Jalada la kitabu cha ‘MIFUPA YA ALBINO’.
Mwandishi Daniel Mbega, akiwa ameshikilia Karunguyeye waliokaushwa nyumbani kwa mganga wa jadi.
MWANDISHI
wa habari mwandamizi nchini, Daniel Mbega, amekamilisha kuandika kitabu
kinachofichua siri zilizo nyuma ya pazia kuhusiana na mauaji ya
vikongwe na albino nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.
Mwandishi
huyo, ambaye alifanya utafiti kwa kipindi cha miezi nane mfululizo
katika mikoa 10 ya Kanda ya Maziwa Makuu, amesema kitabu hiyo alichokipa
jina la ‘MIFUPA YA ALBINO’ kinatarajiwa kuwaingia kiwandani wakati
wowote na kwa sasa anatafuta msaada wa fedha za kuchapia.
“Nimekamilisha,
lakini nimekwama kidogo kuhusu fedha za uchapaji na kama kuna taasisi
yoyote au mtu anayeweza kunisaidia nitashukuru sana,” amesema
mwanahabari huyo.
“Yeyote
mwenye nia njema na jamii ya Watanzania na anaguswa kusaidia uchapaji
wa kitabu hiki, ninaomba awasiliane nami kwa namba hii 0656-331974,
kwani naamini kitabu hiki kitakuwa msaada pia wa kiroho baada ya kujua
mambo yanayofanywa hata na baadhi ya viongozi wa dini wanaotumia
ushirikina,” aliongeza.
Bw.
Mbega amesema kwamba, katika utafiti wake huo alifanikiwa kukutana na
waganga wa jadi, wachawi na matapeli katika mikoa ya Shinyanga, Geita,
Simiyu, Mwanza, Kagera, Mara, Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa, ambako
alikaa kwa miezi miwili akifanya uchunguzi.
Aidha,
amesema kwamba, katika uchunguzi wake huo alishiriki pia kikamilifu
katika misako mbalimbali ya wahalifu walioshiriki kwenye matukio hayo na
kushuhudia namna vyombo vya ulinzi na usalama vinavyotenda kazi.
Kunusurika
kifo kwa ajali ama kuzingirwa na baadhi ya wananchi ni moja ya hatari
alizokumbana nazo wakati wa uchunguzi wake, huku akisafiri umbali wa
zaidi ya kilometa 40,000 katika kipindi hicho.
“Wakati
mwingine nilikosa usingizi hata kwa siku tano mfululizo, nililazimika
kusafiri mchana na usiku katika mazingira mengi hatarishi nikikusanya
habari,” alisema.
Akaongeza:
“Haikuwa kazi rahisi kuweza kufanya mahojiano na waganga wa jadi,
achilia mbali wachawi ambao baadhi yao waliamua kujiweka wazi na kueleza
mambo yanayotendeka katika ulimwengu wa giza na jinsi yanavyohusiana na
mauaji ya wenye ualbino.”
Alisema
katika uchunguzi huo alikumbana na mambo mengi ya ajabu ikiwa ni pamoja
na kushika matunguli, pembe zinazofoka damu, damu na maiti, mifupa
inayodhaniwa kuwa ya binadamu na mambo mengine kadha wa kadha.
Aidha,
alisema kwamba, alizungumza pia na wanamichezo, baadhi ya viongozi wa
dini ambao nao wanatumia nguvu za giza ambapo waganga walieleza jinsi
nao wanavyoshiriki katika matukio hayo ya mauaji ya wenye ualbino.
“Ni
mtandao mpana sana, siyo Tanzania tu, bali hata katika nchi jirani za
Kenya, Malawi, Burundi, Msumbiji, Afrika Kusini na Swaziland… naamini
kkitabu hiki kitaiamsha jamii na kubadilisha mitazamo ya watu mara
watakapojifunza yale niliyoyakusanya kutoka kwa vinywa vya wahusika
wenyewe,” amesema na kusisitiza kwamba amepanga kitabu hicho kiwwe
mtaani mwishoni mwa mwezi Septemba ikiwa atapata msaada wa kufanikisha
uchapaji.
Mganga
wa jadi akimpigia ramli mwandishi wa kitabu hiki (hayuko pichani) baada
ya kutoa Shs. 2,000 akitaka amwangalizie kwanini 'mkewe' (askari mmoja
wa kike aliyekwenda naye wakiwa kikazi) alikuwa hazai. Mganga alisema
mwanamke huyo alikuwa 'amelogwa' na mwanamke aliyetaka kuolewa na
mwandishi halafu yeye akamkataa, ambapo kiuhalisia hakuwepo mwanamke wa
aina hiyo na hata huyo aliyekwenda naye walikutana kikazi na hawakuwa
wakifahamiana kabisa.
Mtoto Baraka Cosmas akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya baada ya kukatwa kitanga cha mkono Machi 7, 2015.
Mwandishi
Daniel Mbega (mwenye fulana nyekundu na kofia ya sweta) akiwa sambamba
na wanausalama katika nyumba ambamo Baraka Cosmas alikatwa kitanga cha
mkono Machi 7, 2015.
Mtuhumiwa
Sajenti Kalinga Malonji akiwa chini ya ulinzi baada ya kukishusha
kiganja cha Baraka Cosmas kwenye mti nyumbani kwake kijijini Hanseketwa,
Mbozi siku ya Jumapili, Aprili 26, 2015. Sajenti tayari amehukumiwa
miaka nane jela na wenzake wamehukumiwa vifungo vya hadi miaka 20 jela.
Mwandishi Daniel Mbega, akiwa kwa mganga huko Kachwamba, wilayani Chato wakati akifanya uchunguzi wa mauaji ya albino.
Post a Comment