Mkurugenzi wa Namaingo, Biubwa Ibrahim
Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia Cedaba, akiwapa majukumu washiriki wa warsha hiyo.
MKURUGENZI
Mtendaji wa kampuni ya Namaingo Business Agency, Biubwa Ibrahim,
amewataka akinamama wanatekeleza mradi wa Green Voices Tanzania kuwa
wabunifu na kutokata tamaa katika shughuli wanazozifanya.
Akizungumza
wakati wa kufunga semina ya siku sita ya mafunzo yaliyowashirikisha
akinamama 15, Biubwa alisema kwamba, ubunifu, jitihada na kutokata tamaa
ndiyo silaha kubwa katika mafanikio, huku akiwahimiza watafute fedha
bila kuchoka.
“Lazima muwe wabunifu, halafu ni dhambi kubwa kukata tamaa bali mnatakiwa kuongeza jitihada katika mradi yenu,” aliwahimiza.
Aidha,
alisema kwamba, mafanikio yoyote hayawezi kuja kwa siku moja, hivyo
wanapaswa kuwa wavumilivu daima ili waweze kufanikiwa.
Akinamama
hao wa Green Voices wanatekeleza miradi mbalimbali ya kilimo
inayoendana na mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko
ya tabianchi, ambayo inadhaminiwa na taasisi ya Women for Africa
Foundation ya Hispania inayoongozwa na makamu wa rais mstaafu wa nchi
hiyo, Bi. Maria Tereza Fernandes de la Vega.
Biubwa
alisema, wajasiriamali wengi wanaposhindwa kuona faida ya shughuli
wanazozifanya huvunjika moyo mapema, lakini hilo lisiwe kikwazo kwao
kwani wanapaswa kukaa chini na kutafakari njia mpya ya kuendesha
biashara ama miradi yao.
“Inabidi
kujiuliza wewe mwenyewe kama hapo ulipo ndipo mahali sahihi, vinginevyo
usife moyo unapoona mambo hayaendi, bali angalia wapi ulipokosea na
ujipange upya halafu utaona matokeo yake,” alisema.
Akaongeza:
“Mimi nilianza na mtaji wa shilingi elfu nne tu, nimepitia changamoto
nyingi ikiwemo kudhulumiwa fedha, lakini katu sikukata tamaa nimeendelea
kupambana na mpaka sasa kupitia kampuni yangu nimeweza kusajili
wakulima 400,000 nchi nzima.”
Mwanahabari
mshiriki wa mradi wa Green Voices, Farida Hamisi, akipokea cheti kutoka
kwa Alicia Cedaba, Mratibu wa Green Voices kutoka Hispania. Katikati ni
muwezeshaji wa mafunzo hayo, Dkt. Olomi kutoka taasisi ya IMED.
Mradi
wa Green Voices unatekelezwa nchini Tanzania pekee, ambapo akinamama 10
kati ya 15 wanaendesha miradi mbalimbali ya kilimo, ufugaji wa nyuki,
ukaushaji wa mboga na matunda pamoja na utengenezaji wa majiko rafiki
katika jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Akinamama walioanzisha miradi hiyo – miradi na mikoa watokayo vikiwa kwenye mabano –ni Regina Kamuli (Mkuranga, Pwani – Majiko Banifu), Abiah Magembe (Kisarawe, Pwani – Usindikaji wa Muhogo na Mtama), Magdalena Bukuku (Kinondoni, Dar es Salaam – Kilimo cha Uyoga), Mariam Bigambo (Dakawa, Morogoro – Ufugaji wa Nyuki), na Esther Muffui (Morogoro – Ukaushaji wa Mboga na Matunda).
Wengine ni Farida Makame (Kilimanjaro – Majiko ya Umeme-Jua), Leocadia Vedastus (Ukerewe, Mwanza – Kilimo na Usindikaji wa Viazi Lishe), Monica Kagya (Kisarawe, Pwani – Ufugaji wa Nyuki), Dkt. Sophia Mlote (Kinyerezi, Dar es Salaam – Kilimo Hai cha Nyanya na Mbogamboga), na Evelyn Kahembe (Uvinza, Kigoma – Kilimo cha Matunda).
Mradi
huu wa Green Voices ambao mwaka huu uko katika awamu ya pili,
ulizinduliwa Julai mwaka 2016 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan.
Katika
awamu ya pili kinamama hawa wameendelea kuboresha kilimo cha mazao yao
kinachozingatia uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi katika
mikoa sita nchini.
“Pamoja
na kilimo, Mradi wa Green Voices umaeandaa mafunz mbalimbali ya
kuongeza ujuzi katika kilimo (climate smart agricultura) pamoja na
mafunzo ya jinsi ya kuandaa mazao au bidhaa wanazozalisha kupitia
kilimo,” alisema Mratibu wa Green Voices nchini Tanzania Secelela
Balisidya.
Katika
kutekekelza hilo, Green Voices kupitia mfadhili wake, Women for Africa
Foundation, walishiriki katika mafunzo mbalimbali ya Mbinu bora za
kuweka nembo na kufungasha bidhaa za vyakula, Viwango vya Ubora, na
Kanuni za uchakataji wa vyakula.
Mafunzo
hayo ambayo yalifanyika Julai 16 -22, 2017 yalizinduliwa na Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jaffo, ambaye
aliahidi kuwapa ushirikiano akina mama hao.
Utengenezaji bidhaa na ufungashaji
Kwa
siku sita baada ya kuzinduliwa kwa mafunzo, akinamama hao walijifunza
kuhusu Mchango wa kilimo katika mabadiliko ya tabianchi, Jinsi ya kuweka
mazingira bora ya umwagiliaji, Mikakati ya biashara katika ujasiriamali
wa kilimo, Utafutaji wa rasilimali na mkakati wa kuongeza mtaji,
Ukuzaji wa mtaji kupitia Vicoba, na Mbinu za uongozi.
Akinamama
hao walipata fursa ya kutembelea Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),
Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) ambapo ilikutana na
wajasiriamali walio katika hatua za juu za kufungasha na kuuza bidhaa
zao, ambapo walipata nafasi ya kubadilishana nao mawazo ili kuongeza
ujuzi wao.
Katika
mafunzo hayo, Linus Gedi ambaye ni mtaalam wa ubora wa chakula na
viwango kabla ya kuvipeleka sokoni, aliwaeleza washiriki kwamba ni
muhimu kufungasha na kuweka nembo kwani inasaidia kuhifadhi bidhaa na
inarahisisha mteja kutambua hiyo ni bidhaa ya aina gani, imetengenezwa
wapi na ina mchanganyiko gani.
Akinamama wanaotekeleza mradi wa Green Voices walipotembelea Ofisi za SIDO jijini Dar es Salaam.
“Ni
muhimu sana kuhakikisha chakula hakisababishi maradhi, lakini pia
kinafikia malengo ya walaji, hii huepusha sumu kwenye chakula,
mchanganyiko usiofaa, upotevu wa chakula, kupoteza bidhaa na kuepukana
na masuala ya kisheria,” alisema Linus.
Alisema uzalishaji wa chakula unatakiwa kuzingatia mbinu bora za uzalishaji na pamoja na usafi.
Aidha, aliwataka kuzingatia ubora, usafi na viwango vya chakula wanachozalisha ili kifikia malengo ya walaji.
Kwa
upande wake, Richard Jackson akielezea umhimu wa kunadi bidhaa, alisema
ni lazima kuwa na mikakati imara ya masoko ili kuhakikisha mjasiriamali
anapata faida.
Alisema ni vizuri kujua wateja maalum na wateja wa ujumla na nini hasa wanahitaji ikiwa ni pamoja na namna ya kuwafikia.
“Ni
lazima kujua kati ya wanaohitaji bidhaa zako, ni nani ambao siyo wateja
wako walengwa na kwa nini wateja wanunue bidhaa zako na siyo kwa
washindani wako? Lazima ujue tabia zao na ukubwa wa soko lako,” alisema Jackson.
Aidha,
alisema ni muhimu kuwajua wateja wako ili kuelewa mahitaji yao na kwa
nini wananunua bidhaa wanazonunua pamoja na kutambua mambo yanayowaudhi
ili usiwakwaze.
Kwa
upande wa uchangishaji fedha na kutafuta mitaji kwa biashara na kilimo,
Rais wa VICOBA Endelevu Tanzania, Devota Likokola, alieleza jinsi mfumo
wa VICOBA Endelevu unavyoweza kuwasaidia kinamama wa Green Voices
kupata mitaji ya kuendeleza miradi yao.
Post a Comment