WAKURUGENZI wawili wa Kampuni za Saha Limited na Lucky Shipping Co.Ltd,
wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na
mashitaka mawili ya uhujumu uchumi ikiwemo kupeperusha bendera ya
Tanzania bila kibali.
Washitakiwa hao ni Issa Haji au Salum (39) ambaye ni baharia na
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lucky Shipping pamoja na Abdullah Hanga (73)
mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kampuni ya Saha ambaye ni mkazi wa Mbezi
Beach.
Akisoma mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria
Nongwa, Wakili wa Serikali, Wankyo Saimon alidai washitakiwa
walijihusisha na mtandao wa uhalifu kinyume na aya 4(1) C, jedwali la
kwanza na kifungu cha 57(1) na 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu uchumi.
Saimon alidai kuwa Julai 19, mwaka jana na Januari 16, mwaka huu jijini
Dar es Salaam, walitoa ushauri, msaada na maelekezo katika kutenda kosa
la jinai la mtandao wa uhalifu ambalo ni kupeperusha bendera ya Tanzania
kwenye meli iitwayo Huihang 68 zamani ilijulikana kama Greko 02, bila
kuwa na hati ya usajili kutoka kwa msajili wa meli nchini kwa lengo la
kujipatia faida kutoka katika shughuli za uvuvi haramu.
Pia alidai kuwa Julai 19, mwaka jana na Januari 16, mwaka huu, katika
jiji la Dar es Salaam washitakiwa hao huku wakifahamu kuwa ni kosa
kisheria waliruhusu upeperushwaji wa bendera katika meli hiyo ya Huihang
68 au zamani ilijulikana kama Greko 02 bila kuwa na leseni kutoka kwa
msajili wa meli kwa lengo la kuifanya ionekane kuwa ya Tanzania wakati
sio kweli.
Hakimu Nongwa alisema washitakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Hata hivyo, Saimon alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo upo katika hatua
za mwisho kukamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya
kuieleza mahakama taarifa za upelelezi huo.
Wakili wa utetezi, Dismas Raphael aliiomba mahakama ijielekeze katika
Katiba ambayo inawatambua washitakiwa hao kama watuhumiwa na kwamba
iwatendee haki kwa kuwapatia dhamana.
Akijibu hoja hiyo, Saimon alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini
(DPP), amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa washitakiwa hao kwani
wakipewa dhamana wataingilia maslahi ya Taifa hivyo mahakama ijielekeze
katika suala hilo.
Pia alidai Ibara ya 59 (B) ibara ndogo ya 3 inaainisha mamlaka ya DPP
kuhusu masuala yote yanayolenga maslahi ya Taifa kama ilivyoainishwa
kwenye Katiba.
“Kama upande wa utetezi wanalenga kuipinga hati ya kuzuia dhamana
wanatakiwa wafuate taratibu nyingine katika mahakama za Kikatiba ambapo
watakapowasilisha maombi yao, sisi tutayajibu ndipo mahakama itatoa
maamuzi,” alidai Saimon.
Hakimu Nongwa alisema upande wa utetezi uwasilishe mapingamizi yao
kuhusu hati hiyo na upande wa mashitaka ujibu na kwamba mahakama hiyo
itatoa maamuzi kama hati hiyo ni sahihi au la.
Hata hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 22, mwaka huu kwa ajili
ya kutajwa na kwamba washitakiwa hao wamerudishwa rumande.
Home
»
HABARI ZA BIASHARA
»
KITAIFA
»
Matukio
» WALIOPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KWENYE MELI BILA KIBALI WAPANDISHWA KIZIMBANI
About Author
Journalist , Enterpreneur, Lecturer and Blogger. Email :ngoboleaa@gmail.com.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment