Mwandishi Wetu,Arusha
Mirerani. Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewataka wamiliki wa migodi ya
madini ya Tanzanite kuiga kampuni ya TanzaniteOne kwa kusaidia miradi ya
jamii na kuachana na mtindo wa kuchuma na kuondoka bila kuchangia
chochote.
Mnyeti
aliyasema hayo jana wakati akizindua madarasa matano ya shule ya msingi
Songambele Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, yaliyojengwa na
kampuni ya TanzaniteOne.
Alisema
wamiliki wengi wa madini ya Tanzanite huwa wanachimba na wakipata
wanakwenda kuwekeza kwenye mikoa ya jirani ya Arusha na Kilimanjaro.
"Wamiliki
wa migodi mnapaswa kubadilika igeni mfano wa kampuni ya TanzaniteOne
ambayo inasaidia jamii kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo," alisema
Mnyeti.
Alisema jamii ya
eneo hilo ingefurahi kuona faida ya uwepo wa madini hayo kwa wamiliki
hao kurudisha kidogo walichokipata kwa kuchangia maendeleo.
Mwalimu
mkuu wa shule hiyo, Mwanahamisi Musa alisema TanzaniteOne imejenga
madarasa hayo baada ya kubaini baadhi ya wanafunzi wanasoma nje sababu
ya mafuriko yaliyotokea Machi mwaka 2013 na kuharibu vyumba saba.
Mwalimu Musa alisema mafuriko hayo pia yaliharibu ofisi ya walimu, choo cha wanafunzi na nyumba mbili za walimu.
"Vyumba
saba vya madarasa vilizuiwa na mhandisi wa wilaya hiyo visitumike
kutokana na nyufa zilizohatarisha usalama wa wanafunzi," alisema mwalimu
Musa.
Alisema kutokana
na uharibifu wa mafuriko hayo, shule hiyo ilibakiwa na vyumba vitano
pekee ambavyo walivitumia kufundishia wanafunzi 1,158.
Alisema
shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2002 ina wanafunzi 1,158 wavulana 602 na
wasichana 556 hivyo madarasa hayo yatapunguza msongamano.
Alisema
wanaishukuru kampuni ya TanzaniteOne kwa kukamilisha madarasa hayo ila
wanawaomba wamalizie vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na
kisima cha maji kama walivyoahidi.
Ofisa
mahusiano wa kampuni ya TanzaniteOne, Halfan Hayesh alisema atafikisha
salamu za pongezi zilizotolewa na mkuu huyo wa mkoa kwa viongozi wake.
Hayeshi
alisema pia atafikisha ombi la kutakiwa wamalizie vyumba viwili vya
madarasa, ofisi ya walimu na kisima cha maji kama walivyoahidi.
Post a Comment