Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino
Mokiwa amejibu tuhuma mbalimbali zikiwamo za wizi wa fedha
zilizoelekezwa kwake, akidai ni uzushi wenye lengo la kumchafua ili
aondolewe kwenye nafasi hiyo.
Mbali ya kujibu tuhuma hizo, Dk Mokiwa amedai mgogoro huo umezushwa
kutokana na hofu ya uchaguzi wa askofu mkuu mpya mwakani na uongozi wa
kutojiamini wa Askofu Mkuu, Dk Jacob Chimeledya.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika ofisini kwake kujua kiini
cha mgogoro katika kanisa hilo ambao umesababisha Dk Chimeledya
kumwandikia barua akimtaka ajiuzulu, Dk Mokiwa alisema mzozo uliopo
katika kanisa hilo umetengenezwa na ‘wakubwa’ kwa kuwatumia mapadri
wawili waliofukuzwa utumishi katika dayosisi ambao waliandaa mashtaka
ili aonekane kuwa hafai na aondolewe.
“Ili niondoke, wakatengeneza mashtaka 10 wakitumia mapadri wawili ambao
bahati mbaya nimewaondoa kwa utovu wa nidhamu,” alisema. “Kila shtaka
lililotengenezwa dhidi yangu linafurahisha, linasikitisha, linachekesha
kwa sababu malengo yake ni hatimaye Mokiwa aondolewe. Haya Askofu Mkuu
wangu, Dk Chimeledya ameyaamini, ameyafanyia kazi, anaamini kabisa
kwamba Mungu, Roho Mtakatifu amemtuma na huduma yake ya uaskofu mkuu
itakuwa nzuri ikiwa mimi nitaondolewa kwa mashtaka hayo.”
Akijibu tuhuma moja baada ya nyingine kadri ilivyoandikwa katika
mashtaka aliyopelekewa na Dk Chimeledya, Dk Mokiwa alisema: “Kuna shtaka
eti nimezuia michango isiende jimboni. Hii ina sababu yake, kuna sheria
katika katiba yetu inazuia dayosisi moja isivuke mipaka kwenda kufanya
kazi katika dayosisi nyingine. Hapa kuna mwenzetu ametoka huko kwake
anakuja kufungua makanisa hapa. Ni ukiukwaji wa katiba tu.”
Alitaja shtaka la pili kuwa ni madai ya kuitoa Dayosisi ya Dar es Salaam
katika udhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania. Shtaka hilo linatokana
na hoja ya dayosisi kutaka kutumia viwanja vyake katika uwekezaji na
kwamba kiwepo kifungu cha kuwa na majadiliano katika uwekezaji huo.
“Hapa wanamaanisha kwamba nilitaka kujitenga niwe mwenyewe. Hata kama
ningekuwa nimekula dawa fulani haiwezekani kwa sababu hii siyo taasisi
yangu, kama ni kweli nataka kufanya hivyo basi nianzishe kanisa langu na
mke wangu anifanye kuwa askofu,” alijibu.
Kuhusu ufujaji wa mali na kuingia mikataba mibovu, alisema havipo na
kama ni mikataba iliamuliwa na sinodi na kamati ya dayosisi na kwamba,
chombo hicho kina uwezo wa kurekebisha kama kuna makosa na tayari
kimetengeneza kamati ya kupitia mikataba hiyo.
Ingawa mashtaka yalionyesha kuwa Dk Mokiwa alifuja mali za dayosisi,
ushahidi wa nyaraka na taarifa za fedha za benki aliouweka wazi
unaonyesha mapadri wawili walihusika katika akaunti zilizopo kwenye
Benki ya Maendeleo, ACB (Benki ya Biashara ya Akiba) pamoja na DCB (Dar
es Salaam Commercial Bank) iliyopanga katika jengo la dayosisi hiyo
lililopo Magomeni.
Dk Mokiwa alisema kuna miamala inayoonyesha fedha zilikuwa zinaingizwa
ACB tawi la Buguruni na kuna nakala za hundi zinazoonyesha fedha
zikichotwa na kuingizwa kwenye akaunti binafsi za mapadri hao.
Alisema tangu aanze kazi kwenye dayosisi hiyo ameboresha taasisi alizozikuta na kuanzisha nyingine mpya ili kuinua mapato.
“Sipigi vita mafanikio, nataka maendeleo. Sijisifu ila kanisa hili
nimelitoa kimasomaso. Sema tu nabii haheshimiki kwao,” alisema.
Dk Mokiwa alisema ushahidi kwamba mgogoro huo unapaliliwa na wakubwa ni
baruapepe aliyodai kiongozi mmoja wa ngazi za juu alimwandikia mmoja wa
mapadri waliofukuzwa Desemba 16, 2016 akimjulisha kuhusu tume iliyotumwa
kumhoji Dk Mokiwa na kwamba timu nyingine inatumwa kwa ajili ya kazi
hiyo.
Mwezi uliopita, Dk Chimeledya alisambaza waraka kwa makanisa ya
Anglikana Dar es Salaam uliomtaka Dk Mokiwa kujiuzulu kutokana na tuhuma
mbalimbali. Hata hivyo, askofu Mokiwa ameutaka uongozi wa Anglikana
Taifa kufuata Katiba.
Post a Comment