Ujerumani
imeipatia Tanzania kiasi cha Euro milioni 198.5 sawa na Sh. Bilioni 520.86 zilizotumika kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo
ya Maliasili na Mazingira, Afya, Maji, Nishati, Udhibiti wa Fedha za Umma (Good
Financial Governance) na Kusaidia Huduma za Wakimbizi katika mkoa wa Kigoma,
katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Hayo
yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban wakati wa tukio la Tanzania na Ujerumani kusaini
kumbukumbu za Mkutano wa Mashauriano ya Kimaendeleo (Bilateral Development
Consultations) ambapo Ujerumani imeonesha nia ya kuendelea kuisaidia Tanzania
katika Sekta hizo kuanzia mwaka 2018 hadi 2021.
Kumbukumbu za
Mashauriano hayo zimesainiwa na Naibu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Naibu Mkuu wa Idara ya Kanda ya Afrika Mashariki katika Wizara
ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani Bw. Georg Rademacher kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani.
Mkutano
huo ni maandalizi ya mkutano wa Majadiliano ya Kimaendeleo (Bilateral
Negotiations) kati ya nchi hizi mbili unaotarajiwa kufanyika mwaka 2018 ambapo
Serikali ya Ujerumani itatangaza kiasi cha fedha watakazotoa kama msaada kwa
ajili ya kufadhili Sekta zilizoainishwa katika kumbukumbu zilizosainiwa.
“ Tunaishukuru
Ujerumani kwa kuwa miongoni mwa washirika wa muda mrefu wanaotoa misaada
mikubwa ya kimaendeleo kwa Tanzania na sisi tunaahidi kuendeleza ushirikiano
huo kwa faida ya pande zote mbili” alisema Bi. Amina Khamis Shaaban.
Kwa upande wake Bw. Georg Rademacher kwa niaba ya Serikali ya
Ujerumani amesema kwamba Tanzania imekuwa na sifa njema nchini Ujerumani hasa
kwa sababu ya amani iliyopo, jinsi ambavyo imehifadhi maliasili zake na
kuifanya kuwa nchi yenye vivutio vya kipekee vya utalii.
Bwana Rademacher aliongeza kwamba kwa sasa nchi ya
Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika kupambana na ubadhirifu wa mali za
Umma na kwamba Ujerumani itaendelea kuisaidia Tanzania ili kuweza kuleta
maendeleo kwa watu wake na kuondoa umaskini.
Imetolewa
na;
Benny
Mwaipaja
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Fedha na Mipango
Post a Comment