Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba amewataka maofisa na
askari Polisi kote nchini kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu ili
kujenga taswira nzuri kwa wananchi wanaowahudumia jambo ambalo
litaongeza imani na ushirikiano katika kukomesha vitendo vya uhalifu
nchini.
Waziri
Nchemba ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua kikao kazi cha
Maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu, Makamanda wa Polisi
wa Mikoa na vikosi kutoka bara na Zanzibar kinachoendelea mkoani
Dodoma.
Alisema
Pamoja na Jeshi hilo kufanya kazi nzuri bado linakabiliwa na changamoto
ya baadhi ya askari na maofisa wasio waadilifu wanaofanya vitendo vya kuwabambikia
wananchi kesi na wakati mwingine kuwabadilishia kesi ili kujenga
mazingira ya kupatiwa rushwa jambo ambalo ni kinyume na maadili ya
askari Polisi.
“Fanyeni
kazi kwa weledi hasa kwa kuwasimamia waliopo chini yenu kwa kuwa wapo
baadhi yao bado hawataki kubadilika na katika awamu hii lengo letu ni
kutoa haki kwa maskini hivyo ninyi kama wasimamizi wa sheria mnapaswa
kutenda haki mnapofanya kazi zenu na wale wasiotaka kubadilika hamna
budi kuchukua hatua ” Alisema Nchemba.
Aidha
alilitaka Jeshi hilo kuwachukulia hatua bodaboda wanaofanya makosa na
wale wasiokuwa na makosa waachwe waendelee na majukumu yao ya kujipatia
kipato na kuachana na dhana ya kuwa kila bodaboda ni mhalifu.
Kwa
upande wake Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Ernest Mangu alisema kikao
hicho kinafanyika kwa siku tatu kwa lengo la kufanya tathmini ya
utendaji kazi kwa mwaka uliopita na kuweka mikakati kwa mwaka huu ili
kuendeleza juhudi za kukabiliana na vitendo vya uhalifu hapa nchini.
Mangu
alisema Jeshi hilo litaendelea na Oparesheni zake za kupambana na
uhalifu zikiwemo za dawa za kulevya, uhalifu wa kutumia silaha na wizi
wa mtandao kwa mikakati mipya ambayo itaibuliwa katika kikao kazi hicho
ili kuhakikisha hakuna mhalifu anayetamba hapa nchini.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge mambo ya nje na usalama Balozi
Adadi Rajabu alisema kamati hiyo itaendelea kuishawishi Serikali
kuboresha maslahi na vitendea kazi vya Jeshi la Polisi ili Jeshi hilo
liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Ufunguzi
wa Kikao kazi hicho ulihudhriwa pia na Waziri Mkuu mstaafu Samweli
Malechela, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana pamoja na baadhi ya
wabunge na Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dodoma.
Post a Comment