema Pia Serikali ya China na Tanzania zinaendelea majadiliano
kuhusu ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, na kuongeza kuwa majadiliano hayo
yatakapokamilika nchi yake itasaidia ujenzi wa bandari hiyo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji Taifa (NIT) Prof. Zacharia Mganilwa
ameishukuru Serikali ya China kwa msaada huo na kusema kuwa msaada huo
utaisaidia chuo hicho kuweza kutoa wataalamu wa kutosha
kuweza kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo sekta ya anga.
Amebainisha
kuwa Chuo hicho Kikuu kitatoa mafunzo kwenye fani muhimu na zinazohitajika
ikiwemo ufundi wa reli, masuala ya anga na sekta nyingine mtambuka kwa kutoa
wataalamu waliobobea watakao changia kufanikisha azma ya Serikali ya uchumi wa
viwanda.
Kwa
upande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi Uendeshaji wa Shirika la Reli Tanzania-TRC,
Bw. Focus Msasani ameeleza kuwa msaada huo wa shilingi bilioni 3.22, utasaidia
kuipunguzi serikali gharama ilizokuwa izitumie kwa kazi hiyo kenye mradi mkubwa
wa kihistoria wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa.
Post a Comment