Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza
na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini
Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya kujitambulisha na
kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo
katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini.
Na Hamza Temba - Dodoma
.............................. .............................. ..
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla ameipongeza
Serikali ya Finland kwa ushirikiano na misaada mbalimbali ambayo imekuwa
ikiitoa kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi wa maliasili na
uendelezaji wa misitu nchini.
Dk.
Kigwangalla ametoa pongezi hizo leo Januari 16, 2018 kwa Balozi wa nchi
hiyo hapa nchini, Mhe. Peka Huka ambaye amemtembelea ofisini kwake
mjini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya
kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na maendeleo ya
misitu nchini.
“Napenda
kutoa pongezi zangu za dhati kwa Serikali ya Finland, mmekuwa
washirika wetu wakubwa wa maendeleo kwa muda mrefu ambao mmetusaidia
mambo mbalimbali ikiwemo kuendeleza misitu nchini, kuendeleza Chuo cha
Mafunzo ya Misitu Olmotonyi na hata mapitio ya Sera ya Taifa ya Misitu
ya mwaka 1998, ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kudumisha ushirikiano
huu”, alisema Dk. Kigwangalla.
Alimueleza
balozi huyo kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika
uhifadhi wa misitu nchini ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha na
teknolojia kwa ajili ya kuwezesha uhifadhi endelevu. Alisema changamoto
nyingine ni uvunaji haramu wa mazao ya misitu ambayo husababisha eneo la
hekta 372,000 za misitu kupotea kila mwaka.
Alisema
mbali na nguvu kubwa inayotumiwa na Serikali katika udhibiti wa uvunaji
holela wa mazao ya misitu Wizara yake kwa kushirikiana na taasisi
zilizoko chini yake inaendelea kuweka mikakati thabiti kwa kushirikiana
na mamlaka zingine za kiserikali kwa ajili ya kutafuta nishati mbadala
pamoja na kuanzisha mashamba kwa ajili ya uzalishaji wa miti ya mkaa kwa
njia endelevu.
Akizungumzia
umuhimu wa misitu nchini, Dk. Kigwangalla alisema takribani kila kitu
hapa nchini kinategemea uwepo wa misitu. Alisema zaidi ya asilimia 80 ya
chanzo cha nishati ya umeme nchini ni maji ambayo hutegemea uwepo wa
misitu, alitaja pia kilimo na ufugaji ambao pia hutegemea mvua na maji
ambayo hutegemea pia uwepo wa misitu.
Kutokana
na umuhimu huo, Dk. Kigwangalla amemuomba Balozi huyo kuhamasisha
wawekezaji wa Finland kuja kuwekeza Tanzania katika uzalishaji na
matumizi endelevu ya rasilimali za misitu nchini na kuahidi kuwapa
ushirikiano.
Kwa
upande wake Balozi Huka, alimueleza Dk. Kigwangalla kuwa nchi yake
imekua ikifadhili miradi mbali mbali ya uendelezaji wa misitu katika
maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo mikoa ya nyanda za juu kusini na
kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.
Alimueleza
Waziri Kigwangalla kuwa changamoto iliyopo ya uharibifu wa misitu
nchini inahitaji uwepo wa nishati mbadala ambayo mchakato wa upatikanaji
wake unatakiwa kushirikisha wadau na Mamlaka nyingine za Kiserikali
ikiwemo Wizara ya Nishati.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia)
akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini
kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya
kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano
baina ya nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza
na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini
Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya kujitambulisha na
kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo
katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia)
akimsikiliza Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake
mjini Dodoma leo.
Balozi Peka Huka akimsikiliza Waziri Kigwangalla katika kikao hicho.
Waziri Kigwangalla akifafanua jambo kwa Balozi Peka Huka (hayuko pichani) katika kikao hicho mapema leo mjini Dodoma.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akimuaga
Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka baada ya mazungumzo
ofisini kwake leo mjini Dodoma .
Post a Comment