Baada ya kamati ya uchunguzi wa makinikia ya madini kutoa ripoti yake
juzi, wengi wanaona kuwa Tanzania imekuwa ikiibiwa kiasi kikubwa cha
fedha tangu usafirishaji mchanga wa dhahabu ulipoanza takriban miaka 20
iliyopita.
Wako wanaosema kuwa kiwango hicho cha fedha kinachotokana na kati ya
tani 7.8 hadi 15 za madini yaliyo katika makinikia hiyo, kingeweza hata
kutosheleza mahitaji ya bajeti ya mwaka.
Lakini kwa mujibu wa kanuni za uchimbaji madini, stahiki ya nchi katika madini haiwezi kuzidi asilimia 10 ya mrabaha.
Kamati iliyoundwa na Rais ambayo iliongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma,
ilisema imebaini kuwa kampuni ya Acacia, ambayo inaendesha migodi
mitatu nchini, haikutangaza madini yote yaliyomo kwenye mchanga huo
uliozuiwa bandarini na kwamba kiwango cha dhahabu iliyomo ni kubwa zaidi
ya kilichotangazwa.
Wachimbaji wa madini wenye leseni pamoja na kulipa kodi nyingine kwa
Serikali kama za mapato na kampuni, hutakiwa na Sheria ya Madini ya
Mwaka 2010 kulipa mrabaha.
Mrabaha ni malipo yanayofanywa na kampuni inayochimba madini kama fidia
ya kiuchumi inayolipwa kwa Serikali kutokana na kuchimba rasilimali zake
ambazo hazina mbadala.
Kwa mujibu wa kifungu 87(1) wachimbaji wa urani, almasi ghafi na vito
ghafi wanatakiwa kulipa mrabaha wa asilimia tano huku kwa madini kama
dhahabu, shaba, fedha na platina wakitoa asilimia nne ya thamani ya
madini yote.
Madini mengine ya ujenzi kama mchanga, mawe, chokaa hutakiwa kulipiwa
mrabaha wa asilimia tatu wakati vito vilivyokatwa na kuchongwa
vikilipiwa asilimia moja.
Matokeo ya kamati yanaonyesha kuwa thamani ya madini yote yaliyopo
kwenye makontena 277 ni kati ya Sh829.4 bilioni hadi Sh1.439 trilioni.
Iwapo hesabu ya asilimia nne ya mrabaha itapigwa kwa thamani ya chini
iliyoanishwa na kamati ya Sh829.4 bilioni kwa kuzingatia dhahabu, fedha
na shaba zina thamani kubwa kuliko madini mengine yaliyoanishwa, basi
Serikali ilitakiwa ipate Sh33.17 bilioni.
Ripoti ya kamati ya Profesa Mruma ilijumuisha hesabu za madini yote
yenye thamani katika makontena hayo yakiwemo yale ya kimkakati kama
lithium inayotumika zaidi duniani kutengeneza betri za vifaa vya
kielektroniki kama simu za mkononi.
Na iwapo asilimia hiyo nne itapigwa kwa kiwango cha juu cha thamani ya
madini hayo cha Sh1.439 trilioni, Serikali ilitakiwa ipate mrabaha wa
Sh57.56 bilioni.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa nyaraka zilizotolewa na wazalishaji
zilionyesha makontena hayo yalikuwa na dhahabu tani 1.1 yenye thamani ya
Sh97.5 bilioni.
Lakini Acacia katika moja taarifa zao za hivi karibuni juu ya ufafanuzi
kuhusu makinikia wanaeleza kuwa kontena moja la tani 20 lina thamani ya
wastani wa Sh310 milioni. Hii ina maana kuwa mzigo wote uliomo kwenye
makontena 277 una thamani ya Sh85.87 bilioni.
Post a Comment