Habari kutoka ndani ya chama hicho katika wilaya za Moshi, Siha na Hai zinadai kuwa vivuli vya wanasiasa hao ndiyo kiini cha kufutwa kwa uchaguzi wa mwenyekiti katika wilaya hizo.
Wiki iliyopita, chama hicho kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alisema mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), umefuta uchaguzi katika wilaya nne. Mbali ya wilaya hizo tatu za Mkoa wa Kilimanjaro, nyingine ni Makete ya Iringa.
Alisema sababu ya kufuta matokeo hayo ni kubainika kwamba wagombea waliojitokeza hawakuwa na sifa pamoja na kubainika kuwepo na viashiria hatarishi kwa chama hicho kikongwe nchini.
Kutokana na uamuzi huo, Polepole alisema wilaya hizo zitaanza upya mchakato wa uchaguzi katika ngazi hiyo. Taarifa zilizopatikana jana kutoka Moshi Mjini zimeeleza kuwa tayari makada kumi na moja walikuwa wameshachukua fomu.
Taarifa zilizovuja kutoka ndani ya chama hicho katika wilaya za Hai, Moshi na Siha, zinadai kuwa mojawapo ya ‘viashiria hatari’ ni uwepo wafuasi wa Lowassa na Ndesamburo waliojitokeza kuwania nafasi hizo.
Wagombea katika wilaya ya Moshi ni Christopher Lyimo, Alhaji Omar Shamba, Consolata Lyimo na Elizabeth Minde ambaye ni mwenyekiti aliyemaliza muda wake na anayetetea nafasi hiyo.
Habari hizo zimedai kuwa kikundi kimoja cha makada wa CCM, kilichotwaa majukumu ya maofisa usalama wa chama, kinadaiwa kumwaga sumu kuwa mmoja wa wagombea alikuwa kwenye payroll ya Ndesamburo.
Hayati Ndesamburo alikuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa vipindi vitatu (2000-2015) alipoamua kustaafu mwenyewe. Alifariki dunia ghafla mapema mwaka huu.
“Hicho kikundi kinaoongozwa na kada mmoja (jina linahifadhiwa) kinajifanya usalama na kusema, (anamtaja mgombea) alikuwa kwenye payroll ya Ndesamburo ambaye ni marehemu,”
“Hivi wewe unavyoona ana shida gani mpaka awe analipwa na Ndesamburo wakati akiwa hai? Ni siasa za kuchafuana na hicho kimetengenezwa na huyo kada na kundi lake,” alidai kada mwingine wa CCM.
Mbali na mgombea huyo, lakini mgombea mwingine kati ya hao wanne anatajwa kuwa “haaminiki”, lakini haikuelezwa sababu za kuwajumuisha wagombea wote hadi uchaguzi wao kufutwa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Moshi Mjini, Priscus Tarimo alipoulizwa kuhusu uamuzi huo wa Nec alisema umekuwa ni changamoto kwao kwa sababu walishajiandaa kwa uchaguzi.
“Ni uamuzi wa vikao vya juu kutokana ni taarifa za kiusalama kwa hiyo sisi hatuna budi kuupokea na leo (jana) wanachama wetu wameanza kuchukua fomu upya. Tunaenda vizuri,” alisema Tarimo.
Tarimo alipoulizwa iwapo waliogombea awali na kuonekana baadhi yao hawana sifa na wana viashiria hatarishi wataruhusiwa kugombea tena, alisema wanaruhusiwa kwa sababu hawakuzuiwa.
Minde aliyemaliza muda wake, ambaye ni wakili kwa taaluma alipoulizwa jana kuhusu hatima yake alisema yuko nje ya Moshi lakini atarejea leo na atachukua tena fomu kuwania nafasi hiyo.
Mbali na wilaya ya Moshi, taarifa kutoka wilaya za Hai na Siha zinadai kiini cha kufutwa kwa uchaguzi wao, ni baadhi ya wanaowania kutajwa kumuunga mkono Lowassa 2015.
Habari hizo zimedai kuwa baadhi ya wagombea ambao ndiyo wenye nguvu na wanaoonekana watashinda uchaguzi huo, wanatajwa kuwa katika mtandao wa Lowassa wakati akiwania urais ndani ya CCM.
Mara baada tu ya Rais John Magufuli kuingia madarakani, alifanya mkutano wake wa kwanza ofisi ndogo ya CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam na kulalamikia uwepo wa makada wasaliti.
Aidha, tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015, chama hicho kimekuwa kikitekeleza mkakati wake wa kujiimarisha na kuwaondoa makada waliokisaliti katika kinyang’anyiro hicho kilichokuwa na ushindani mkali.
Ushindani huo ulikuwa baina ya Dk Magufuli na Lowassa ambaye licha ya kuondoka CCM na kugombea kwa tiketi ya Ukawa, bado alikuwa na kundi kubwa linalomuunga mkono ndani ya CCM.
Post a Comment