BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwanasiasa mkongwe na Waziri wa Maji
mstaafu, Profesa Mark Mwandosya, anatarajiwa kuibuka katika maadhimisho
ya Siku ya Nile, leo hii.
Profesa Mwandosya ametajwa kuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika
maadhimisho hayo ya yatakayofanyika jijini Dar es Salaam yakihusisha
mawaziri wa maji wa nchi 10 wanachama wa Bonde la Mto Nile, ambapo
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.
Ushiriki wa Profesa Mwandosya katika mkutano huo unatajwa kuwa tukio la
kwanza la hadhara tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015 alipojaribu
kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini kura za maoni
hazikutosha.
Hivyo Profesa Mwandosya anatarajiwa kuvuta hisia za wengi, hasa baada ya
kukosekana kwenye majukwaa ya kisiasa na kijamii tangu mwaka juzi.
Katika maadhimisho hayo, mambo mbalimbali yanatarajiwa kujadiliwa
ikiwamo umuhimu wa Mto Nile katika kuzipatia nchi wanachama maji,
chakula na umeme wa uhakika.
Mahitaji hayo yatatolewa kupitia miradi endelevu tofauti inayofaidisha
nchi wanachama kupitia rasilimali zake chini ya Taasisi Inayosimamia
Shughuli za Nile (NBI).
Naibu Mkurugenzi wa Maji katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji inayoandaa
maadhimisho hayo, Sylvester Matemu alisema Profesa Mwandosya amepewa
nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake na utaalamu katika sekta ya maji.
Pia Matemu alisema Profesa Mwandosya amefanya utafiti na kuandika kitabu kuhusu Mto Nile.
“Pamoja na Mwandosya, mawaziri wote wa maji kutoka nchi wanachama
watazungumza katika maadhimisho hayo ya kihistoria,” alisema Matemu
katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho
hayo mwishoni mwa wiki.
Alisema maadhimisho hayo yatafanyika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu
Nyerere ukishuhudia pia upandaji miti, ambao utatanguliwa na maandamano
yatakayoanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa NBI, Mhandisi Innocent Ntabana alisema
madhimisho ya siku hiyo alitaja nchi wanachama kuwa ni Tanzania, Kenya,
Uganda, Sudan, Sudan Kusini na Kongo.
Nyingine ni Ethiopia, Burundi, Rwanda na Misri ambapo Ntabana alieleza
kwamba maadhimisho hayo yatatumika pia kama jukwaa la majadiliano kwa
nchi hizo kuhusu rasilimali maji ya Mto Nile, mikakati ya kuifanya
endelevu na kukabili changamoto za kimazingira zilizopo ili liendelee
kuhudumia mamilioni ya watu wanaotegemea mto huo.
Profesa Mwandosya amekuwa kimya kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu
kumalizika kwa mchakato wa kutafuta mgombea urais ndani ya CCM mwaka
2015, ambapo wagombea zaidi ya 35 akiwamo yeye walijitokeza na kuchujwa
hatua za awali.
Hali hiyo iliyozua malalamiko kutoka baadhi ya wajumbe hata baadhi
kuamua kujitoa CCM akiwamo Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa
aliyehamia Chadema.
Katika mchakato huo, Rais John Magufuli alipitishwa kabla ya kuchaguliwa
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30 mwaka jana akimshinda mpizani wake wa
karibu, Lowassa.
Lowassa aliwania nafasi hiyo kupitita Chadema na kuungwa mkono na vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa).
Mara kadhaa gazeti hili limekuwa likimtafuta Mwandosya aliyewahi kuwa
Waziri wa Maji na Umwagiliaji katika Serikali ya Awamu ya Nne na pia
Waziri Asiye na Wizara Maalum ili kupata maoni yake kuhusu masuala
mbalimbali lakini mara azote simu yake imekuwa ikiita bila kupokelewa.
Ukimya wa Profesa Mwandosya ulizua maswali mengi, lakini Desemba mwaka
jana alipopigiwa simu na gazeti hili ili kuzungumzia pamoja na mambo
mengine mwaka mmoja wa Serikali ya Rais ya Awamu ya Tano na CCM, alisema
hana cha kusema.
“Mimi nipo kijijini kama unataka kujua masuala ya kijijini kwangu
niulize hayo ya mwaka mmoja wa Magufuli na CCM sina ‘coment’ kwa sasa
nafanya shughuli zangu kijijini na kupumzika,” alisema.
Mwandosya anatajwa kama moja ya viongozi waliofanya kazi kwa mafanikio
huku akionesha utulivu na kujiamini kwa kila jambo hasa bungeni ambapo
alikuwa akitumia msemo wa kisomi kwa kuwataka wabunge watoe hoja na si
kufoka katika jambo wasilolijua.
Post a Comment