Rais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashim Rungwe Spunda
amemshauri Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kujitokeza
hadharani na kutoa ufafanuzi juu ya utata wa jina lake unaozidi kuvuma
mitandaoni
Utata huo unadaiwa kutokana na mkuu huyo wa mkoa kutumia cheti cha mtu mwingine cha kidato cha nne kujiendeleza kielimu.
Rungwe ametoa ushauri huo kupitia kipindi cha maswali na majibu cha
Kikaangoni , akimsisitiza Makonda kuweka ukweli mezani na kuacha kupiga
chenga za mchangani kwa maana akiendelea kukaa kimya watu wanazidi
kuamini uvumi huo.
"Namshauri Mkuu wa mkoa ambaye ni kama mwanangu, atoke azungumze ili
kumaliza huu utata wa vyeti, asimsumbue Rais ana mambo mengi" Amesema
Rungwe
Pia, amemtaka kuacha kulia madhabahuni, kwakuwa hilo halitamsaidia kwa
kuwa kulia siyo jibu, na atambue kuwa ofisi hiyo aliyopo sasa siyo yake
bali ni wananchi, hivyo kila alichokikuta atakiacha.
"Siku moja nafungua 'ipad' yangu namuona Mkuu wa Mkoa analia mbele ya
kanisa halafu mchungaji anambembeleza kama mjukuu wangu, mimi namwambia
kulia kwake hakusaidii kitu yeye anapaswa kusema ukweli tu kama hilo
jina siyo la lake halisi ila ni la kisanii sisi tutamuelewa". Alisema
Rungwe
Kwa upande mwingine, Rungwe ambaye ni wakili msomi, ametoa ushauri wa
kisheria kwa watu wenye ushahidi na suala hilo kwenda mahakamani kwa
kuwa sheria inaruhusu mashtaka binafsi, ingawa bado Jamhuri itahitajika
zaidi kuisimamia kesi hiyo.
Aidha Rungwe aliendelea kufunguka kwa kumtaka Makonda kuacha
kung'ang'ania nafasi ambazo anastahili katika nafasi hiyo huku akimpiga
kijembe kuwa mwanaume hachagui kazi aende akabebe hata zege kama hana
ujuzi wa kufanya.
Kwa upande mwingine Mzee Spunda amemuomba Rais Magufuli kuliingilia kati
suala hilo kama alivyofanya kwa maafisa wengine wa serikali.
Rungwe alilazimika kutoa ushauri huo kutokana na swali aliloulizwa
kuhusiana na maoni yake kuhusu vita dhidi ya dawa kulevya ambapo amesema
kuwa anaunga mkono vita hiyo, isipokuwa njia iliyotumika ya kutaja
majina ya watu hadharani bila uhakika, haikuwa nzuri.
Post a Comment