Bunge
limeelezwa kuwa, Wizara ya Nishati na Madini inahitaji Sh2 bilioni kwa
ajili ya kusambaza gesi majumbani katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar
es Salaam.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema jana kuwa,
mradi wa usambazaji gesi unaweza kukamilika ifikapo mwezi Julai.
Dk
Kalemani alitaja kiasi kamili cha gesi kinachohitajika kwenye nyumba za
watu katika mikoa hiyo ni mita za ujazo kati ya milioni tano hadi 10
ambazo uwezekano wa kupatikana ni mkubwa kwa kuwa gesi ipo ya kutosha.
Naibu
waziri huyo alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtwara Mjini
(CUF), Maftaha Nachuma aliyetaka kujua kiasi na gharama zitakazotumika
kwa ajili ya usambazaji majumbani.
Katika
swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua ni lini Serikali itasitisha
usafirishaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Kinyerezi Dar es Salaam, ili
wananchi wa Mtwara waweze kunufaika kwanza na ajira zitokanazo na
uchakataji wa gesi hiyo asilia na kujenga viwanda.
Hata
hivyo, naibu waziri alisema sera mpya ya nishati ya mwaka 2015 na Sera
ya Gesi ya mwaka 2013 zinalenga kutoa fursa ya gesi asilia kuwanufaisha
Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na wananchi wa eneo inakopatikana
rasilimali hiyo.
Alisema
kuna miradi miwili inayosafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi
hadi Dar es Salaam. Dk Kalemani alisema mradi mmoja ni mpya
unaosafirisha gesi kutoka Mtwara ambao ulikamilika mwaka 2015, huku
mwingine ni wa Songas uliokamilika mwaka 2004 wakati gesi inayochakatwa
Madiba, Mtwara inasafirishwa kwa bomba kwenda Mkuranga.
Alisema
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
inatekeleza mradi wa kuunganisha gesi hiyo katika Kiwanda cha Dangote
kilichopo Mtwara ambacho kitahitaji takriban futi za ujazo 45 milioni.
Post a Comment