Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limesema
tukio la kutekwa kwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications
Limited (MCL), Azory Gwanda limeongeza hofu kwa waandishi wa habari nchini hasa
wale wanaoripoti habari za uchunguzi
Pia, TEF imesema matukio ya kuzuiwa kwa
mikutano ya siasa, kushambuliwa kwa mwanasiasa Tundu Lissu, mauaji ya Kibiti na
kufungiwa kwa vyombo vya habari, hayana afya kwa Taifa
Gwanda alitoweka tangu Novemba 21 mwaka jana
na mpaka sasa hajulikani alipo
Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile
alisema jana kuwa jukwaa hilo limetafakari kwa kina na kujadili hali inayoibua
sintofahamu na malalamiko kutoka katika makundi mbalimbali ndani ya jamii
“Kuminywa kwa uhuru wa maoni, athari yake ni
kikwazo cha utendaji na ufanisi wa vyombo vyetu vya habari huku hofu ikiwafanya
wananchi kusita kuzungumza na vyombo vya habari wanapohitajika kufanya hivyo,”
alisema Balile
Alisema malalamiko mengi yaliyo katika jamii
yanagusa kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni hasa kupitia vyombo vya habari,
kuzorota kwa demokrasia nchini kwa ujumla wake na ukuaji wa uchumi usioakisi
hali halisi ya watu
Alisema vyombo vya habari nchini vinafanya
kazi katika mazingira magumu na ya woga kutokana na watendaji wake kuitwa na
kuhojiwa na mamlaka kama Idara ya Habari –Maelezo kwa magazeti na Mamlaka ya
Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa vyombo vya kielekroniki
“Na wakati mwingine kupewa adhabu kubwa za
kulipa faini au kufungiwa na baadhi ya adhabu nyingine kama kufungia magazeti
zikitolewa kinyume cha Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016,” alisema
Balile
Alipoulizwa kuhusu taarifa ya TEF, Msemaji
wa Serikali, Dk Hassan Abbas alisema, hajaipata. Hata alipoelezwa maudhui ya
taarifa hiyo aliomba atumiwe ili aisome na alipotumiwa hakupatikana tena
kuizungumzia
Kuhusu mikutano ya vyama vya siasa Balile
alisema, imezuiwa kinyume cha sheria huku vyama vya upinzani vikiathiriwa zaidi
kwa kuwa watendaji wa chama tawala wanaendelea na shughuli za kisiasa kama
kawaida
Kadhalika, Balile alieleza kuwa matukio ya
mauaji ikiwamo ya Kibiti, ya Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
(NIT) Akwilina Akwiline, askari wanane Kibiti, mashambulizi ya risasi kwa
Lissu, yamezidisha woga kwa wanahabari kwa kuwa hayajapata majibu ikiwamo
wahusika kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. “Tunayo mifano ya
nchi nyingi duniani, zilizoingia katika gharama kubwa kwa kudharau matukio
madogo kama yanayotokea nchini mwetu hivi sasa,” alisema
Balile alisema TEF, kama wataalamu wa habari
wanaotazama mambo kwa jicho la kiuchambuzi, wanashauri kuwapo kwa meza ya
mazungumzo kitaifa kwa Serikali kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii ili
kujadiliana kuhusu mustakabali wa amani na maridhiano ya kitaifa
Hata hivyo, Balile alisema TEF inapongeza na kutambua juhudi za Serikali za kusimamia misingi ya uwajibikaji, vita dhidi ya rushwa na ufisadi na usimamizi wa mapato ya Serikali na matumizi endelevu ya raslimali za umma.
Post a Comment