Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba akitoa taarifa ya Mradi
wa Ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa vya kuhifadhia chakula
wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi huo Mtaa wa
Relini-Kizota Mjini Dodoma, Jana 21 Aprili 2018. Picha Na Mathias Canal-NRFA
Na Mathias Canal, NFRA-Dodoma
Hali
ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini inazidi kuimarika huku
serikali kupitia wizara ya kilimo ikiwa imejipanga kukabiliana na
changamoto ya uchache wa maghala ya kuhifadhia mazao mbalimbali hususani
mahindi.
Katika taarifa ya Bi Vumilia L. Zikankuba Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula katika hafla ya kuweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi
wa vihenge na maghala ya kisasa katika Mtaa wa Relini-Kizota Mjini
Dodoma aliyoitoa mbele ya mgeni rasmi-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) jana tarehe 21 aprili, 2018 alieleza kuwa mradi huo pindi utakapokamilika utafungua fursa kubwa kwa wakulima nchini.
Alisema
kuwa Baada ya Mradi huu kukamilika uwezo wa kuhifadhi wa Wakala wa
Taifa wa Kuhifadhi Chakula utakuwa mara mbili ya uwezo wa sasa yaani
kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000 huku ikitarajiwa kufikia Tani
700,000 kufikia mwaka 2025.
Bi
Vumilia alieleza kuwa Mikataba ya mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi
chakula, ilisainiwa na kuanza kazi tarehe 09 Desemba 2017 kati ya (NFRA)
na makampuni mawili toka nchini Poland ambayo ni Feerum S.A na Unia
Araj Realizacje Sp.o.o. Aidha, mradi huo utatekelezwa kwa gharama ya
Dola za kimarekani milioni 55 na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi
cha miezi kumi na nane (18) kuanzia mwezi Mei 2018.
Maandalizi
ya awali ya mradi huo yalifanywa na kampuni kutoka nchini Poland
iliyofanya upembuzi yakinifu wa awali na kupendekeza gharama za mradi
kuwa dola za kimarekani millioni 55 ambazo zingetosheleza kujenga
vihenge vyenye uwezo wa Tani 150,000 na maghala yenye uwezo wa Tani
50,000, hivyo kufanya uwezo wa jumla wa mradi kuwa Tani 200,000.
Alisema,
ili kujiridhisha zaidi Wakala kupitia Wizara mama, iliunda timu ambayo
ilifanya upya tathmini ya mradi na kupata thamani halisi ya mradi (value
for money) ili kuleta ushindani katika utekelezaji wa mradi kwa
kushirikisha timu ya Wataalamu wa ndani.
Timu
hiyo iliundwa na Wahandisi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,
Mhandisi na Wataalamu wa mazingira kutoka TBA pamoja na Mhandisi toka
Wizara ya Kilimo. Hivyo timu hiyo ilifanya upya kazi ya usanifu wa
msingi, kuandaa makadirio ya gharama za mradi, na kuandaa makabrasha ya
zabuni ili kutimiza azma mbili nilizotangulia kuzitaja hapo awali.
Matokeo
ya jumla ya kazi hiyo, yalibainisha kuwa kiasi cha fedha Dola milioni
55 kinatosheleza ujenzi wa vihenge vya kisasa vyenye uwezo wa kuhifadhi
Tani 190,000, na maghala Tani 60,000 hivyo kufanya ongezeko la hifadhi
ya Tani 50,000.
Aidha,
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unamiliki maghala ya kuhifadhi
nafaka 34 yenye uwezo wa jumla ya Tani 251,000. Uwezo huu wa sasa wa
maghala hautoshelezi mahitaji ya dharula ya chakula kwa mfululizo wa
miezi mitatu kwa akiba isiyo pungua Tani 700,000, hivyo kupelekea
uhitaji wa kuongeza uwezo wa uhifadhi.
Post a Comment