Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
SAUTI
za kuku zinasikika hata ukiwa nje ya jengo dogo ndani ya Soko la Kisutu
jijini Dar es Salaam, lakini ghafla zinakoma na zinasikika nyingine.
Siyo
kwamba kuku hao wanahitaji chakula ama wanacheza, bali hapa ni
machinjio, na sauti zinapokoma ujue tayari zimekwishapigwa kisu na
zinaandaliwa kwa ajili ya kitoweo.
Nje ya jengo hilo unaweza kuwa umekuta akinamama wengi wakiwa wamelundikana huku wakiwa wamekalia ndoo zao.
Hawa nao wanasubiri huduma, wanataka kununua utumbo, miguu pamoja na vipapatio vya kuku hao wanaochinjwa ili wakafanye biashara.
Akinamama
hawa wanatoka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na hapa
Kisutu ndiko mahali pekee ambako wanaweza kupata bidhaa hiyo
wanayokwenda kuuza mitaani.
Bila
shaka baadhi yetu tumekutana ama tumewakuta akinamama wakiuza firigisi
na utumbo mitaani, basi amini kwamba asilimia kubwa wanapata bidhaa hiyo
katika eneo hili la Kisutu.
Ukiingia ndani ya jengo hilo usishangae ukasalimia usiitikiwe na watu wengi, japokuwa waliomo ni wengi.
Kabla hujajua usimame wapi, utasikia sauti ya mtu akikutaka radhi kwamba anaomba kupita ama anataka kuweka mzigo.
Naam.
Kila mtu hapa yuko ‘busy’ na kazi inakwenda mtindo mmoja, na hata
kutokukuitikia si kwamba wanafanya kiburi ama hawajakuona, la hasha. Kwa
sababu wanataka kuhakikisha kazi wanayoifanya inakuwa katika hali bora
hasa ikizingatiwa kwamba hicho ni chakula kwa afya ya binadamu.
Mazingira ya ndani yanaridhisha kutokana na usafi ambao unazingatiwa sana na wahusika licha ya changamoto za hapa na pale.
Hawa
ni wanaushirika wa Kisutu Poultry Farm Cooperative Society (KIPOCOSO),
ambao wamekuwepo katika soko hilo kwa zaidi ya miaka 28 na ndio
waanzilishi wa kuchinja kuku jijini Dar es Salaam.
Japokuwa
hivi sasa baadhi ya masoko yana machinjio ya kuku, lakini wengi
wanaohusika na uchinjaji wamejifunza ama wamewahi kufanya shughuli hizo
katika Soko la Kisutu.
Kuku walionyonyolewa, kuchunwa ngozi au kukatwakatwa wanaweza kukutoa udenda wangali wabichi na wamewekwa mafungu mafungu.
“Kila
fungu unaloliona hapo lina mwenyewe, hawachanganyani kabisa,” ndivyo
anavyoeleza Bw. Hamisi Malamla, Mwenyekiti wa KIPOCOSO.
Anaongeza:
“Kazi yetu hapa ni kuchinja, kuku wote wana wenyewe na kila mmoja hapa
ndani anakwenda hapo nje kwenye mabanda wanakonunua kuku na kutafuta
oda, akiipata anakuja kuchinja na kuwatengeneza.”
Bw.
Malamla anasema kwamba, asilimia kubwa ya kuku wanaoliwa jijini Dar es
Salaam wanachinjwa na kuandaliwa katika soko hilo, sehemu ambayo pia ni
maarufu kwa wauzaji wa kuku – wa nyama wa kisasa pamoja na wa kienyeji.
Ndani
ya jengo hilo lililowekwa terazo, kujengwa masinki bora pamoja na
majiko matatu makubwa yanayotumia gesi, takriban kuku 3,000 huchinjwa
kila siku.
Licha
ya kufanya shughuli zao kwa ufanisi, lakini unapozungumza na
wanaushirika hawa utagundua kwamba wana mawazo makubwa ya maendeleo
tofauti na unavyoweza kuwadhania.
“Malengo
yetu ni kujikita katika uwekezaji wa kilimo na mifugo, tunataka tuanze
kufuga wenyewe kuku (wa kisasa na kienyeji), kuuza kuku wenyewe,
kutotolesha vifaranga, kutengeneza vyakula vya kuku pamoja na kusambaza
madawa,” anasema Bw. Malamla.
Anasema
kwamba, ikiwa wataanza uwekezaji wa kufuga kuku itakuwa ni hatua kubwa
kwao kwani watakuwa na uhakika wa kuchinja na kuuza, na kwamba oda
wanazozipata kwa sasa zitakuwa ni nyongeza tu na ziada.
Malamla
anasema, kwa uzoefu walionao, ikiwa watajikita pia katika ufugaji
wanaweza kulisha wananchi wengi jijini Dar es Salaam na kwamba hata kuku
watakaowafuga wanaweza kuongezeka ubora tofauti na baadhi ya wanaouzwa
sokoni hapo ambao mara nyingi huwa hawana uzito mkubwa.
“Tukianza
ufugaji ni dhahiri tutaongeza ubora kulingana na mahitaji ya soko na
hatuwezi kubahatisha, kwa sababu hapa wakati mwingine kuku wanaadimika
na inapotokea hivyo maana yake tunakosa kazi ya kufanya,” anasema.
Anaongeza
kwamba, tangu uongozi wake ulipoingia madarakani mwezi Machi 2017
(miezi nane iliyopita) wamefanikiwa kujiwekea akiba ya kutosha ambayo
inawapa msukumo wa kuangalia fursa za uwekezaji ili kuongeza kipato
pamoja na kupanua wigo wa ajira.
Usajili
Mwenyekiti
wa Ushirika wa Wachinja Kuku Soko la Kisutu (KIPOCOSO), Bw. Hamisi
Malamla (kushoto) akiwa na Mjumbe wa Kamati ya Uongozi, Mzee Shaaban
Hassan Bogoma leo hii walipotembelewa na MaendeleoVijijini.
KIPOCOSO,
ambacho ni miongoni mwa vikundi nane vinavyounda Umoja wa
Wafanyabiashara Soko la Kisutu (UWASOKI), kilisajiliwa Juni 28, 1989
kama chama cha ushirika na kupewa hatia namba DSR-382.
Kikundi
hicho cha ushirika kina jumla ya wanachama 57 na kinaongozwa na Bw.
Malamla kama mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti ni Zuberi Luwono, Hassan Ally
Sozigwa (Katibu), na wajumbe ni Shaaban Hassan Bogoma, Ally Omari
Vullu, Suleiman Kitalambo na Juma Said Mwinyi.
Malamla
anasema kwamba, kwa utaratibu waliojiwekea, kila mwanachama kati ya hao
57 lazima kila siku achangie Shs. 4,000 ambapo Shs. 2,000 ni kwa ajili
ya gesi na Shs. 2,000 kama ada.
“Utaratibu
huu ni kila siku, hivyo kwa kukusanya Shs. 2,000 za ada kila siku tuna
uwezo wa kuingiza Shs. 114,000 kila siku na kwa maana hiyo kwa mwezi
tunaweza kuingiza wastani wa Shs. 3 milioni.
“Tunao
wasaidizi 30 wanaofanya shughuli za kuchinja pia humu ndani, lakini
hawa hawahesabiwi kama ilivyo kwa wanachama wenyewe, na mara nyingi
wasaidizi hawa huwa ni wale wanaowasaidia wanachama husika,” anaongeza.
Kwa
mujibu wa Malamla, hivi sasa wanayo akiba ya kuridhisha ingawa inaweza
isitoshe kuanzisha shughuli za ufugaji mkubwa ambazo zinahitaji fedha
nyingi zaidi.
“Hatujapiga
hesabu, lakini najua shughuli hizi zinahitaji fedha nyingi zaidi,
tunaamini kwa dhamira ya dhati tuliyonayo, ipo siku tutafanikiwa tu
katika mipango yetu,” anasema.
Mbali
ya akiba ya fedha benki, lakini ushirika huo unamiliki viwanja takriban
21 vyenye ‘Offer’ katika eneo la ekari 10 huko Mbutu, Kigamboni jijini
Dar es Salaam ambapo miongoni mwa viwanja hivyo ni eneo la ekari moja
ambalo wanataka waanzie ufugaji wa kuku na samaki.
Kaimu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika
Tanzania (TFC), Bw. Henry Mwatwinza Mwimbe, anasema kwamba, KIPOCOSO ni
miongoni mwa vyama vya ushirika vya msingi vilivyoonyesha mafanikio
makubwa katika kipindi kifupi.
“Kimeanzishwa
muda mrefu, lakini kimepitia katika uongozi mbovu ambao pengine haukuwa
na malengo, uongozi wa sasa tangu ulipoingia madarakani mwezi Machi 19,
2017 umeweza kufanya mambo makubwa sana kwa usimamizi wetu na bado
tunaendelea kuwasaidia maoni na mambo mbalimbali kuhakikisha kwamba
wanapiga hatua,” anasema Mwimbe.
Mwimbe
anasema kwamba, kwa hatua waliyofikia, KIPOCOSO wanaweza kabisa
kukopesheka kwani licha ya akiba waliyonayo, bado wanayo rasilimali
ardhi na wana malengo ya kuwekeza katika kilimo na ufugaji.
Changamoto
Pamoja
na mafanikio waliyonayo, lakini wajasiriamali hao wanasema kwamba,
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan masuala ya usafi wa
mazingira.
Mzee
Shaaban Bogoma anasema kwamba, mifumo ya majitaka iliyowekwa na
Halmashauri ya Jiji (mifumo ya DSSD) haikidhi mahitaji na wakati
mwingine mitaro hufurika na kuchafua mazingira.
“Majengo
ya jirani hapa yameweka mifumo ya nje ya kumwaga maji, sasa mvua
ikinyesha maji yote yanaingia kwenye mfumo wetu na kwa vile wakati
mwingine unakuwa umeziba, basi maji hufurika na kuleta kero kubwa ndani
ya soko,” anasema Mzee Bogoma.
Kwa
upande wake, Malamla anasema kwamba, bila DSSD kurekebisha mifumo ya
majitaka, hali itaendelea kuwa tete na kuhatarisha afya za
wafanyabiashara na walaji.
“Majengo
mengine mara nyingi hutiririsha maji machafu kwa muda mrefu bila
watendaji wa halmashauri kufuatilia, lakini ikitokea kwamba mfumo wetu,
ambao ni mdogo na unazidiwa, ukatiririsha maji yenye damu kutokana na
mitaro kuziba, hapa huwa ni mshike mshike,” anasema.
Amezitaka
mamlaka husika kuhakikisha zinawajibika kwa nafasi zao ili kuweka
mazingira bora katika soko hilo kwa kulinda afya za walaji na
wafanyabiashara kwa ujumla, kwani huduma yao ni muhimu kwa afya ya
binadamu na usafi ndiyo kipaumbele cha kwanza.
Post a Comment