Wazee wa baraza wameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa
mwigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu amehusika
kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Wakitoa maoni yao jana baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili,
wazee hao walieleza kuwa Lulu ndiye aliyesababisha kifo cha mpenzi wake
huyo wakati wa ugomvi baina yao usiku wa Aprili 7, 2012.
Wakizungumza mmoja baada ya mwingine, wazee Omary Panzi, Sarah Lugoma na
Rajabu Mlawa, walihusisha tukio la Kanumba kujibamiza kichwa ukutani na
kusukumwa na mshtakiwa.
“Kutokana na sababu na uainishi wa kesi (ushahidi) wa pande zote, mimi
kwa upande wangu nimeridhika kuwa Elizabeth (Lulu) ameua bila
kukusudia,” alisema mzee Mlawa na kuongeza: “Katika ugomvi, inawezekana
hekaheka za kujinusuru, alitumia nguvu kumsukuma Kanumba na kuanguka
ukutani. Hivyo, kwa maoni yangu kosa la kuua bila kukusudia kwa
Elizabeth limethibitika.”
Akitoa maoni yake, Sarah Lugoma alisema Kanumba alifariki dunia kutokana
na ugomvi baina yake na mpenzi wake (Lulu) kwa kuwa ndani kulikuwa
giza, Kanumba aliteleza wakati wa ugomvi huo akaanguka.
“Hivyo mshtakiwa aliua bila kukusudia,” alisisitiza Lugoma wakati akihitimisha maoni yake.
Mzee mwingine, Panzi alisema Kanumba aliteleza na kuanguka wakati wa
ugomvi huo, mshtakiwa ndiye aliyehusika na kifo chake kwa kuua bila
kukusudia.
Hata hivyo, maoni ya wazee hao wa baraza siyo hukumu halisi ya Mahakama
bali yanayotokana na mtazamo wao tu katika hali ya kawaida nje ya sheria
kwa namna walivyousikiliza ushahidi wa pande zote.
Hivyo, kumtia hatiani mshtakiwa huyo hakumaanishi kuwa tayari ana hatia
kwa kuwa maoni hayo hayamfungi jaji katika hukumu yake ambaye huongozwa
na sheria husika.
Kwa hiyo, hatima ya msanii huyo kama ana hatia au la itabainishwa na
Mahakama Novemba 13 wakati Jaji Sam Rumanyika anayesikiliza kesi hiyo
atakapotoa hukumu.
Jaji Rumanyika aliwakumbusha wazee hao muhtasari wa ushahidi uliotolewa na pande zote kabla ya kutoa maoni yao.
Jaji Rumanyika akieleza kwa ufupi kilichozungumzwa na kila shahidi wa
pande zote, alitoa mwongozo kwa wazee hao pamoja na mambo mengine, kutoa
maoni yao bila kuongozwa na huruma wala kuogopa chochote.
“Mnalo jukumu la kutoa maoni yenu bila kuongozwa na huruma wala vitisho.
Mnatakiwa kutoa maoni yenu kwa mujibu wa ushahidi mliousikia,” alisema
Jaji Rumanyika.
Aliwaeleza kuwa kama walivyosikia ushahidi wa upande wa mashtaka kuwa
umejikita kwenye ushahidi wa kimazingira, mshtakiwa ndiye aliyekuwa mtu
wa mwisho kuwa na Kanumba.
Alisema ushahidi wa kimazingira lazima uwe ni vipande ambavyo ni
mnyororo (muunganiko) unaomhusisha mshtakiwa kuwa ndiye ametenda kosa.
“Kama mkiona kuwa mshtakiwa ametoa maelezo ya kutosheleza basi mnaweza
kusema hana hatia, lakini kama mna maoni tofauti pia mtaniambia,”
alisema Jaji Rumanyika na kuongeza:
“Mkiona kuwa kifo hicho kilitokana na ugomvi, basi shtaka lake huwa ni
la kuua bila kukusudia, mkishawishika kwa vyovyote na kwa namna yoyote
ile mshtakiwa hakuhusika na kifo hiki msisite pia kunipa maoni yenu.”
About Author
Journalist , Enterpreneur, Lecturer and Blogger. Email :ngoboleaa@gmail.com.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment