Shimo lililosababisha ajali iliyoua watu 12
Igunga mkoani Tabora, limezua mjadala bungeni jana, huku waziri wa mambo ya
ndani ya nchi, Dk Mwigulu Nchemba akiliagiza jeshi la polisi kuwaweka ndani
madereva wanaoendesha kwa kasi
Mjadala huo ulizuka, baada ya mbunge wa
Ulanga, Mashariki (CCM) Goodluck Mlinga kuhoji kuhusu ajali hiyo iliyotokea
juzi na kusema kuwa kama chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa barabara, basi
Serikali haina budi kuitoza faini Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads
Katika mwongozo wake, Mlinga alisema ajali
hiyo imesababishwa na ubovu wa barabara na hivyo akataka Tanroads itozwe faini
kama askari wa usalama barabarani wanavyowatoza madereva wazembe
Ajali hiyo iliyotokea juzi, ilihusisha basi
la abiria la City Boy na lori. Mbali ya kusababisha vifo hivyo vya watu 12,
wengine 43 walijeruhiwa
Hata hivyo, akijibu mwongozo huo, Waziri
Nchemba alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi lakini akaongeza kuwa lori
ambalo ndilo lililosababisha ajali hiyo lilikuwa likikwepa shimo ndipo moja ya
kifaa cha tairi kilipokakatika na kupoteza mwelekeo kisha kugonga basi
“Kama jana nilivyosema kuwa tunapotoza faini
lengo letu si kupata ile fedha, lakini lengo letu ni kuwakumbusha madereva kuwa
wanatakiwa kutokwenda kwa mwendo wa kizembe na kasi unaoweza kusababisha
madhara hayo,” alisema
Alisema kutokana na watu kutozwa faini,
wanachukulia adhabu hiyo kama mazoea na kudhani lengo ni kukusanya fedha wakati
lengo ni kulinda usalama wao, “Naelekeza polisi watakapokamata dereva yeyote
anayekwenda mwendo kasi pamoja na hiyo ya kuwatoza faini, wamuweke ndani hadi
aende mahakamani. Kama rekodi yake ni mbaya, anyang’anywe leseni asiendelee
kuendesha magari na kusababisha ajali.”
Wakati Dk Nchemba akisema hayo bungeni,<br/>Rais Magufuli mbali
na kutoa pole kutokana na ajali hiyo, amewataka viongozi wote wanaohusika na usimamizi wa usalama barabarani kutafakari kwa nini ajali nyingi zimekuwa zikitokea katika maeneo yaleyale na kutafuta ufumbuzi ili kuepusha madhara ya watu kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na kupoteza mali
Rais Magufuli katika taarifa yake
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais
Ikulu, Gerson Msigwa amesema, “Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa
taarifa za vifo vya watu 12 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani jana
usiku (juzi) katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, nawapa pole wafiwa wote, ndugu,
jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu mkubwa
“Aidha, nalitaka Jeshi la Polisi, kamati za
ulinzi na usalama za mikoa na wilaya na mamlaka zote zinazohusika na usalama wa
barabarani kujitathmini na kutafuta majawabu ya kwa nini ajali za barabarani
zinaendelea kutokea kwa kusababishwa na uzembe na uvunjaji wa sheria za
barabarani.”
Kuhusu ajali hiyo, kamanda wa Polisi Mkoa wa
Tabora, Wilbroad Mutafungwa alisema ilitokea baada ya lori lililokuwa likikwepa
shimo kupasuka tairi hivyo dereva kushindwa kulimudu na kugongana uso kwa uso
na basi kabla ya kupinduka
Majeruhi wawili walipelekwa Hospitali ya
Rufaa ya Bugando, Mwanza na mmoja alipelekwa Hospitali ya Nkinga na 43
walitibiwa katika Hospitali ya wilaya Igunga na miili sita kati ya 12,
imetambuliwa na ndugu zao na mmoja wao ni mhasibu wa Halmashauri ya wilaya ya
Igunga, Harold Nyamwangi.
Post a Comment