WATU wanne wakiwamo watatu wa familia moja ambao ni wakazi wa Kijiji cha
Isighu kitongoji cha Majumba Sita wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma
wamekufa maji baada ya makazi yao kusombwa na mvua iliyonyesha usiku wa
kuamkia Januari 31.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa wilayani hapa, Dk Said Mawji amekiri kupokea miili ya watu wanne na majeruhi wawili.
Dk Mwaji aliwataja waliokufa kuwa ni Maritha Mabula (60), Shukuru Donald
(15) mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwana
Kianga na Bernadeta Mabula(7) mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya
Msingi Ilolo na mwingine ni Jeska Lubeleje (19) mkazi wa Kijiji cha
Chinyika katika Kata ya Vighawe.
Aliwataja majeruhi wawili waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ni Beka Mlami
na Joseph Sumisumi. Aidha, alisema kwamba majeruhi wametibiwa na
kuondoka.
Alieleza kuwa katika ajali hiyo, mmoja wa watoto walionusurika na kifo
Beca Mrami (10), alisema maji yaliingia ndani ya nyumba na akalazimika
kukimbilia darini na ndugu yake, lakini walipoona yamezidi walikimbia
wakimwacha bibi yao na dada zake.
“Mimi nilipoona maji yanazidi nikawaambia tukimbie, lakini bibi na akina
dada walibaki ndani; mimi na Mandili (Joseph Sumisumi ) tulipanda juu
ya paa baada ya nyumba kuanguka nilikimbia na kuwaacha ndani,” alieleza
mtoto huyo.
Mzee wa kaya hiyo, Mabula Sumisumi, alisema hakuwapo katika mji huo siku
hiyo alienda kulinda mifugo kambini ndipo alipoambiwa familia yake
imesombwa na maji.
Hata hivyo, Sumisumi alisema kila kitu kilichokuwamo ndani kimesombwa na
maji ikiwamo akiba ya chakula na fedha kiasi alizokuwa amehifadhi ndani
ya nyumba ambazo hakuzitaja kiasi chake.
Shuhuda wa tukio hilo, Simon Kazimoto alisema nyumba hiyo imesombwa
kutokana na kuwa ilijengwa kwenye mkondo wa maji na kutokana na
uharibifu wa mazingira unaoendelea umesababisha maji kutawanyika na
kuingia katika makazi ya watu na kusababisha vifo.
Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Said Kilungo alisema kwa hatua za
awali zilizochukuliwa na serikali ni kuhifadhi maiti kwa kugharamia
jeneza na sanda kwa kila maiti baada ya hapo hatua zaidi zitafuata.
Kilungo aliwataka wananchi wa kitongoji hicho kuhama katika maeneo
hatarishi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa sasa.
Pamoja na mvua hiyo, kusababisha vifo vya watu wanne, lakini tayari
baadhi ya miundombinu ya Wilaya ya Mpwapwa iko hatarini kusombwa na
maji, ikiwamo daraja la Tanesco na daraja la kwenda Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya.
Post a Comment