MSHAHARA wa Rais Uhuru Kenyatta na ule wa makamu wake William Ruto
utaongezeka kwa asilimia 10 katika mwaka wa fedha wa kuanzia mwezi Julai
katika kipindi ambacho serikali ya Kenya imekuwa ikijaribu kupunguza
mzigo mkubwa wa mishahara kwa wafanyakazi wake.
Nyaraka za wizara ya fedha nchini humo zinaonyesha kwamba kwa pamoja
mishahara yao kwa mwaka itaongezeka na kufikia shilingi za Kenya milioni
40.2 (sawa na shilingi za Kitanzania milioni 867) kuanzia mwaka wa
fedha wa 2017/18 kutoka wa sasa wa shilingi milioni 36.6 (ambayo ni sawa
na shilingi za Kitanzania milioni 789.36).
Lakini posho zao hazitofanyiwa mabadiliko na zitabakia shilingi milioni 14.6 (sawa na shilingi za Kitanzania milioni 314.7).
Mwaka jana wawili hao walipata ongezeko la asilimia 9.1 la mshahara
pamoja na tangazo lao la mwaka 2014 kwamba walipunguza kiasi cha
mshahara wao kwa asilimia 20 ili kukabiliana na mzigo mkubwa wa
mishahara.
Hata hivyo ongezeko hilo la mshahara litapitishwa iwapo tu wawili hao
watachaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo katika uchaguzi mkuu wa Agosti
mwaka huu.
Iwapo watashindwa katika uchaguzi huo, mrithi wao ataanza na mshahara wa chini kulingana na matakwa ya tume ya mishahara.
Kiasi cha jumla cha mshahara wa kuanzio kwa rais na makamu wake inakadiriwa kuwa ni shilingi milioni 2.7 za Kenya.
Ongezeko hili jipya la mshahara linakuja wakati wizara ya fedha
ikipambana kutekeleza mpango wa kudhibiti matumizi ya fedha ili kupata
fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na huduma muhimu kama usalama,
afya na elimu.
Mshahara wa Rais Kenyatta kwa mwezi ni kati ya shilingi milioni 1.23
(sawa na shilingi za Tanzania milioni 26.5) na milioni 1.65 kwa mwezi,
ikimaanisha kwamba kiwango cha juu cha shilingi milioni 19.8 (sawa na
shilingi za kitanzania milioni 426.6) kwa mwaka kabla ya makato,
kulingana na Tume ya Mishahara na Posho nchini humo.
Ruto anapokea kiasi cha shilingi milioni 1.05 (sawa na shilingi za
kitanzania milioni 22.6) kwa mwezi na jumla ya shilingi milioni 16.8
(sawa na shilingi 361.9) kwa mwaka.
Mwaka jana wizara ya fedha nchini humo ilisimamisha ongezeko la mshahara
kwa Rais na makamu wake kwa miaka miwili hadi mwaka 2018 kama sehemu ya
kupunguza matumizi nchini humo.
Bado haifahamiki ni kitu gani kimesababisha kubadili mawazo.
Kenya imekuwa na mzigo mkubwa wa mishahara ambao hadi Juni 2015, malipo
ya mishahara yalikuwa yanafikia asilimia 52 ya makusanyo yote ya fedha,
kiasi cha kupunguza matumizi katika miradi ya maendeleo ambayo ndiyo
hasa yanayochangia ukuaji wa uchumi.
Kiasi hicho cha asilimia 52 cha Kenya kwa mishahara, kipo juu kwa
asilimia 17 kikilinganishwa na wastani wa dunia katika nchi zenye
kipato cha kati.
Wiki iliyopitam Ikulu ya nchi hiyo ilitangaza viwango vipya ambavyo
vitashuhudia mishahara ya wafanyakazi wa serikali vikiongezeka.
Viwango hivyo vitaongezeka kutoka kutoka shilingi bilioni 568 cha mwaka huu wa fedha hadi kufikia shilingi bilioni 658.
Hili linakuja katika mwaka ambao kiwango cha ukuaji wa uchumi
kinatarajiwa kupungua huku wawekezaji wakisubiri na kutazama hali ya
mambo kabla ya uchaguzi wa Agosti, kulingana na taarifa ya Shirika la
Fedha Duniani IMF.
Post a Comment