Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza na
watumishi wa Pori la Akiba Mpanga Kipengele alipotembelea makao makuu ya
pori hilo jana katika Wilaya ya Wangin'ombe mkoani Njombe. Katikati ni
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania,
David Kanyata na Kaimu Meneja wa pori hilo, Stanslaus Odhiambo.
Na Hamza Temba, Mbarali - Mbeya
.............................. .............................. ...........................
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ametoa miezi mitatu kwa
uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA kukamilisha
malipo ya fidia ya shilingi milioni 771.6 kwa kaya 308 za Kitongoji cha
Machimbo ili ziweze kupisha eneo la hifadhi katika Pori la Akiba la
Mpanga Kipengele.
Naibu
Waziri Hasunga ametoa agizo hilo jana katika mkutano wa hadhara baada
kutembelea kitongoji hicho katika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wakati
wa ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kutatua migogoro kwenye maeneo ya
hifadhi mkoani humo.
“Kaimu
Mkurugenzi (TAWA) kama unavyoona wananchi hawa wapo tayari kupisha eneo
hili la hifadhi, wanachosubiri ni malipo yao ya fidia, naagiza mpaka
ifikapo mwezi Februari mwakani (2018) wawe wameshalipwa fidia zao, na
ikiwezekana hata ndani ya mwezi Januari wawe wameshalipwa,”alisema
Hasunga.
Awali
akiwasilisha taarifa ya pori hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
hiyo, David Kenyata alisema wakati pori hilo linaanzishwa mwaka 2002 kwa
Tangazo la Serikali Na. 483 wananchi wa kitongoji hicho na vitongoji
vingine walikuwa ndani ya eneo hilo la hifadhi.
Alisema
mazungumzo yalishafanywa kupitia vikao halali vya uongozi wa viijiji na
halmashauri ambapo wananchi hao waliridhia kulipwa fidia ili kuachia
maeneo hayo ya hifadhi.
Alisema
sababu kubwa ya kuanzishwa kwa pori hilo ni pamoja na kuhifadhi vyanzo
vya maji yanayotiririka kwenda mto Ruaha na kwenye mabwawa ya kidatu na
mtera yanayotumika kuzalisha umeme nchini.
Akizungumzia
malipo ya fidia kwa vijiji na vitongoji vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo
alisema kijiji kimoja kilishalipwa mwaka 2015 jumla ya shlingi milioni
500 na vijiji vilivyosalia vitalipwa kwa awamu ambapo kwa mwaka wa fedha
2017/2018 fedha zimetengwa kwa ajilia ya kulipa wananchi wa kitongaoji
cha Machimbo ambao tayari walishafanyiwa uthamini mwaka 2015.
Awali
akizungumza na watumishi wa Pori hilo katika ofisi zao zilizopo Wilaya
ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Naibu Waziri Hasunga aliwataka watumishi
hao kuongeza nguvu na ubunifu kwenye kuzuia mifugo isiiingie hifadhini
badala ya kusubiri iingie ndipo waikamate na kuitoza faini au
kuitaifisha.
“Nyie
ni watalaamu, tumieni mbinu na ubunifu wenu wote muhakikishe mnazuia
mifugo isiingie hifadhini, sitaki kusikia mmekamata au mmetaifisha
mifugo hifadhini, hiyo siyo sifa, sifa ni kuzuia isiingie kabisa, na
nitawapima kwa hilo,” alisema Hasunga.
Aidha
aliwataka watumishi hao kuimarisha uhifadhi shirikishi, kujiepusha na
vitendo vya rushwa, kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa
umma na kuongeza ubunifu utakaowezesha ongezeko la mapato ya Serikali.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri huyo aliwatembelea wananchi
wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji katika Skimu ya Igomelo
ambao awali waligomea zoezi la uwekwaji wa vigingi vya mpaka kwenye eneo
lao na Pori la Akiba la Mpanga Kipengele kwa hofu ya kupoteza maeneo
hayo.
Hata
hivyo baada ya kuwaelimisha kuwa lengo la zoezi hilo ni kuiwezesha
Serikali kufanya uamuzi wa mwisho wa kumaliza migogoro ya ardhi
iliyodumu kwa muda mrefu baina ya vijiji na maeneo ya hifadhi nchini
wananchi hao walielewa na kuahidi kushirikiana na mamlaka husika kukamilisha zoezi hilo kwa muda uliopangwa.
Kwa
upande wake Kaimu Meneja wa Pori hilo, Stanslaus Odhiambo alisema pori
hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uwepo wa vijiji na
vitongoji 13 ndani ya pori hilo, uchomaji moto maeneo ya hifadhi,
ukataji miti hovyo, ujangili na uhaba wa vitendea kazi.
Pori
la Akiba la Mpanga Kipengele lina ukubwa wa Kilometa za mraba 1574.25
katika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na Wilaya za Wanging’ombe na
Makete Mkoani Njombe.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (waliokaa mbele katikati)
akizungumza na watumishi wa Pori la Akiba Mpanga Kipengele
alipotembelea makao makuu ya pori hilo jana katika Wilaya ya Wangin'ombe
mkoani Njombe.
Baadhi ya watumishi wa Pori la Akiba Mpanga Kipengele wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (hayuko pichani).
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (wa pili kushoto)
akisalimiana na Kaimu Meneja wa Pori la Akiba la Mpanga Kipengele, Stanslaus Odhiambo muda mfupi baada ya kuwasili makao makuu ya pori hilo jana katika Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na wananchi
wa Kitongoji cha Machimbo wapatao kaya 308 katika Wilaya ya Mbarali
mkoani Mbeya jana ambapo aliiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania kuwalipa fidia ya shilingi milioni 771.6 kabla ya Februari,
2018 ili wapishe eneo la Hifadhi katika Pori la Akiba la Mpanga
Kipengele.
Baadhi
ya wananchi wa kitongoji cha Machimbo wapatao kaya 308 katika Wilaya ya
Mbarali mkoani Mbeya wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Japhet Hasunga ambaye aliwatembelea jana na kuagiza Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania iwalipe fidia ya shilingi milioni
771.6 kabla ya Februari, 2018 ili wapishe eneo la Hifadhi katika Pori la
Akiba la Mpanga Kipengele alipowatembelea.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na wananchi wanaojishughulisha
na kilimo cha umwagiliaji katika Skimu ya Igomelo, wilaya ya Mbarali
Mkoani Mbeya ambao waligomea zoezi la uwekwaji wa vigingi vya mpaka
kwenye eneo lao na Pori la Akiba la Mpanga Kipengele kwa hofu ya
kupoteza maeneo hayo. Baada ya kuwaelimisha wananchi hao walikubali
kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika ili kukamilisha zoezi hilo.
Post a Comment