JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
TAARIFA KWA UMMA
Serikali kupitia Wizara ya
Fedha na Mipango inaendelea na juhudi za kusimamia, kudhibiti na kurahisisha
upatikanaji wa taarifa mbalimbali za kifedha ikiwemo mishahara ya watumishi na
wastaafu wa Umma. Aidha, Mifuko ya Hifadhi za Jamii, Mashirika ya Bima,
Mabenki, Taasisi za Fedha, Saccos na wadau wengine wameendelea kufanikisha
utoaji huduma mbalimbali kwa watumishi na wastaafu wa Umma kwa kutumia taarifa
za mishahara zikiwa kwenye nakala ngumu. Hata hivyo, bado kuna changamoto
mbalimbali katika upatikanaji wa taarifa hizo ikiwemo kuongezeka kwa gharama za
uchapishaji na usambazaji wa nakala ngumu nchi nzima, usumbufu na gharama kubwa
kwa watumishi na wastaafu kuzitafuta taarifa hizo Hazina na wakati mwingine
kughushiwa. Kutokana na changamoto hizo, Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa
mfumo wa kielektroniki wa utoaji wa hati za malipo ya mishahara ya watumishi wa
Umma unaojulikana kama “Government Salary Slip Self Service”. Mfumo huu
unatumia taarifa sahihi zilizopo kwenye mfumo shirikishi wa taarifa za
Kiutumishi na Mishahara (Human Capital Management Information System) wa
Serikali ujulikanao kama “Lawson”. Utaratibu wa kujisajili na kutumia huduma
hii kwa watumishi wa Umma unatolewa na waajiri wao.
Walengwa
na watumiaji wa mfumo huu ni watumishi wa Umma, Wastaafu, Mifuko ya Hifadhi za
Jamii, Mashirika ya Bima, Taasisi za Fedha (Mabenki, Saccos) na wadau wengine
wanaotoa huduma kwa Watumishi wa Umma na
wastaafu kwa kutumia hati za malipo ya mishahara (Salary Slip) ikiwa kwenye
nakala ngumu.
Wizara
inapenda kuzitangazia Taasisi kuwa, huduma hiyo kwa sasa inapatikana kwa njia
ya kielektroniki kwa kutumia internet kwa masharti ya kusajiliwa kwanza ili
ziweze kuondokana na matumizi ya nakala hizo ngumu kwa kutumia namba maalum ya mshahara wa mtumishi kwa mwezi husika (salary
slip token) inayotolewa na mwajiri wake.
Sifa
za kusajiliwa kwa taasisi ni kutuma maombi yanayoambatana na namba za makato
(Deduction Codes) za taasisi husika pamoja na orodha ya watumiaji wa mfumo
wakiwa na taarifa zifuatazo; Namba ya mtumishi (Employee ID), Majina yake
matatu, namba ya simu, anuani pepe, namba ya utambulisho iliyoko kwenye
kitambulisho chake cha Taifa au namba iliyoko kwenye kitambulisho cha Mpiga Kura
au namba ya hati ya kusafiria.
Taasisi zinazotaka kujiunga
na mfumo huu ziwasilishe Maombi kwa Katibu
Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Barabara ya Jakaya Kikwete, Jengo
la ‘Treasury Square’ S.L.P 2802 DODOMA.
Taarifa hii inapatikana pia katika Tovuti ya Wizara
(www.mof.go.tz)
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Fedha na Mipango.
Post a Comment