SIKU tatu zikiwa zimepita tangu kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa
cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Maftah (22), imeelezwa alipanda
daladala ambalo mauti yalimfika humo akipeleka barua ya kuomba kufanya
mazoezi kwa vitendo aliyokuwa akitarajia kuanza Jumatatu ijayo mkoani
Pwani.
Akwilina alipigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni,
Kinondoni na polisi waliokuwa wakijaribu kutawanya maandamano ya wafuasi
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ijumaa jioni.
Rais John Magufuli jana alisema katika akaunti yake ya mtandao wa
kijamii ya Twitter kuwa "Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi
na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili."
Rais Magufuli pia alielezea kusikitishwa "sana" na kifo cha Akwilina, na
kutoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na
msiba huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako
alisema marehemu alikuwa ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya
juu.
Aidha, Prof. Ndalichako alisema siku ya Ijumaa Akwilina alikuwa njiani
kupeleka barua ya kuomba kufanya kazi kwa vitendo katika moja ya kampuni
zilizopo Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Marehemu alipanda daladala linalofanya safari kati ya Mabibo na
Makumbusho katika kituo cha NIT na kufuatia maelezo ya waziri kwamba
alikuwa akielekea Bagamoyo, ilikuwa ashuke mwisho wa safari kabla ya
kuunganisha daladala nyingine kwenda Bunju Sokoni au Tegeta Nyuki zilizo
stendi za Bagamoyo.
Taarifa za kipolisi zilizotolewa jana zilisema mwili wa marehemu
aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma katika daladala hiyo yenye namba T558
CSX aina ya Nissan Civilian, ulikutwa ukiwa na jeraha kubwa kichwani
lililooneka kutokana na kupigwa na kitu chenye ncha kali, kilichoingia
upande wa kulia na kutoka upande wa kushoto.
Prof. Ndalichako alisema Akwilina alikuwa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Ununuzi na Ugavi katika chuo hicho.
"Wizara yangu itagharamia mazishi yake hadi hapo atakapopumzishwa katika
makao yake ya milele," alisema Prof. Ndalichako. "Tutasimamia shughuli
zote za msiba huo.
"Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki... kwa uongozi wa NIT, kwa wanafunzi na wananchi wote.
"Serikali imepata pigo kubwa kwa sababu inawekeza pesa nyingi katika
kuwasomesha wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu kwa
kuwapa mikopo."
FUNDISHO KWA MTU Akirejea agizo la Rais Magufuli la vyombo vya dola
kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio
hili, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni
alisema:
Uchunguzi utakapokamilika serikali itatoa taarifa ambayo itakuwa
fundisho kwa mtu mwingine kusababisha hali kama hiyo kutokea tena.
Aidha, Masauni alisema siasa isiwe chanzo cha watu kufariki au kuwa
walemavu.
Alisema serikali kwa sasa inataka kujiridhisha undani wa tukio hilo
lilivyotokea bila ya kumuonea mtu yoyote, na kwamba uchunguzi
hautachukua muda mrefu.
"Nani anajua ile risasi ilitoka kwa nani? Kama yupo anayejua aje
atuambie, kwa sasa maiti ipo hospitali tunasubiri taarifa, hatuwezi
kukurupuka tu," alisema Masauni.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilishasema
mapema jana linawashikilia askari wake sita kufuatia tukio hilo na
silaha zao zinachunguzwa, ikiwa ni pamoja na kuzipeleka kwa wataalamu wa
milipuko kwa uchunguzi wa kina.
Aidha, jeshi hilo lilisema limeunda timu ya upelelezi ili kuchunguza chanzo cha kifo cha binti huyo.
Post a Comment