WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa
Jumanne Maghembe ameivunja bodi ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Tarafa ya
Idodi na Pawaga (Mbomipa) pamoja na kufuta mikataba ya kampuni mbili
zinazoendesha shughuli za uwindaji wa kitalii katika eneo hilo.
Mbomipa ni eneo la hifadhi ya jamii ya
wanyamapori linalopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Iringa mkoani
Iringa lenye wanyamapori wengi wanaoingia na kutoka katika hifadhi hiyo linaloundwa
na vijiji 21 vya tarafa hizo mbili.
Bodi iliyovunjwa inaundwa na Mwenyekiti Zabron
Luvinga na Steven Nyandongo, Alban Lutambi, Mawazo Malembeka na Denis Ngede
ambao ni wajumbe; na kampuni zilizofutiwa mikataba ni Kilombero North Safaris
Ltd na Mkwawa Hunting Safaris Ltd.
Wakati mmiliki wa kampuni ya Mkwawa
Hunting Safaris Ltd Ahamed Huwel alisema amepokea bila kinyongo chochote uamuzi
huo wa waziri alioutangaza juzi mbele ya wanajumuiya hiyo katika kijiji cha
Tungamalenga, mmiliki wa Kilombero North Safaris Ltd, Acram Aziz hakupatikana
kuzungumzia uamuzi huo.
Hatua ya Waziri Maghembe kuvunja bodi na
kufuta mikataba ya jumuiya hiyo na kampuni hizo imekuja kwa kuzingatia matokeo
ya timu ya wataalamu aliyoiunda hivikaribuni kuchunguza dosari na malalamiko ya
uendeshaji wa taasisi hiyo na kubaini mapungufu makubwa ya kisheria na kiutendaji.
“Kwanza Katiba inayotumiwa na jumuiya hii
inakinzana na sheria za wanyamapori, kanuni za uwindaji wa wanyamapori na
utalii wa kupiga picha; lakini pia bodi haiko pamoja, kila upande una mwekezaji
wake,” alisema.
Kwa mazingira hayo, waziri huyo alisema
katiba ya jumuiya hiyo inatakiwa kufumuliwa upya na baada ya hapo bodi mpya
uindwe katika mchakato alioagiza uwe umakamilika kabla ya Oktoba mwaka huu na
baada ya hapo shughuli ya kutafuta wawekezaji ianze upya.
Profesa Maghembe alisema eneo la jumuiya
hiyo lina utajiri mkubwa lakini akashangaa kuambiwa kwamba wana jumuiya hawana
wanachopata kutokana na uwekezaji unaofanywa eneo hilo, jumuiya haina uwezo wa
kulipa mishahara watumishi na walinzi wake na inashindwa kufanya shughuli zake
mbalimbali za kiofisi na matengenezo ya vifaa na gari lao yamekuwa yakifanywa
kwa kupitisha bakuri.
Awali katibu wa Mbomipa, Josephat
Kisanyagi alisema jumuiya imekuwa katika mtikisiko mkubwa wa kukosa mapato kutoka
kwa wawekezaji wake katika kipindi chaJulai 2016 hadi sasa.
“Kukosekana kwa mapato hayo kumesimamisha
shughuli muhimu za jumuiya hiyo huku viongozi na walinzi wanaofanya kazi ya
doria katika eneo hilo la Mbomipa wakikosa mishahara na stahiki zao,” alisema.
Akionekara kukerwa na kile kinachoendelea
ndani ya jumuiya hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema; “hakuna
kijiji hata kimoja kati ya vijiji 21 vinavyounda jumuiya hiyo kinachoweza
kusema kimenufaika na uwepo wa Mbomipa.”
Masenza alisema katika jumuiya hiyo
pamekuwepo na migongano isiyokwisha na utapeli uliokithiri ambao sehemu yake
kubwa ulifanywa na bodi zilizopita kana kwamba Mbomipa ilikuwa mali yao.
“Kwa maneno mepesi bodi ilipewa mamlaka
na madaraka makubwa juu ya Mbomipa kuliko inavyotakiwa, kumekuwa na kufukuzana
na kuchaguana mara kwa mara kwasababu baadhi ya watu waliokuwa wakipata uongozi
waliomba uongozi ili kukidhi maslai yao,” alisema.
Akiahidi kuyasimamia maamuzi hayo ya
waziri, Masenza aliwageukia pia baadhi ya wawekezaji katika eneo hilo la
Mbomipa akisema wamekuwa matapeli na hivyo kuifanya jumuiya hiyo ifike hapo
ilipo na kugeuka kuwa ombaomba.
Baada ya taarifa hiyo ya mkuu wa mkoa,
Profesa Maghembe aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
kufanya uchunguzi wa mapato na matumizi ya jumuiya hiyo ili hatua za kisheria
ziweze kuchukuliwa kwa watu watakaobainika waliitumia kujinufaisha.
Post a Comment