PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Tanzania Yatajwa Kwenye Orodha ya Nchi Zenye Mishahara Mikubwa Afrika
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
  Shirika la Numbeo limetoa orodha ya nchi kumi zenye mishahara mikubwa zaidi barani Afrika. Hili ni shirika kubwa zaidi ...


Shirika la Numbeo limetoa orodha ya nchi kumi zenye mishahara mikubwa zaidi barani Afrika. Hili ni shirika kubwa zaidi duniani la ukusanyaji wa taarifa za majiji na nchi. Shirika hili linatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu hali za maisha duniani ikiwemo gharama za maisha, upatikanaji wa nyumba za kupanga, huduma za afya, foleni za barabarani, uhalifu na kiwango cha uchafuzi wa mazingira.
Zifuatazo ni nchi kumi za kiafrika zenye viwango vya juu zaidi vya mshahara:

1. Libya
Libya ndiyo nchi inayoongoza barani Afrika kwa kuwa na viwango vikubwa vya mishahara. Nchi hii yenye utajiri wa mafuta imejulikana kwa zaidi ya miongo minne ya utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hayati Muammar Gaddafi na machafuko yaliyofata baada ya kifo chake. Na pamoja kwa machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo mpaka sasa yanayosababisha hali ya usalama kuwa tete, kiwango cha kawaida cha mshahara kwa mwezi baada ya makato ya kodi ni shilingi milioni tatu na laki nane (3,800,000)

Ingawa machafuko nchini Libya yamekuwa ni kikwazo kikubwa barani Afrika, kiwango cha hifadhi ya mafuta kwenye nchi hiyo kinachokadiriwa kuwa mapipa bilioni 48 kunaifanya nchi hiyo sio tu kuwa moja ya nchi kumi zenye utajiri mkubwa zaidi wa mafuta duniani lakini pia Serikali yake inawafurahisha wananchi kwa kuwapa viwango vya juu vya mishahara pamoja na kufanya gharama za maisha kuwa chini.

2. Zambia
Jambo kubwa zaidi litakalokufanya uhamie kwenye nchi hii isiyo na bahari ni idadi kubwa ya wanyamapori. Ina mbuga na hifadhi nyingi sana, jambo linaloweza kuwa la kuvutia sana kama moja ya vitu unavyopendelea ni kufanya safari za mbugani. Kiwango cha kawaida cha mshahara kwa mwezi nchini Zambia ni shilingi milioni tatu na laki tatu (3,300,000), na kwa hakika huu ni mshahara mkubwa kwa yeyote yule. Gharama za kodi za nyumba na maisha kwa ujumla nchini Zambia zipo chini. Pamoja na viwango vikubwa kiasi hiki, Zambia kwa sasa inapitia katika mgogoro wa kisiasa na mifumo yake ya kiuchumi na kisheria bado inafata mfumo wa uendeshaji wa kikoloni.

3. Afrika Kusini
Mwisho wa siku kila mmoja anataka kazi yenye mshahara mzuri. Nchini Afrika Kusini, kazi zinazotokana na taaluma za Sheria, Umeneja wa mifumo ya kompyuta na teknolojia, waongoza ndege, udhibiti wa mafuta ya petroli, uhandisi wa majengo na uhandisi wa programu ni baadhi ya ajira zenye mishahara mizuri zaidi nchini humo. Kiwango cha kawaida cha mshahara nchini humo ni shilingi milioni mbili na laki sita (2,600,000+), ingawa wazungu bado mpaka sasa wanaishi maisha mazuri zaidi.

4. Namibia
Uchumi wa Namibia unaendeshwa na sekta ya madini – kuchimba, kusafisha na kusafirisha kwenda nje ya nchi. Sekta ya madini inachangia asilimia 11.5 ya pato la Taifa lakini inaiingizia nchi hiyo zaidi ya asilimia 50 ya fedha za kigeni.

Pia, Namibia ni moja ya nchi tano zinazozalisha madini ya uranium kwa wingi zaidi na pia wana utajiri mkubwa sana wa madini ya almasi. Ingawa uchumi wa nchi hiyo unaathiriwa sana na kupanda na kushuka kwa soko la dunia pamoja na ukame unaoikumba mara kwa mara, mshahara wa kawaida kwa wafanyakazi nchini humo ni shilingi milioni moja na laki sita (1,600,000) kwa mwezi.

5. Mauritius
Nchi hii ambacho ni kisiwa kilichopo nje kidogo ya pwani ya Kusini-Mashariki mwa Afrika kina historia ndefu ya kuwa na utulivu wa kisiasa, utawala bora pamoja na uwajibikaji wa uwazi wa Serikali yake. Ni moja ya nchi za Afrika zenye uchumi mzuri zaidi ikiwa na idadi ya watu milioni 1.3. Mshahara wa kawaida nchini Mauritius ni shilingi milioni moja na laki tano (1,500,000) kwa mwezi.

6. Tanzania
Hii ni nchi ya sita kwa nchi za bara la Afrika zenye viwango vya juu vya mshahara ambapo mshahara wa kawaida kwa wafanyakazi unakadiriwa kuwa ni shilingi laki tisa (900,000). Zaidi ya nusu ya wafanyakazi nchini Tanzania wapo kwenye sekta ya kilimo kama njia kuu ya kuwasingizia kipato. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Tanzania imeweza kuwa na uchumi imara na unaokua kwa asilimia saba kila mwaka katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Kiwango cha umaskini kimeendelea kupungua na vita dhidi ya Rushwa inayoongozwa na Rais John Magufuli inabaki kuwa msingi imara wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

7. Morocco
Tangu mwezi Oktoba mwaka 2016 nchi ya Morocco imekuwa kwenye mgogoro mkubwa sana wa kisiasa. Kwa sasa, nchi hiyo ina muunganiko mkubwa wa vyama vya siasa unaojumuisha vyama sita vya siasa nchini humo. Kilimo bado kinachangia asilimia 15 ya pato la Taifa. Pamoja na nchi hiyo kukumbwa na ukame mkubwa mwaka 2016, bado waliweza kuweka rekodi ya mavuno mengi zaidi ya nafaka. Katika nchi ya Morocco, mshahara wa kawaida kwa wafanyakazi ni shilingi laki tisa (900,000).

8. Zimbabwe
Mshahara wa kawaida kwa wafanyakazi nchini Zimbabwe ni shilingi laki nane (800,000). Nchi hii inayoongozwa na Rais Robert Mugabe tangu kupata kwa uhuru wake inatabiriwa kuwa itaweza kuwa na uchumi bora zaidi ya sasa na kupunguza umaskini iwapo itadhibiti hali ya kisiasa na kufikia makubaliano kuhusu kufanyika kwa siasa na sera za ushindani kwenye uwekezaji.

9. Ghana
Nchi hii imepiga hatua kubwa sana kwenye kujenga demokrasia imara. Ni nchi inayosifika kwa kuwa na mfumo huru wa Mahakama pamoja na uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza kwa wananchi na wanaharakati. Mshahara wa kawaida nchini Ghana ni shilingi laki saba (700,000) kwa mwezi. Uchumi wa nchi hii unategemea zaidi sekta ya mafuta, sekta nyingine zisizo za mafuta zina mchango mdogo kwenye uchumi wa nchi hiyo.

10. Algeria
Pamoja na bei ya mafuta kuporomoka kwenye soka la dunia, bado uchumi wa Algeria uliweza kukua kwa asilimia 3.8 mwaka 2016 ingawa pia yategemewa uchumi wake utashuka kati ya mwaka 2017 na 2019. Kiwango cha kawaida cha mshahara nchini Algeria baada ya makato ya kodi ni shilingi laki sita na elfu hamsini (650,000), kiwango ambacho ni kikubwa ukilinganisha na nchi nyingine nyingi za Afrika.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top