Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma
Serikali
imewashauri wakazi wa Wilaya ya Malinyi mkoa wa Morogoro, kutumia njia
mbadala kupata huduma za kibenki ikiwemo kupitia simu za mkononi yaani
(simbanking) ya CRDB na Banking on the Wheel ya NMB iliyoko Mlimba kwa
kipindi hiki ambacho mchakato wa kufungua matawi rasmi ya benki
unaendelea.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la
Mbunge wa Malinyi Dkt. Hadji Hussein Mponda (CCM), aliyetaka kujua ni
lini huduma rasmi za kibenki zitaanzishwa katika wilaya ya Malinyi ama
kama kulikuwa na mpango wa taasisi za fedha kuanzisha huduma za matawi
ya benki yanayohamishika (mobile banking) wilayani humo.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, wilaya ya Malinyi ni moja ya
wilaya ambazo zinanufaika na mfumo wa utoaji huduma kupitia mawakala wa
Fahari Huduma (Malinyi SACCOS na Zidua Waziri Shop) zinazoendeshwa na
benki ya ‘CRDB Bank’ ambapo wateja wanapata huduma za kibenki ikiwemo
kufungua akaunti, kuweka na kuchukua fedha, kuomba mikopo na kupata
ushauri wa huduma za kifedha.
“Gharama
za kuanzisha na kuendesha tawi kuwa kubwa Benki ya NMB na CRDB
zinaendelea na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kufungua tawi katika
wilaya ya Malinyi utakaotoa mwelekeo wa kufungua tawi au la, kwa sababu
Tawi linatakiwa liwe endelevu na kujiendesha kwa faida”. Alisema Dkt.
Kijaji.
Dkt.
Kijaji aliongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa wananchi wa Tanzania
kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao na kwamba huduma hizo
lazima ziwe na faida kwa pande zote yaani kwa mabenki na wateja pia.
Aidha
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa mabadiliko ya mfumo wa fedha nchini ya mwaka
1991, yaliitoa Serikali katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli
za mabenki nchini ili kuruhusu ushindani huru na kuwezesha kuboresha
huduma katika sekta ya fedha.
Katika
swali la nyongeza Mbunge wa Malinyi Dkt. Hadji Hussein Mponda (CCM),
alitaka kujua namna Jeshi la polisi linavyoweza kuwasaidia wakazi wa
wilaya hiyo wanaotembea na fedha nyingi kufuata huduma za kibenki mbali
na wilaya hiyo ili wasipoteze mali zao.
Akijibu
swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba
amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usalama katika maeneo hayo
ili kuweka ushawishi kwa Taasisi za kifedha kuweza kufungua mabenki ili
kupunguza changamoto ya huduma za kibenki.
Post a Comment