Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri
wakipanda mti wa kumbukumbu wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya
upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya
ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Na Hamza Temba, WMU, Kishapu, Shinyanga
.............................. .............................. ...........................
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewaagiza Wakuu wa
Mikoa nchini kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinatenga maeneo katika
kila kijiji kwa ajili ya uhifadhi wa misitu ikiwa ni pamoja na vijiji
hivyo kuunda kanuni na taratibu zao wenyewe za kusimamia maeneo hayo.
Ametoa
agizo hilo jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani
Shinyanga wakati wa kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Upandaji Miti
Kitaifa yaliyofanyika mkoani humo kuanzia Aprili 03 mwaka huu.
Katika
kufanikisha zoezi hilo ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) kuchagua mikoa 10 ya kuanza utekelezaji wa agizo hilo
ikiwemo mikoa ya Shinyanga na Tabora ambayo inakabiliwa na changamoto
kubwa ya uharibifu wa misitu.
Ameugiza
pia we uongozi huo wa TFS kuweka mpango wa uhifadhi wa misitu ya asili
katika maeneo hayo kwa kushirikiana na vijiji kupanga maeneo
yanayostahili kuhifadhiwa sambamba na kuwapa elimu ya umuhimu wa
uhifadhi wa maeneo hayo.
Wakati
huo huo Dk. Kigwangalla ametoa siku saba kwa uongozi huo wa Wakala wa
Huduma za Misitu kuwasilisha kwake mpango wa tathmini ya uvunaji wa
mazao ya misitu wa nchi nzima kwa kuzingatia kiasi cha rasilimali misitu
kilichopo na kiwango halisi kitakachotakiwa kuvunwa ambacho hakitazidi
robo ya rasilimali iliyopo.
"Hatuwezi
kuendelea tu kutoa vibali vya kuvuna misitu hatujui tunavuna wapi, tuna
rasilimali kiasi gani, wavune kiasi gani, hapana, mnitengenezee mpango
laa sivyo nitasitisha uvunaji, nikisema nasitisha uvunaji nitapeleka
waraka kwa Wakuu wa Mikoa, na nina uhakika kwa nguvu walinayo
hawashindwi kuzuia uvunaji.
"Kwahiyo
TFS nawapa siku saba mniletee mpango wa tathmini ya namna ambavyo tuna
rasilimali kwenye kila mkoa, tujue mkoa flani una miti cubic mita kadhaa
ya mbao kadhaa, ya kuni kadhaa, ya mkaa kadhaa na kwa mwaka huu
tutaruhusu wavune kwenye msitu fulani kiasi kadhaa, twende kisayansi,
sio Meneja wa TFS anakaa Wilayani anatoa vibali watu wanaenda kuvuna,".
Dk.
Kigwangalla amesema takwimu za uharibifu wa misitu hapa nchini
zinatisha jambo ambalo likiachwa liendelee bila kuchukua hatua nchi
itageuka kuwa jangwa.
"Kwa mwaka tunakata miti kwa mahitaji mbalimbali kati ya ekari 800,000 na 1,200,000.
Ili
kurejesha walau nusu ya miti tunayokata kwa mwaka tunahitaji kupanda
miti 3,000,000 kwa mwaka mfululizo kwa miaka 17 ili kufidia kiasi cha
uharibifu tunachofanya kwa nusu mwaka" alisema Dk. Kigwangalla.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Dk. Ezekiel Mwakalukwa ambaye alimuwakilisha Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo alisema kumekuwepo na jitihada za kuandaa programu
kubwa za kitaifa za uhifadhi wa mazingira katika maeneo mahususi
yaliyoonekana kuzidiwa na tatizo la uharibifu wa mazingira.
Alitaja Programu hizo kuwa ni Hifadhi Ardhi Dodoma (HADO), Hifadhi Ardhi Shinyanga (HASHI), na Hifadhi Mazingira Iringa (HIMA).
Mkuu
wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema mkoa wake kwa kushirikiana
na uongozi wa mkoa wa Tabora umeanza kuchukua hatua za kurejesha uoto wa
asili katika maeneo yao ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kugawa miche ya
miti kwa kila kaya pamoja na kuimarisha kamati za uhifadhi wa mazingira.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Taboba, Aggrey Mwanri alisema ushirikiano huo ni muhimu
kwani utawezesha kukabiliana na changamoto zilizopo katika mikoa hiyo
kwa kuweka mikakati ya pamoja wa kudhibiti vitendo vya uharibifu wa
mazingira kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyopo.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri
wakipanda mti wa kumbukumbu wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya
upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya
ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwahutubia wananchi wakati wa kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga jana.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri
wakiteta jambo wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti
kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu
mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akiwahutubia wananchi wakati wa maadhimisho hayo.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri
wakiwasalimu wananchi wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji
miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya
Kishapu mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi
wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk.
Ezekiel Mwakalukwa ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
akitoa maelezo kuhusu maadhimisho hayo.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri
wakielekea eneo la tukio la kupanda miti wakati wa kilele cha
kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika
kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akishiriki kucheza ngoma wakati wa maadhimisho hayo.
Post a Comment