Mgogoro wa uongozi ndani ya CUF unaendelea
kukitikisa chama hicho baada ya jana katibu mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad
kusema Profesa Ibrahim Lipumba hana uwezo wa kumfukuza uanachama huku
akimwambia, “Sifukuziki
Maalim Seif alitoa kauli hiyo jana katika
kongamano la kujadili mwenendo wa CUF lililofanyika Tandale jijini Dar es
Salaam, kumjibu Profesa Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho
anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Kauli ya makamu huyo kwa kwanza wa Rais wa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka 2010 hadi 2015, imekuja siku mbili
baada ya Profesa Lipumba kusema Maalim Seif atajadiliwa na kamati ya maadili na
nidhamu ya chama hicho kwa utovu wa nidhamu na kudhoofisha CUF
Katika kile kilichoonekana kumjibu Profesa
Lipumba, katibu mkuu huyo alisema kamwe hatakwenda kuhojiwa kwenye kamati hiyo
aliyodai ni haramu akisema ipo kinyume cha sheria na taratibu za chama hicho
“Nitabaki kuwa katibu wa chama hiki hadi
uchaguzi wa CUF utakapofanyika mwakani. Kamati ya maadili inamwita Seif, Seif
yupi? Siwezi kuungana na wasaliti hata siku moja na wasijisumbue,” alisema
Alidai kwamba kuna mipango inaratibiwa ya
kumfukuza katika wadhifa wake ili nafasi hiyo apewe kiongozi mmoja wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ
“Kiongozi huyo akiwa katibu mkuu, atapata
fursa ya kugombea urais wa Zanzibar lakini ninawaeleza kamwe hawawezi
kufanikiwa,” alisema Maalim Seif
Akijibu madai hayo, mkurugenzi wa habari na
mawasiliano kwa umma (CUF Lipumba), Abdul Kambaya alisema anachokifanya katibu
mkuu huyo ni sawa na kupiga ramli akisema kitendo chake cha kutofika ofisi za
chama hicho, sawa na kujifukuza
“Maalim Seif alishajifukuzisha CUF kwa
sababu hafiki ofisini Buguruni. Kwa hiyo hatuwezi kufukuzana na kulumbana na
kivuli chetu wenyewe,” alisema
Katika kongamano hilo, Maalim Seif pia
aligusia jinsi Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulivyompokea aliyekuwa
mgombea urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Edward Lowassa na
kubainisha kuwa Profesa Lipumba alishiriki kumleta, jambo ambalo mara kadhaa
msomi huyo amekuwa akilikanusha
Pia, Maalim Seif alisema hivi karibuni
atafanya ziara kisiwani Pemba na kusema anataka kujihakikishia kama kweli
Profesa Lipumba ana wafuasi wengi kisiwani humo kama alivyodai baada ya ziara
yake mwezi uliopita
“Ninawataka wanachama wa CUF kuendelea na
mshikamano maana haki itapatikana. Mjitokeze kwa wingi katika kesi zinazoendelea
mahakamani. Tuamini kuwa haki itatendeka,” alisema Maalim Seif
Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa CUF (upande wa Maalim Seif), akiwemo mkurugenzi wa uchaguzi,
Sheweji Mketo na naibu katibu mkuu, Joran Bashange na madiwani
Katika kikao cha baraza la uongozi kilichofanyika Machi 22, Profesa Lipumba alidai kuwa Maalim Seif ameidhoofisha CUF kwa kuwakumbatia viongozi wa Chadema na kutotekeleza azimio la Baraza Kuu la kufungua kesi Mahakama Kuu ya Zanzibar kupinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa wawakilishi na madiwani ambao alisema walikabidhiwa hati za ushindi wa majimbo na Shehia zao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Post a Comment